Monday, May 4, 2015

Wakati wa vijana kuacha mawazo ya kuajiriwa ni sasa


Ni kawaida kwa vijana wengi nchini kuwa na ndoto lukuki za mafanikio wanapoingia vyuo vikuu na vyuo vya kati. Asilimia kubwa huamini kozi wanazochagua na kusomea zitawapatia mafanikio ya haraka zaidi katika maisha.
Dhana hiyo huwafanya kuchagua kozi nzuri ambazo wakihitimu bila shaka watakua mameneja au watu wenye nafasi nzuri zaidi katika kampuni au mashirika makubwa ya umma.
Katika mawazo hayo ya ‘kusadikika’ huwa kuna mipango mingi ya kutekeleza mara baada ya kumaliza elimu zao ikiwamo kupata kazi haraka katika kampuni wanazotarajia kufanya, kuoa au kuolewa na wachache sana huwaza kuwekeza.
Hata hivyo mambo huwa ni magumu pale wanapomaliza stashahada au shahada zao kwa kukosa ajira ambazo huaribu mipango mingine yote. Kwa kiasi kikubwa ajira ndiyo msingi wa mipango mingi ya vijana hivyo ikikosekana kila kitu kinazama.
Nakumbuka hata mimi nilipata wakati mgumu kuchagua kozi ya kusoma kutokana na ushawishi mkubwa niliokuwa na upata kwa wakubwa zangu kuchagua masomo waliyoyaita ya ‘pesa pesa’.
Katika kundi la watu wote waliokuwa wakinishauri hakuna aliyeniambia kuwa nikienda kusoma Mlimani nitumie masomo hayo ili niweze kupata ufahamu wa kuwekeza.

Hakuna aliyethubutu kuniambia kuwa nikiwa shule nitunze fedha kidogo ntakazokuwa napata kwenye mkopo wa elimu ya juu au kutafuta ‘dili’ za muda mfupi zitakazoniongezea kipato kitakachosaidia kuanzisha biashara zangu.
Aina hiyo ya ushauri inazidi kuangamiza asilimia kubwa ya vijana nchini hasa wanaobahatika kupitia vyuo vikuu. Dhana ya kijamaa ya miaka 35 iliyopita ya kupata kazi baada ya chuo bado inatutafuna na kutufanya tuwe watumwa wa ajira.
Vijana wengi tumekuwa waoga wa kujaribu kujiajiri na kujikuta tunabaki mtaani hata baada ya kuhitimu kozi nzuri za biashara. Baadhi yetu hata kabla ya kujaribu kutafuta mawazo ya biashara tunakatishwa tamaa na nafsi zetu kuwa hatuwezi na hakuna vyanzo vya fedha kutuwezesha.
Hofu hiyo kama hiyo ndiyo anayoiita aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Utouh, kuwa ni matokeo ya kutobadilika ya mawazo ya muda mrefu ya kijamaa. Ni sehemu ya utegemezi wa kufikiri kila kitu kinafanywa na serikali na kuwapatia wananchi mambo mazuri.
Kizazi chetu kimebatika kuishi katika ulimwengu wa habari tele za biashara na uwekezaji lakini ni wachache sana wanaoweza wakatulia na kompyuta zao mpakato au simu wakasoma habari kama hizo.
Aina hiyo ya mawazo itaongeza idadi kubwa ya vijana wasio na ajira ambao baadhi ya wanasiasa wanaliita tatizo hilo kama bomu linalosubiri kulipuka. Iwapo kila mwaka wanahitimu zaidi ya 1 milioni na kuingia kwenye soko la ajira, na asilimia ndogo tu ndiyo wanaajiriwa kuna umuhimu mkubwa kujifunza kuwekeza.
Lakini mawazo na tabia ya kusubiri ajira yanaweza kuondolewa miongoni mwa vijana iwapo tunaweza kufanya yafuatayo;
Mosi, kujenga tabia ya kuwekeza kidogo kinachopatikana wakati tukiwa masomoni. Ni dhahiri kuna baadhi ya vijana wana matatizo ya kifedha lakini pia wapo wenye fedha kidogo zinazoweza kukusanywa taratibu benki pale wawapo masomoni zitakazowasaidia kupata mitaji watakapomaliza vyuo.
Ukikusanya Sh3 milioni kwa miaka mitatu itakayotokana na kuhifadhi kiasi kidogo cha pesa zako na kufanya vibarua bila shaka inaweza kusaidia kuanzisha biashara yoyote itakayosaidia kuishi mjini.
Pili, usomaji wa taarifa mbalimbali utasaidia vijana wengi kupata taarifa za namna ya kuanzisha biashara kutoka kwa watu mbalimbali wenye uzoefu. Binafsi nimejiunga na mtandao kibao inayotoa mafunzo ya ujasiriamali kama yes.com, Forbes, Vijanatz.com, Buni hub na mingine lukuki.
Kwenye vyanzo hivyo vya habari unaweza kupata taarifa nyingi zikiwemo namna ya kupata mitaji kwa kuanzisha mawazo mazuri ya biashara. Kuna wawekezaji lukuki wanatafuta vijana wabunifu watakaokuja na mawazo mazuri ya biashara yatakayoleta faida kubwa kwa mwekezaji na jamii.
Tatu, kuunda mtandao wa vijana wenye malengo ya kibiashara kunaweza kutuepusha na bomu. Vijana tunatakiwa tuwe na uhusiano wa karibu wa kibiashara kwa kuunda mtandao. Aina ya mtandao kama huo unaweza kusadia kuunda wazo, kuwakutanisha na taasisi za kimataifa na za ndani zinazotoa mitaji isiyo na riba kwa njia ya ushindani wa mawazo. Pia, kupitia kikundi ni rahisi kuomba miadi na wajasiriamali wakubwa ili kupatiwa mafunzo ya kutoka kibiashara. Katika soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kuna wawekezaji lukuki wanaotafuta maeneo ya kuwekeza ila hawajapata mawazo  na kumpuni nzuri za chini na kati.
Mbinu kama hizo zinaweza kuwatoa vijana woga katika kufanya biashara na hatimaye kupunguza idadi ya wanaotegemea ajira. Kama asilimia kubwa ya vijana waliosoma watakuwa wanawaza ujasiriamali basi kuna kila dalili kuwa ajira nyingi zitatengenezwa na kupunguza kundi la wasio na ajira wenye elimu na ujuzi.