Friday, August 26, 2011

Kwa hili... Vyuo Vikuu vitageuka Darfur!

       Hatimaye Tume iliundwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete mnamo  tarehe 14/02/2011 imetoa mapendekezo yake ya namna ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharimiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya Elimu ya Juu. Mapendekezo hayo yalitolewa rasmi na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dk. Shukuru J. Kawambwa tarehe 19 Agosti mwaka huu kama taarifa kwa umma. Taarifa hiyo ilitangazwa na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini yakiwemo magezeti ya kila siku. Kwa undani zaidi rejea Gazeti la Mwananchi la Jumanne Agosti 23 2011 Ukurasa wa 15 Sehemu ya Matangazo.
       Kwa wadau wote nchini wanafuatilia na waliomo katika mfumo wa Elimu ya Juu najua wanatambua adha wanayoipata Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuhusiana na Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Toka Bodi ianzishwe matatizo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku. Bodi Imesababisha Migomo mingi ya Vyuo Vikuu huku ikisababisha baadhi ya Wanafunzi wa Vyuo hivyo kupoteza masomo kabisa. 
     Bodi imekuwa kero kwa Wanafunzi, Utawala wa Vyuo Vikuu pamoja na Jeshi la Polisi nchini. Tukianza na Wanafunzi Bodi hii ya Vyuo Vikuu imesababisha Wanafunzi wengi kusoma kwa shida sana aidha kwa kucheleweshewa Mikopo yao au kucheleweshewa Means Test zao. Kwa upande wa Utawala wa Vyuo Vikuu wamekuwa wakipata kashikashi nyingi za kufunga Vyuo mara kwa mara, kuharibiwa mali na bajeti nyingine za kiutawala. Na kwa upande wa ndugu zetu Jeshi la Polisi wamekuwa wakipambana na Wanafunzi kila Mgomo unapotokea. Kwa maana hiyo Bodi inaongeza gharama za utendaji badala ya kuzipunguza kama ilivyotarajiwa.
    Matarajio ya Watanzania wengi kutoka kwenye Tume maalumu ilioundwa na Mheshimiwa Rais ni Maboreshao zaidi na si kuharibu zaidi kama inavyotabiriwa na taarifa iliyotolewa na Wizara kama ilivyotolewa na Mheshimiwa Kawambwa. Katika taarifa hiyo kwa Ummakuna vipengele sita vinavyoeleza mapendekezo hayo. Kwenye vipengele hivyo mi napenda nivielezee vipengele namba 2, 3, 4 na 5. 
    Kipengele namba 2(i) kinaelezea Utoaji wa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Katika kipengele hiki taarifa hii inawataarifu Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuwa Mikopo itatolewa kwa Wanafunzi waliodahiliwa na Vyuo Vikuu moja kwa moja Shuleni tu yaani Direct entrants na wale wenye sifa kupitia mfumo wa mafunzo ya Elimu ya Ufundi (TVET) na si kwa wale ambao wanatumia sifa linganishi (Equivalent qualifications  & Mature Age entrants). Kipengele hiki kinaondoa haki za Watanzania waliounganisha elimu na wanahitaji kusoma Elimu ya Juu kwa udhamini wa Bodi ya Mikopo.
      Hata hivyo kipenegele 2(ii) kinamaboresho kidogo hasa ni ile sehemu ya kugharamia Mafunzo kwa vitendo kwa fani zote zitakazobainishwa na Tume ya Vyuo Vikuu kwa Asilimia Mia Moja. Ingawa mabadilisho haya yameandikwa ila inawezekana yakabaki kwenye makaratasi tu. Kwa hilo tunasubiri utekelezaji. Na sehemu nyingine za asilimia Mia Moja zinabaki kama kawaida hasa kwenye maeneo ya Chakula na Malazi, Vitabu na Viandikwa (Stationary) na Utafiti (Research). 
     Fani za kipaumbele zimebaki zilezile za awali yaani Ualimu, Sayansi za Tiba, Uhandisi, Sayansi za Kilimo,  na Sayansi za Mifugo. Hata hivyo Walimu wa Masomo ya Sanaa wamepitiwa na Tsunami kwani hawatapata Asilimia Mia Moja kama wale wa Sayansi na na hawatapata chini ya Asilimia 50%. Hali mbaya  zaidi kwa wale wa fani zisizo za Ualimu, Sayansi na Uandisi. Kwa wale wote ambao ni Mature Age entrants  na wenye sifa linganishi mikopo watapata kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii au kwa Waajili wao. Je kwa hili ni haki?
      Mbaya zaidi ni hii ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kupewa gharama za ada sawa na zile za Serikali wakati muundo wa ada upo tofauti kati ya Vyuo Binafsi na Vya Umma. Kama hali hii je wanafunzi waliopo Vyuo Banafsi watasaivu? Kwa mabadiliko haya lazima tukubaliane kuwa Migomo ya Vyuo Vikuu hasa vile vya Binafsi itawekwa kwenye ratiba maalumu kwa ajili ya kushindwa kulipa kiasi hicho cha ziada. Mifano tunayo mingi sana ya hivi karibuni. Moja ya mifano hiyo ni kufungwa kwa Chuo cha IMTU, na maandamano ya Wanafunzi wa Udaktari wa Chuo cha Kumbukumbu ya Hurbert Kairuki kwenda tume ya Vyuo Vikuu (TCU). 
      Haya si maboresho tena bali ni maangamizi kwa sababu Wanafunzi wengi hawatasoma Vyuo Vikuu kulingana na uwezo kifedha hasa hiyo ya kujazia viwango vya ada vilivyozidi kutoka kwenye vile vya Serikali. Ikumbukwe kuwa Vyuo Binafsi ndio vinachukua idadi kubwa ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Kama hali itakuwa kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mheshimiwa Rais basi ndugu zetu wote wasio na uwezo na waliokosa nafasi za Vyuo Vya Umma hawatasoma kabisa. Hili ni angamizo kabisa hata wale wanaosoma Sayansi kama kipaumbele kinavyoeleza hawatafankisha kwa sababu ada za Vyuo binafsi fani za Sayansi ni tofauti na Vyuo vya Umma. Hapa Tume au wizara iliangalie upya suala hili kwani gharama itakayotumika kuzima migogoro itakayojitokeza inaweza kuwa kubwa kuliko hata wangeghalamia masomo ya Wanafunzi hawa wa Vyuo binafsi.
     Kipengele namba 3 kinaelezea Urejeshaji wa Mikopo. Katika kipengele hiki Tume imeweka kiwango cha urudishwaji wa mikopo kuwa ni Asimia 8 ya Mshahara wa kila Mfanyakazi aliyesomeshwa na Bodi ya Mikopo na Sheria zitatungwa kuwabana Wafanyakazi hao ili kurejesha Mikopo.
       Kipengele ambacho kitaleta sana balaa ni hiki cha namba 4. Kipengele hiki kinazungumzia Masuala ya kiutawala hasa kuhusiana na Mikopo kwa Ujumla. Hapa Vyuo Vikuu vyote nchini vimeombwa vianzishe Dawati Maalumu la Masuala ya Mikopo na Dawati hili litakuwa chini ya Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma. Na kuanzia Mwaka wa Masomo unaokuja yaani 2011/12 Wanafunzi wote watachukulia fedha zao Vyuoni na si Bodi kama awali. Kwa maana hiyo basi Malalamiko yote yanayohusiana na kukosa au kucheleweshewa fedha yatatuliwa ndani ya Chuo husika Hapa Bodi imeamua kujivua gamba. Hata hivyo gamba lenyewe imechelewa kujivua kwa sababu bado Vyuo Vikuu vitakupambana na balaa kali zaidi ya ile kutoka kwa Bodi. 
      Balaa hili linakuja kwa sababu Vyuo vingi havitakuwa na uwezo thabiti wa kukabilana na kashikashi za Wanafunzi, pili kufeli kwa Mawasialiano na Mahusiano bora katika ya Chuo na Bodi kunaweza kuleta balaa kali kwa Vyuo Vikuu husika. Mfano Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) wamekuwa wakimpa shughuli nzito sana Afisa wa Mikopo wa Chuo hicho Maarufu kama Bush. Ofisi huwa haitulii kwa Wanafunzi wachache sana ambao si zaidi ya Mia tatu. Kama hali ni hiyo kwa Mia Tatu, je Wanafunzi karibia 15000 itakuwaje? Na kama inavyofahamika Wanafunzi wa Chuo hiki huwa wana hitaji haki kila sehemu inayowahusu kama ilivyokuwa Mwezi Februari Mwaka huu ambapo mgomo wao ulisababisha kuundwa kwa Tume hii ilyoleta mapendekezo haya pamoja na kuongezeka kwa fedha za kujikimu (Boom) toka Shilingi 5000-7500.
       Kwa pendekezo hili la kuchukulia hela Vyuoni Serikali ijiandae na Maandamano yasiyoisha kutoka kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vyote nchini. Kwa sababu Vyuo Vingi vina Wanafunzi wengi kuliko uwezo unaohitajika. Utawala wa Vyuo Vikuu vyote nchini ujiandae kwa lolote litakalowakuta iwapo watashindwa kutimiza mipango hiyo.
       Kipengele cha mwisho kujadili ni cha 5 ambacho kinazungumzia Ruzuku kwa Wanafunzi wa sayansi za Tiba. Hapa Wanafunzi wote wenye Division Three wasitegemee kabisa Ruzuku hii isipokuwa kwa wale wenye Three za Penati yaani waliofeli somo la General Studies katika mitihani ya Kidato cha Sita. Ruzuku hii pia inaanzia Mwaka wa Masomo ujao wa 2011/12.
      Kutokana na Mapendekezo hayo ya Tume na Wizara kwa Ujumla bado Bodi ya Mikopo haijaboreshwa na Wanafunzi hawatatuliwa kero zao nyingi. Kilichofanyika ni kutoa nafuu na kuweka angalu. sababu wanafunzi wengi watakosa kusoma na wale wote wanaotumia Mature Age entry na equivalent hawatajiendeleza Masomo yao iwapo Mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii au Taasisi hizo zitakataa kuwasomesha
    Hivyo basi Mapendekezo haya yamekuja kuwagawa Wanafunzi wengi na kuongeza Matatizo. Naiomba Bodi ya Mikopo, Tume pamoja na Wizara warudi tena kazini kurekebisha mapungufu haya ili waje na Maboresho na si haya Mabomosho.


No comments:

Post a Comment