Thursday, December 4, 2014

KUTANA NA MUUZA MADAWA YA KULEVYA ALIYEKATWA MKONO, MGUU

 Nuzulack Dausen
UKIMUONA kwa mara ya kwanza ni vigumu kufikiri kama anaweza akawa amepitia katika mikasa migumu ya kutisha ya maisha kama ilivyomtokea.

Nguo zake kuukuu, nywele za chafu na ulemavu alionao vinaficha historia nzito aliyonayo katika maisha pamoja na utaalamu wa kuongea kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kiitaliano na Kireno licha ya kutosomea.
Huyu ndiye ‘Wa Mbele’ kijana aliyejiwekea ndoto za kuishi nje hasa Ulaya akiamini kuna maisha mazuri ambayo yangemfanya naye awe tajiri.
Hata hivyo ndoto zake hizo zilizimika pale hali hali ilivyobadilika na kujikuta akililia kurudi Tanzania baada ya kukumbana na mateso, manyanyaso, ukatili na biashara za kuhatarisha maisha kiasi cha kumfanya awe mlemavu wa viungo vya mwili uliomdhoofisha na kumharibia maisha yake.
Wa Mbele ambaye jina lake halisi ni Mbembele Said Lipwata nilikutana naye katika safari yangu Mjini Mtwara. Mbali na ulemavu wake  wa mguu na mkono wa kulia, bado ana uwezo mkubwa wa kutembea kwa kuruka kwa masafa marefu.
Anasema alizaliwa mwaka 1967 mkoani Mtwara, alikulia huko hadi mwaka 1976 alipojiunga na elimu ya msingi katika Shule ya Shangani.
“Hali duni ya maisha ilinifanya nimkimbie baba aliyekuwa akiishi Mtwara, kwenda kwa mama Magomeni Kagera Jijini Dar es salaam, niliendelea na masomo yangu huko” anasimulia Mbembele akieleza kuwa wazazi wake hawakuwa wakiishi pamoja.
Kaka zake wakubwa walikuwa wanajishughulisha na kazi za ubaharia jambo ambalo lilimpa matumiani makubwa ya kukamilisha ndoto ambazo alikuwa nazo kwa miaka mingi kwamba siku moja angezamia kwenda Ulaya akiamini angepata maisha mazuri.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi mwaka 1983, Mbembele hakuwa na kazi ya kufanya kutokana na kushindwa kuendelea na masomo ya Sekondari, akaanza kuzunguka na kaka zake katika meli tofauti ndani ya Pwani ya Afrika Mashariki na kujaribu mbinu za kuzamia Ulaya.
Majaribio ya kuzamia
Kutokana na kupata uzoefu kidogo katika safari za meli, Mbembele anasema alianza majaribio ya kuzamia yeye na rafiki zake. Bandari ya Mtwara na Dar es salaam ndiyo vilikuwa vituo vikuu vya majaribio yao.