
Uteuzi wa Majaliwa unaokena kama ni ‘surprise’ kwa
Watanzania waliowengi. Ndiyo, huenda kweli ni surprise kwa sababu mwanasiasa
huyo si mwingi wa kutafuta ujiko kama wengine.
Inawezekana kweli ikawa Surprise kwa kuwa wengi
hawakutarajia kuwa Dk Magufuli angefanya uteuzi wakenje ya miamba ya siasa
iliyozoeleka na iliyokuwa ikitajwa kama William Lukuvi na Dk Harrison Mwakyembe.
Kwa aina ya uteuzi huo wa Rais hapana shaka swali la je,
Majaliwa atakitendea haki cheo hicho hasa katika Seikali inayojinasibu kwa “Hapa
Kazi Tu”, haliepukiki. Na maswali mengi kama hayo yataibuka kila uchwao katika
siku hizi za awali ambazo Mbunge huyo wa Ruangwa atakuwa akianza kutekeleza
majukumu yake.
Kwa mtazamo wangu, Majaliwa anaweza kwenda na kasi ya
Magufuli kwa asilimia 100. Si kwenda nayo yu bali hata kuituliza kasi hiyo pale
itakapoonekana kuzidi na kuleta hatari.
Kama mwanahabari nafahamu utendaji wa Majaliwa kupitia
nafasi zake alizopitia hasa ya Naibu Waziri wa Ofisi ya Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu Tamisemi (Elimu) ambayo baadhi ya mambo nilikuwa nikiyafutilia kwa karibu
likiwemo agizo la rais mstaafu Jakaya Kiwkete la ujenzi wa maabara kwa kila
shule ya Sekondari ya Kata.
Hivyo, matokeo ya utendaji bora wa Majaliwa yatachangiwa zaidi
na baadhi ya mambo yafuatayo:-
- Hafahamiki sana
Licha ya kuwa alikuwa Naibu Waziri katika
Serikali iliyopita, Majaliwa siyo miongoni mwa watu maarufu sana kiasi cha
mfumo wake wa usimamizi na utendaji kufahamika bayana miongoni mwa watumishi wa
umma na wananchi.
Pamoja na kutofahamika sana, Waziri
Mkuu ni mtendaji. Ni mtendaji asiyefahamika na wengi. Wengi wanaomfahamu, angalau
kasi yake, ni wale waliopo Tamisemi na kwenye sekta ya elimu. Vivyo, wanasiasa
wanaoweza kujinadi kuwa wanamfahamu ni wale tu waliokuwa kwenye Kamati
mbalimbali za Bunge ambazo zilikuwa zikishirikiana mara kwa mara na Tamisemi.
Sifa hizo zikijumulishwa na uchapakazi wa bosi
wake, Dk Magufuli inapatikana picha ya moja kwa moja kuwa watumishi hawatakuwa
na njia nyingine zaidi ya kujituma kufanya kazi kutokana na kutojua aina ya
misimamo ya Majaliwa.
Matokeo hayo, yatamsaidia vyema
mwalimu huyo wa zamani kuwasimamia mawaziri wake ambao bila shaka wengi
watakuwa wapya kwenye Baraza la Mawaziri linalotarajiwa kuundwa hivi karibuni.
- Presha ya kukilinda chama tawala
Kama ilivyo kwa Rais, Majaliwa naye
atakuwa na kibarua kigumu cha kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha
anasaidia kuiokoa CCM kutoka madarakani miaka mitano ijayo.
Kwa maana hiyo, hataweza kuruhusu
uzembe wowote ndani ya utumishi wa umma ambao huenda ukaipeleka CCM kwenye
kaburi la sahau na kuiacha nchi chini ya upinzani.
Ushindani uliokuwepo katika Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25 ni salamu tu kwa Serikali ya JPM ambayo Waziri Mkuu
hubeba mizigo kibao ya Serikali pale ufanisi unapopitia mlango wa nyuma.
Hofu hiyo, itasaidia mbunge huyo wa
Ruangwa afanikiwe kuitumikia nafasi yake vyema na kuonekana ni mchapakazi na
kujibu maswali yanayojitokeza kwa sasa.
- Kulinda kibarua chake
Hakuna ubishi kuwa baada ya
kuitumikia nafasi hiyo kwa kipindi kifupi, Majaliwa atavutiwa kuendelea
kuitumikia ili kibarua kisiote nyasi. Hatakubali kirahisi ibara ya 53A ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imng’oe na kuweka historia kwa mara
ya kwanza nchini.
Hatothubutu hata kidogo akina Tundu Lissu au
Zitto Kabwe waanzishe hoja za kuwa na imani na Waziri Mkuu wakati ana uwezo wa
kuzuia hali hiyo mapema kwa kufanya kazi kwa bidii.
Hivyo, nia hiyo njema ya kupalilia
kibarua moja kwa moja itamsaidia kuchapa kazi na hata kukwepa vizingiti vya
kumwangusha hapo mbeleni.
Kwa vyovyote itakavyokuwa, Majaliwa kama mwanasiasa yoyote
anafaa kuwa Waziri Mkuu. Lakini kikwazo kikubwa kinachoweza kumpunguza kasi ni
kwamba sehemu kubwa ya utendaji inategemea zaidi mwitikio na ufanisi wa
utumishi wa umma. Kama inavyohamika, utendaji wa sekta hiyo unahitaji mabadiliko ya jumla na siyo maboresho ya viraka.
Iwapo watumishi hao watafanya kazi kwa moyo na kuonyesha
vipaji vyao bila ya woga wowote Serikali hii itafanikiwa zaidi na kuweka nafasi
nzuri zaidi ya kurudi 2020. Ila, ikishindwa ndiyo utakuwa mwisho wake.
Nifuate kupitia
Twitter @nuzulack
No comments:
Post a Comment