UKUAJI wa uchumi nchini hautawasaidia watanzania kutoka kwenye lindi la umaskini
iwapo njia mbadala hazitachukuliwa
kudhibiti rushwa na uhusiano
usiosawia baina ya serikali na sekta
binafsi, imeelezwa.
Wakichangia mada kuhusu wajibu wa sekta binafsi katika kupunguza umaskini
Jijini Dar es salaam juzi, wadau mbalimbali wa maendeleo walisema kuwa jitahada
za Tanzania kukuza uchumi wake hazitakuwa na msaada wowote kwa Watanzania
katika kupunguza umaskini iwapo rushwa na uhusiano hasi baina ya Serikali na sekta
binafsi havitaondolewa.
Walisema kuwa uhusiano uliopo baina ya Serikali na sekta
binafsi hauna usawa kwani sekta binafsi imekuwa na nguvu nyingi kuliko Serikali
na kusababisha malengo na jitaha za
Serikali kupunguza umaskini nchini kutofikiwa ipasavyo.
Akizungumza katika mdahalo huo Afisa Mtendaji wa Taasisi ya kimataifa isiyo ya Kiserikali ya VSO Marg Mayne alisema kuwa taarifa ya Benki ya Dunia
inaonyesha Uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi lakini ukuaji huo umeshindwa
kuwakomboa Watanzania wengi hususani waishio vijijini kutoka kwenye lindi la
umaskini bali umeongeza tofauti kati ya maskini na matajiri.
Aliongeza kuwa ugunduzi wa gesi na mafuta nchini unaotarajia
kukuza uchumi wa nchi kwa aslimia 6.5 hadi 7 hautaleta mabadiliko yoyote iwapo
mfumo wa sasa wa uhusiano baina ya serikali na sekta binafsi hautavunjwa.
Alishauri uanzishwaji wa ushirikiano wa kina na ushawishi
uliosawa baina ya wadau wa maendeleo na sekta binafsi ambao utaenda mbele zaidi
ya sera ya Wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR) ili kuongeza mchango mkubwa wa
makampuni katika jitahada za kupambana na kupunguza umaskini nchini.
Rananie Kunanayagam, Mkuu wa Utendaji wa Jamii Kampuni ya BG
group alisema ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi si jambo jipya duniani kwani
lilishakuwepo miaka 15 hadi 20 iliyopita katika nchi nyingi zinazoendelea
ikiwemo Tanzania lakini umaskini bado upo palepale hivyo anahitajika mtu wa
kusimamia uhusianobaina ya Serikali na
sekta binafsi.
“Kunahitajika uwepo wa mtu au taasisi katikati ya Serikali na
Sekta binafsi ambaye hatang’ata upande wowote na kuwashawishi wote kutekeleza
majukumu yao kwa usahihi” alibainisha Kunanayagam.
Mshiriki wa mdahalo wa kujadili wajibu wa Sekta binafsi katika jitahada za kupunguza umaskini nchini akitoa maoni juu ya mada hiyo juzi katika ukumbi wa British Council.Jijini Dar es salaam juzi. |
Naye Mkurugenzi Mkazi wa UNDP nchini Phillipe Poinsot alisema
kuwa lazima kuwe na mgawanyo sawa wa wajibu baina ya Serikali na sekta binafsi
katika kupambana na umaskini na pia Serikali izidishe uhusiano ndani ya Sekta
binafsi.
Alisema kuwa Serikali ihakikishe inatengeneza miundombinu na
mazingira rafiki kwa sekta binafsi kwa kutengeneza barabara safi, umeme wa uhakika,
sheria thabiti, usimamizi mzuri wa rasilimali,
wasomi na viongozi makini
wasiopenda rushwa wakati huohuo sekta
binafsi ina wajibu wa kutoa kodi halali, uwazi katika uendeshaji, kuendeleza
teknolojia na kutoa ajira stahiki kwa Watanzania.
Mjumbe wa Mdahalo huo Semkai Kilonzo alisema uwepo wa
miongozo mingi inayohusika na jitahada za kupunguza na kupambana na umaskini kama
MKUKUTA, Dira ya 2025, Kilimo Kwanza na mingine ni chanzo kikubwa cha ukuaji wa
uchumi nchini kushindwa kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye lindi la umaskini.
“Uwepo wa Miongozo mingi kwa wakati mmoja kama MKUKUTA, Mkurabita, Kilimo Kwanza
kunachanganya Wadau wa maendeleo na pia imekuwa haina ushirikishwaji wa
Wananchi katika kufanya maamuzi ya maendeleo yao hivyo inashindwa kupata
ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau” alisema Kilonzo.
Mdahalo huo Uliandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya VSO
International ikishirikana na BG Tanzania na British Council ambapo wadau
walitaka rushwa itokomezwe, uwazi wa
utendaji katika makampuni na serikali, kuanzishwa kwa sera na sheria inayotoa
kiwango na aina za miradi inayoweza kufanywa na makampuni katika Sera ya Wajibu
wa Kampuni kwa Jamii (CSR).