Sunday, April 7, 2013

TANZANIA YAADHIMISHA MIAKA 19 YA KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI


 Leo ulimwengu umeadhimisha miaka 19 baada ya mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 na kugharimu maisha ya watu takriban milioni moja. Maadhimisho hayo hufanyika duniani kote kama siku maalumu ya kuwakumbuka wahanga wa vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Wahutu na Watusi iliyopiganiwa ndani ya siku 1oo.


Maadhimisho hayo yalianza kuazimishwa tangu mwaka 2004 baada ya Umoja wa Mataifa kuiteua April 7 kila mwaka kuwa ni siku ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari.

Nchini Tanzania maadhimisho hayo yamefanyika leo jijini Dar es salaam ambapo baadhi ya Wanadiplomasia mbalimbali walikusanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City kwa ajili ya maadhimisho ambapo waliongozwa na Balozi wa Rwanda nchini Dk Benjamin Rugangazi  huku mgeni rasmi akiwa ni Mwanadiplomasia mkongwe Dk Salim Ahmed Salim.

Kabla ya maadhimisho hayo yalifanyika matembezi  ya kumbukumbu kuanzia  katika Viwanja vya New World Cinema- Mwenge hadi Mlimani City ambapo yalihudhuriwa na Wanafunzi mbalimbali wa Shule za Msingi na Sekondari za jijini Dar es salaam.

Maadhimisho hayo yalianza kwa kuwasha mishumaa ikiwa ni ishara ya upendo wa kuwakumbuka waliopoteza maisha katika vita hivyo mbapo yalifuatiwa na burudani kutoka kwa Wanafunzi wa shule ya Msingi ya Heritage na baadaye kumaliziwa na hotuba mbalimbali ikiwemo ya Dk salim.
Picha zifuatazo zinaonyesha matukio mbalimbali ya maadhimisho hayo.