Na Nuzulack Dausen
 |
Huu ni Mnara wa Mashujaa uliopo langoni mwa Mji wa Mtwara Mikindani |
Itafikia kipindi wananchi wazawa wa mikoa ya Lindi na Mtwara
watajiuliza walimkosea nini mwenyezi mungu, kiasi cha kumchukiza na kuwapa
laana ya kutokuwa na maendeleo ya haraka kama wananchi wa mikoa mingine.
Swali hilo linawezekanaa kuwa ni kufuru na dhihaka kwa
mwenyezi mungu lakini ni stahili yao kutokana na hali halisi ya maisha
wanayoishi pamoja na masahibu yanayowapata wananchi hao wa mikoa ya kusini kabisa mwa nchi licha ya kujaliwa rasilimali za kutosha.
Tangu kupata uhuru, wananchi hao wamekuwa wakilalamika kwa
kuwa nyuma kimaendeleo baada ya serikali kuwasahau kwa muda mrefu katika
mipango mbalimbali ya maendeleo.
Kutokana na hali hiyo wananchi hao waliililia serikali ili
iweze kuwatatulia shida zao nao waweze kufikia hatua ambazo mikoa mingine
imefikia ambapo serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa iliwafikiria
na kuanza kwa kujenga mradi wa barabara kutoka Dar es salaam hadi Mtwara ambayo
mpaka sasa haijakamilika.
Hatua za awali zilikuwa ni kujenga daraja katika mto Rufiji
maarufu kama daraja la Mkapa ambalo liliweza kuwaunganisha wananchi wa kusini
na mikoa mingine ya pwani na Dar es salaam na kuacha kutumia Pantoni.
Pamoja kutatuliwa tatizo la kimuondombinu hususani ujenzi wa
barabara ya Dar mpaka Mtwara ambayo bado kilomita chache kukamilika, wananchi
wa maeneo hayo bado wanayo ya moyoni ya kutonufaika na mradi wa gesi asili wa
Songosongo ambao ulianza miaka 8 iliyopita.
Licha ya matatizo ya kimiundombinu mikoa hiyo inakabiliwa pia
na changamoto za huduma mbaya za afya, elimu, maji, umeme pamoja na ukosefu wa
ajira.
Manung’uniko hayo ndiyo yamekuwa chanzo cha mvutano mzito
unaoendelea hivi sasa kati ya serikali na wananchi wa Mtwara wakiongozwa na
viongozi wa vyama vya siasa huku wananchi hao wakigomea mradi wa ujenzi wa
bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara kwenda Dar es salaam lenye
takribani kilomita 532.
Tukio hilo linaloendelea linazidi kuvuta hisia za watu wa
kada mbalimbali nchini tofauti na wakazi wenyewe huku serikali ikiendelea
kusisitiza kuendelea na mradi huo kwa madai kuwa rasilimali hiyo ni mali ya
taifa na si ya mkoa au kikunndi cha watu fulani.
Kwa mtu ambaye hajawahi kufika mikoa hiyo ya kusini na
kuendelea kusikia madai hayo anaweza kuhisi wananchi hao ni wahuni au wahaini
kama Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alivyowaita lakini kwa
hali halisi mazingira wanayoishi ni magumu yanayohitaji msaada wa haraka.
Kabla mradi huo mpya haujaanza serikali ilibidi ionyeshe kidogo
mafanikio ya mradi wa kwanza wa gesi asili kutoka visiwa vya Songosongo ambayo
hata Mbunge wa Ubungo John Mnyika aliyataka.
Sizani Wananchi wote wa Mtwara na baadhi ya watanzania
wanaopinga ujenzi wa mradi huo ni vichaa au hawayatakii mema maendeleo ya nchi
la ha sha bali wanahitaji kuonjeshwa kidogo namna watakavyonufaika na mradi huo
tofauti na miaka ya nyuma.
Wananchi wa Mtwara wameshagutuka kuwa mradi huo unaweza
usiwanufaishe sana kama ilivyokuwa kwa ule wa Songosongo.
Lazima wananchi hao wajiulize kwanini mpaka sasa ni maskini
licha baadhi ya wilaya zake kama Nachingwea, Lindi na Mkindani kuwa ni wilaya
kongwe nchini kuliko nyingine za mikoa ya Dar esa salaam Kilimanjaro, Mwanza na
Arusha ambazo zimeendelea kwa muda mfupi.
Wananchi hao wamegundua kuwa sera ya Wajibu wa Kampuni kwa
Jamii (Corporate Social Responsibility) iliyopo ndani ya rasimu ya sera mpya ya
gesi asilia haitawakomboa katika umaskini kama wananchi wenzao waishio karibu
na migodi ya madini.
Serikali inapaswa kuyatafakari kwa kina madai ya wananchi hao
licha ya kuwa imeshaanza kuugharamia mradi huo. Ni wazi kuwa Serikali haiwezi
kuzuiwa kufanya jambo lolote juu ya rasilimali za taifa lakini viongozi wa nchi
wakumbuke mvutano huo unaibua hisia tofauti miongoni mwa watanzania ambao ni
hatari kwa amani ya nchi.
Mungu hajawalaani wananchi hawa kuwa na maisha magumu na
maendeleo finyu ambapo makao makuu ya mikoa yao hayafanani hata kidogo na mitaa
ya Tabata Segerea Jijini Dar es salaam au Soweto pale Mbeya Mjini.
Mpaka sasa asilimia kubwa ya wananchi wanaoishi Mtwara mjini katika
maeneo ya Magomeni, Ligula, Raha Leo, Mikindani na mengine hawana huduma ya
umeme licha ya Serikali kushusha gharama za umeme, hii si kuwa hawajui umuhimu
wake bali hawana kipato cha kuwaingizia fedha za kumudu gharama za huduma hiyo.
Vijana wengi hawana ajira, asilimia kubwa za kazi wanazofanya
haziwapatii kipato cha kumudu maisha. Licha ya kuwa kuna asilimia kidogo ya
ajira katika makampuni yanayotafuata gesi na mafuta mkoani humo vijana wengi hawana elimu na ujuzi wa kutosha.
Serikali lazima itambue kuwa wananchi wa Lindi na Mtwara
hawakulaaniwa na mungu wawe na maendeleo finyu kiasi hicho na pia sera na mipango pendeleo ya nyuma ndiyo chanzo cha matokeo ya
umaskini wa maeneo hayo.