Thursday, November 19, 2015

Uwaziri Mkuu wa Majaliwa unavyoweza kujaliwa zaidi

Baada ya Rais John Magufuli kupendekeza jina la Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya awamu ya tano na hatimaye kupitishwa na Bunge, habari zinazozunguka kwa sasa nchini ni kwamba kiongozi huyo mpya ataweza jukumu hilo zito.
Uteuzi wa Majaliwa unaokena kama ni ‘surprise’ kwa Watanzania waliowengi. Ndiyo, huenda kweli ni surprise kwa sababu mwanasiasa huyo si mwingi wa kutafuta ujiko kama wengine.
Inawezekana kweli ikawa Surprise kwa kuwa wengi hawakutarajia kuwa Dk Magufuli angefanya uteuzi wakenje ya miamba ya siasa iliyozoeleka na iliyokuwa ikitajwa kama William Lukuvi na Dk Harrison Mwakyembe.
Kwa aina ya uteuzi huo wa Rais hapana shaka swali la je, Majaliwa atakitendea haki cheo hicho hasa katika Seikali inayojinasibu kwa “Hapa Kazi Tu”, haliepukiki. Na maswali mengi kama hayo yataibuka kila uchwao katika siku hizi za awali ambazo Mbunge huyo wa Ruangwa atakuwa akianza kutekeleza majukumu yake.
Kwa mtazamo wangu, Majaliwa anaweza kwenda na kasi ya Magufuli kwa asilimia 100. Si kwenda nayo yu bali hata kuituliza kasi hiyo pale itakapoonekana kuzidi na kuleta hatari.
Kama mwanahabari nafahamu utendaji wa Majaliwa kupitia nafasi zake alizopitia hasa ya Naibu Waziri wa Ofisi ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi (Elimu) ambayo baadhi ya mambo nilikuwa nikiyafutilia kwa karibu likiwemo agizo la rais mstaafu Jakaya Kiwkete la ujenzi wa maabara kwa kila shule ya Sekondari ya Kata.
Hivyo, matokeo ya utendaji bora wa Majaliwa yatachangiwa zaidi na baadhi ya mambo yafuatayo:-

  1. Hafahamiki sana
Licha ya kuwa alikuwa Naibu Waziri katika Serikali iliyopita, Majaliwa siyo miongoni mwa watu maarufu sana kiasi cha mfumo wake wa usimamizi na utendaji kufahamika bayana miongoni mwa watumishi wa umma na wananchi.
Pamoja na kutofahamika sana, Waziri Mkuu ni mtendaji. Ni mtendaji asiyefahamika na wengi. Wengi wanaomfahamu, angalau kasi yake, ni wale waliopo Tamisemi na kwenye sekta ya elimu. Vivyo, wanasiasa wanaoweza kujinadi kuwa wanamfahamu ni wale tu waliokuwa kwenye Kamati mbalimbali za Bunge ambazo zilikuwa zikishirikiana mara kwa mara na Tamisemi.
Sifa hizo zikijumulishwa na uchapakazi wa bosi wake, Dk Magufuli inapatikana picha ya moja kwa moja kuwa watumishi hawatakuwa na njia nyingine zaidi ya kujituma kufanya kazi kutokana na kutojua aina ya misimamo ya Majaliwa.
Matokeo hayo, yatamsaidia vyema mwalimu huyo wa zamani kuwasimamia mawaziri wake ambao bila shaka wengi watakuwa wapya kwenye Baraza la Mawaziri linalotarajiwa kuundwa hivi karibuni.

  1. Presha ya kukilinda chama tawala

Kama ilivyo kwa Rais, Majaliwa naye atakuwa na kibarua kigumu cha kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha anasaidia kuiokoa CCM kutoka madarakani miaka mitano ijayo.
Kwa maana hiyo, hataweza kuruhusu uzembe wowote ndani ya utumishi wa umma ambao huenda ukaipeleka CCM kwenye kaburi la sahau na kuiacha nchi chini ya upinzani.
Ushindani uliokuwepo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 ni salamu tu kwa Serikali ya JPM ambayo Waziri Mkuu hubeba mizigo kibao ya Serikali pale ufanisi unapopitia mlango wa nyuma.
Hofu hiyo, itasaidia mbunge huyo wa Ruangwa afanikiwe kuitumikia nafasi yake vyema na kuonekana ni mchapakazi na kujibu maswali yanayojitokeza kwa sasa.

  1. Kulinda kibarua chake
Hakuna ubishi kuwa baada ya kuitumikia nafasi hiyo kwa kipindi kifupi, Majaliwa atavutiwa kuendelea kuitumikia ili kibarua kisiote nyasi. Hatakubali kirahisi ibara ya 53A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imng’oe na kuweka historia kwa mara ya kwanza nchini.
Hatothubutu hata kidogo akina Tundu Lissu au Zitto Kabwe waanzishe hoja za kuwa na imani na Waziri Mkuu wakati ana uwezo wa kuzuia hali hiyo mapema kwa kufanya kazi kwa bidii.
Hivyo, nia hiyo njema ya kupalilia kibarua moja kwa moja itamsaidia kuchapa kazi na hata kukwepa vizingiti vya kumwangusha hapo mbeleni.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, Majaliwa kama mwanasiasa yoyote anafaa kuwa Waziri Mkuu. Lakini kikwazo kikubwa kinachoweza kumpunguza kasi ni kwamba sehemu kubwa ya utendaji inategemea zaidi mwitikio na ufanisi wa utumishi wa umma. Kama inavyohamika, utendaji wa sekta hiyo unahitaji mabadiliko ya jumla na siyo maboresho ya viraka.
Iwapo watumishi hao watafanya kazi kwa moyo na kuonyesha vipaji vyao bila ya woga wowote Serikali hii itafanikiwa zaidi na kuweka nafasi nzuri zaidi ya kurudi 2020. Ila, ikishindwa ndiyo utakuwa mwisho wake.
Nifuate kupitia Twitter @nuzulack