Tuesday, July 10, 2012

Njia za kutatua Migomo Vyuo Vikuu Tanzania hizi hapa.

MAONI YANGU KWA UTAWALA WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM JUU YA NAMNA YA KUONDOA AU KUPUNGUZA MIGOMO NA MAANDAMANO YANAYOONEKANA KUONGEZEKA KILA KUKICHA.
Na: Ole Mesaya

Tatizo la migomo na maandamano ndani ya chuo kikuu cha Dar es salaam halijaanza hivi karibu. Tatizo hili lilikuwepo toka enzi lakini kwa miaka ya hivi karibuni limeonekana kushika kasi zaidi na kupelekea chuo kupoteza rasilimali nyingi na kuwatimua chuo wanafunzi wote ambao wanaonekana kuwa ni chanzo cha tatizo hili. Pamoja na jitihada zote hizi zinazofanywa na uongozi wa chuo bado tatizo hili limeonekana kutokoma, zaidi wanafunzi wengi wanazidi kupotea na rasilimali nyingi zinatokomea bila mafanikio.

Ningependa kuchukua nafasi hii kama mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam kutoa maoni yangu juu ya nini kifanyike ili kupunguza kama sio kutokomeza kabisa suala la migomo ndani ya chuo chetu.
I. Kwanza kabisa Chuo pamaja na taasisi zinazohusika zijitahidi kukabiliana na kutatua matatizo yanayowakabili wanafunzi kwa njia ya majadiliano na kwa haraka zaidi na siyo kusubiri mpaka mgomo au maandamano kutokea. Tofauti na ilivyo sasa hivi, ambapo taasisi zinazohusika zinasubiri mpaka mgomo utokee ndipo wachukue hatua za kukabiliana na mgomo badala ya kuchukua hatua hizo kukabiliana na matitizo hayo kabla mgomo haujatokea.

II. Chuo kiangalie zaidi na kijikita kwenye vyanzo vya migomo, ikiwa ni pamoja na sababu ya mgomo kutokea kuliko kujikita na kuwapa adhabu wanafunzi wanaoanzisha na kushiriki kwenye mgomo huo. Kwa kufanya hivyo chuo kitakuwa kimezuia uwezekano wa mgomo mwingine kutokea kuliko ilivyo sasa ambapo chuo kinawapa adhabu, ikiwepo kuwafukuza chuo wanafunzi wanaooekana kushiriki kwenye mgomo ilihali tatizo lilosababisha mgomo likibaki bila muafaka.

III. Chuo kiweke utaratibu ambao utawalazimu viongozi wa serikali ya wanafunzi kukutana na wanafunzi na kujadili kwa pamoja juu ya matatizo na changamoto zinazowakabili wanafunzi angalau mara tatu kwa muhula wa masomo yaani mwanzo, katikati na mwishoni mwa muhula wa masomo. Tofauti na ilivyo sasa ambapo school baraza ipo mara moja tu kwa mwaka na mara nyingi imekuwa haifanyiki. Kwa kufanya hivi wanafunzi wataweza kuwasilisha changamoto zinazowakabili kwa uongozi wao na hoja hizo kuwasilishwa panapohusika haraka na mapema zaidi.

IV. Chuo kikuu kifanywe kitovu cha kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili nchi yetu. Hii itawezekana kama chuo kitaweka utaratibu wa kuruhusu jukwaa la malumbano ya hoja baina ya wanafunzi angalau kila jumamosi ya mwisho wa wiki, kwani hii itawapa nafasi vijana na wasomi wa vyuo vikuu kushiriki katika harakati za kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi yetu. Kwa kufanya hivyo chuo kitakuwa kimeondoa uwezekano wa wanafunzi kufanya mikutano isiyo ya halali kama ilivyo sasa kujadili mwenendo na hatma ya taifa letu.

V. Ilivyo sasa, Chuo kinatumia rasilimali na nguvu nyingi kupambana na wanafunzi. Kwa kufanya hivi Chuo kitakuwa kinapambana na wahanga wa tatizo huku tatizo likiendelea kushamiri na kunawiri pasipo kutafutiwa ufumbuzi wa kuliondoa tatizo lenyewe. Kwa maoni yangu chuo kingetumia nguvu hizo na rasilimali hizo kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi, kwani kama wataendelea kupambana na wanafunzi na kuliacha tatizo likiendelea kukua ni dhahiri shairi kwamba migomo na maandamano kamwe hayatakwisha kwani chanzo cha mgomo bado kipo na kinaendelea kukua.

VI. Pindi mgomo au maandamano yanapotokea, chuo kijikite zaidi kwenye tatizo lililosababisha mgomo kuliko kukimbilia kuhusisha matatizo yaliyosababisha mgomo na vyama vya siasa. Kwani kufanya hivyo kamwe hakutakuwa na suluhisho la migomo na maandamano, kutokana na kwamba tatizo halisi litakuwa limeachwa kwa kujikita kwenye hoja isiyo ya msingi.

VII. Pindi adhabu inapotolewa na chuo, Chuo kijitahidi kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuondoa malalamiko miongoni mwa wanafunzi pamoja na wale waliopewa adhabu. Kwa mfano wanafunzi wapewe adhabu baada ya kuhojiwa na kusikilizwa ushahidi wao badala ya kufuata hisia na hasira kama ilivyo sasa. 

VIII. Uongozi na utawala wa chuo usikimbie changamoto bali watumie changamoto hizo kama vyanzo vya uwajibikaji. Tofauti na ilivyo hivi sasa, wenye madaraka ndani ya chuo kikuu wanakwepa changamoto zinazowakabili wanafunzi kwa kuogopa kupoteza nafasi zao za madaraka endapo wataungana pamoja na wanafunzi kuwasilisha changamoto hizo panapohusika.

IX. Serikali ya wanafunzi DARUSO iwe chombo huru na kinachotambuliwa na kuheshimiwa na utawala wa chuo kikuu cha Dar es salaam. Ilivyo sasa, serikali ya wanafunzi DARUSO haitambuliwi wala kuheshimiwa na utawala wa chuo kwani katika hatua zote za kinidhamu zilizochukuliwa na utawala wa chuo kwa wanafunzi, serikali ya wananfunzi haijajulishwa kimaandishi. Mfano barua zote za kuwasimamisha na kuwafukuza chuo wanafunzi hakuna nakala yoyote iliyopelekwa kwa serikali ya wanafunzi.
Ni matumaini yangu kwamba kama tutashirikiana kwa pamoja kuyatekeleza haya, siyo siri tutakuwa tumepunguza kama siyo kutokomeza kabisa mianya yote inayosababisha migomo na maandamano na kushusha heshima ya chombo hiki cha umma.

Asanteni.
Maoni haya yamenivutia sana mpaka nimeona niyachapishe hapa ili wahusika waweze kuchukua chochote wanachoona kinafaa kutatua Migomo Vyuo Vikuu nchini hususani Utawala wa Vyuo hivyo na Serikali. Pia serikali za Wanafunzi kama DARUSO, IFMSO, UDOSO na zingine zisome makala hii kujiongeza. maoni haya ni mali ya mwandishi Bwana ole Mesaya pichani juu. Yametolewa toka kwenye Ukurasa wa facebook wa UDSM. Bofya hapa kujiunga

Wednesday, July 4, 2012


Tumehitimu Vyuo Vikuu……….. wapi ajira?
Mwishoni mwa mwezi wa sita na mwezi huu wa saba taasisi nyingi za elimu ya juu zimeanza kutoa wahitimu wa taaluma mbalimbali na katika  ngazi tofauti za elimu toka cheti, diploma, degree na masters. Wanafunzi tuliohitimu ni maelfu kwa maelfu kutoka zaidi Vyuo vikuu 30 na Vyuo vya  mafunzo ya ufundi (Vocational Training Colleges). Kundi lote hili la wahitimu linahitaji ajira katika makampuni binafsi na Serikali huku asilimia ndogo sana ya wahitimu wakipanga kujiajiri. 

Baadhi ya Wahitimu wa Shahada ya Sayansi Siasa na Utawala kutoka  Chuo Kikuu cha Dar es salaam 2009/12 katika picha pamoja baada ya mtihani wao wa mwisho. Picha kwa msaada wa Political Science gradutes 2012 facebook page
Inafahamika wazi kuwa mwajiri mkuu nchini ni Serikali huku sekta binafsi ikichikua asilimia zilizobaki. Pia ifahamike kuwa hata hao waajiriwa katika sekta binafsi hufanya kazi mara nyingi katika sekta isiyo rasmi (informal sectors). Wakati jamii kubwa ikitegemea Serikali itoe ajira kwa wahitimu hawa, Serikali yenyewe imejikuta ikishindwa hata kuwahudumia watumishi waliopo. Matatizo mengi yanayohusu ajira za wafanyakazi wa Serikali yameshuhudiwa kwa muda mrefu likiwemo hili linaloshika Vichwa vya habari hivi sasa la mgomo wa madaktari. Serikali imeshindwa kutoa stahili husika kwa Wafanyakazi wake.


Pia serkali imeweka vigezo vigumu sana ambavyo kwa wahitimu wa sasa na wa mwaka jana hawawezi kuomba kazi. Moja ya vigezo hivyo ni kuwa na cheti halisi cha chuo Kikuu na si Provisional statements au transcripts kama ilivyozoeleka. Pili uzoefu kazini bado ni wimbo usiochuja, bado uzoefu usiopungua miaka kadhaa unasisitizwa. Jambo jingine ni ufinyu wa bajeti ya serikali katika kuongeza ajira. Serikali imekua ikijitetea kuwa haina uwezo kifedha kuajiri idadi kubwa ya Wafanyakazi licha ya kuwa na upungufu mkubwa wa watumishi katika taasisi zake. Jingine ni unamfahamu nani kwenye system ya Serikali ili upate kazi kama humfahamu mtu basi nauli yako imeisha. Je kama hali ndo hiyo maelfu ya wahitimu mwaka huu tutaende wapi?

Kwa upande wa Sekta binafsi,  makampuni mengi hayaajiri idadi kubwa ya watu kwa misingi ya kupunguza gharama za uendeshaji. Idadi ndogo sana ya wahitimu huajiriwa na Sekta binafsi iliyo rasmi kama Benki, Viwandani na Makampuni madogomadogo ya biashara. Pia ifahamike tena kuwa sekta binafsi huchagua kundi Fulani la Wahitimu hasa kwa kuangalia ufaulu na uzoefu kazini. Kwa wahitimu waliowengi uzoefu bado mdogo zaidi ya mafunzo ya vitendo ambayo hupatikana kwa njia ya interns (Practical trainings). Kwa upande wa performance kuna kundi kubwa la wahitimu halina First Class degrees au diploma wanazotaka. Uzito na ugumu wa kozi vimetofautiana kutoka aina Fulani ya masomo kama engineering Vs arts au toka Chuo kimoja hadi kingine kama University of Dar es Salaam Vs Tumaini n.k. Kwa utofauti huu wangapi wataajiriwa?

Kwa upande wa Kujiajiri bado kuna tatizo kubwa. Ni idadi ndogo sana ya wahitimu ambao wana uwezo wa kujiajiri wenyewe. Tatizo sio kuwa hawana uwezo wa kujiajiri kwa kufanya biashara na mambo mengi bali ukata wa kifedha na mfumo wa elimu ni vyanzo vikuu hali hii. Mfumo wa elimu ya bongo unamuandaa mwanafunzi kuajiriwa na si kujiajiri. Mfano mzuri ni pale mtu aliyehitimu VETA anapotafuta ajira. Mfumo huu hauna utofauti na ule wakikoloni wa kuandaa watu kufanya kazi za kuajiriwa maalufu kama white Color Jobs. Jambo jingine ni kukosa kwa mtaji wa kuanzisha biashara. Benki zimekuwa na imani ndogo sana kukopeha wahitimu kwa kuwa hawana dhamana yoyote zaidi ya Cheti na akili tu kichwani.  Pia wengine wanakatishwa tama na urasmu wa kusajiri biashara Serikalini na mfumo mzima wa kodi ambao unaharibiwa na wafanyakazi wenye tabia ya rushwarushwa (rent seeking behavior)
Mimi wa pili kushoto waliosimama na wahitimu wengine baada ya kumaliza mtihani wa mwisho wa shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala, June 20, 2012 Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM)

Hii ndio halisi ambayo wahitimu wengi wa Vyuo mbalimbali nnchini wanakumbana nazo. Jamii haitakiwi kuwalumu Vijana kwa dalili za utegemezi wanaouonyesha zaidi jitahada malimu zinahitajika kutatua tatizo la kupunguza vifaranga vingi vinavyototolewa Vyuo Vikuu huku vikienda kwenye mabanda ya no ajira.

Tujifunze kupitia haya. Tutafute njia mbadala wa kutatua tatizo kwa kila mdau nchini.

Monday, July 2, 2012


Happy Birthday!


Umetimia mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa blog hii, ilikua ni july 2011 na sasa ni july 2012. Yapo malengo mengi ambayo hayajatimizwa kama ilivyopangwa hapo awali. Lakini huo si mwisho wa kuifanya Blog hii kuwa bora zaidi na yenye chambuzi na habari za kina.

Ni dhahiri kwamba kushindwa kufikia malengo kwa asilimia mia ni moja ya dalili za kushindwa kutimiza mipango. Hata hivyo kushidwa kutimiza lengo ni changamoto kwangu, kunanipa nguvu ya kujipanga zaidi na kuandaa mipango ya muda mfupi  na mrefu ili kutimiza lengo.


Napenda kuwashukuru wasomaji na wachangiaji wote kwa kushiriki katika Blog hii. Pia shukrani za dhati ziwaendee wote ambao kwa namna moja au nyingine wamesaidia kuwapo kwa blog hii. Napenda tuungane wote kutimiza malengo kwa kuchangia habari na maoni mbalimbali ambayo yatakua chachu ya maendeleo ya jamii yetu ya Tanzania. 


Napenda niahidi kuwa sasa Blog hii itakuwa na taarifa za wakati kwa kushirikiana na viunganishi vingine vya chambuzi na habari. Hii ni moja ya njia ya kuzikusanya habari na chambuzi mbalimbali sehemu moja. Hii itasaidia kujifunza mengi kwa wakati. Tafadhari tusichoke kufuatilia Blog hii katika masuala yote ya siasa, uchumi, jamii, elimu, Sayansi na teknolojia na burudani.

Karibuni sana na msikose kuisoma Blog hii kila siku.
 Nuzulack J. Dausen