Thursday, December 4, 2014

KUTANA NA MUUZA MADAWA YA KULEVYA ALIYEKATWA MKONO, MGUU

 Nuzulack Dausen
UKIMUONA kwa mara ya kwanza ni vigumu kufikiri kama anaweza akawa amepitia katika mikasa migumu ya kutisha ya maisha kama ilivyomtokea.

Nguo zake kuukuu, nywele za chafu na ulemavu alionao vinaficha historia nzito aliyonayo katika maisha pamoja na utaalamu wa kuongea kwa ufasaha lugha za Kiingereza, Kiitaliano na Kireno licha ya kutosomea.
Huyu ndiye ‘Wa Mbele’ kijana aliyejiwekea ndoto za kuishi nje hasa Ulaya akiamini kuna maisha mazuri ambayo yangemfanya naye awe tajiri.
Hata hivyo ndoto zake hizo zilizimika pale hali hali ilivyobadilika na kujikuta akililia kurudi Tanzania baada ya kukumbana na mateso, manyanyaso, ukatili na biashara za kuhatarisha maisha kiasi cha kumfanya awe mlemavu wa viungo vya mwili uliomdhoofisha na kumharibia maisha yake.
Wa Mbele ambaye jina lake halisi ni Mbembele Said Lipwata nilikutana naye katika safari yangu Mjini Mtwara. Mbali na ulemavu wake  wa mguu na mkono wa kulia, bado ana uwezo mkubwa wa kutembea kwa kuruka kwa masafa marefu.
Anasema alizaliwa mwaka 1967 mkoani Mtwara, alikulia huko hadi mwaka 1976 alipojiunga na elimu ya msingi katika Shule ya Shangani.
“Hali duni ya maisha ilinifanya nimkimbie baba aliyekuwa akiishi Mtwara, kwenda kwa mama Magomeni Kagera Jijini Dar es salaam, niliendelea na masomo yangu huko” anasimulia Mbembele akieleza kuwa wazazi wake hawakuwa wakiishi pamoja.
Kaka zake wakubwa walikuwa wanajishughulisha na kazi za ubaharia jambo ambalo lilimpa matumiani makubwa ya kukamilisha ndoto ambazo alikuwa nazo kwa miaka mingi kwamba siku moja angezamia kwenda Ulaya akiamini angepata maisha mazuri.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi mwaka 1983, Mbembele hakuwa na kazi ya kufanya kutokana na kushindwa kuendelea na masomo ya Sekondari, akaanza kuzunguka na kaka zake katika meli tofauti ndani ya Pwani ya Afrika Mashariki na kujaribu mbinu za kuzamia Ulaya.
Majaribio ya kuzamia
Kutokana na kupata uzoefu kidogo katika safari za meli, Mbembele anasema alianza majaribio ya kuzamia yeye na rafiki zake. Bandari ya Mtwara na Dar es salaam ndiyo vilikuwa vituo vikuu vya majaribio yao.

Wednesday, September 17, 2014

Mitandao ya kijamii isipoteze utu wetu na kudhalilisha waliokufa


Ndani ya mwezi mmoja watanzania tumeshuhudia mfulululizo wa ajali mbaya za mabasi ya masafa marefu zilizogharimu maisha ya watu zaidi ya 50 na kuwaacha wengine wakiwa majeruhi.
Tofauti na ajali zilizokuwa zikitokea miaka ya nyuma, ambazo waharifu walikuwa wakiiba mali za majeruhi na marehemu, safari hii kuna aina mpya ya uhalifu: uzalilishaji.
Mara tu baada ya ajali hizo kutokea baadhi ya watu aidha walionusurika au mashuhuda walijikuta wakiacha kusaidia majeruhi na kurekodi video au picha za kutisha na kuweka mtandaoni.
Asilimia kubwa ya picha hizo zimesambaa kwa kasi sana ndani ya majuma matatu haya na sasa zimekuwa zikipatikana kwa haraka bila hata kuangalia utu wa majeruhi au marehemu hao.
Dakika chache baada ya kugongana mabasi mawili ya Mwanza Coach na J4 Express hivi karibuni mkoani Mara, baadhi ya picha za maiti waliotolewa ndani ya magari hayo zilisambazwa zikionyesha wamelala chini bila hata ya kufunikwa.
 Sanjari na picha hizo, pia kulikuwapo na nyingine ilionyesha watu wawili wakiwa wananing’inia kwenye moja ya mabasi hayo baada ya sehemu za miili kunasa kwenye viti.
Picha hiyo ambayo inaonyesha maiti hao--wanaoweza kutambulika--wakiwa wamening’iniza vichwa vyao mtawalia huku damu nyingi zikichuruzika.
Pia, siku kadhaa baada ya ajali hiyo, ilitokea nyingine wilayani Kilosa ambayo iliua watu wanne na kujeruhi 35 baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka dar es Salaam kwenda Tabora kuanguka eneo l la Berega.
Kama ilivyoa ada, watu hao ‘waandishi wa habari’ wa kisasa walisambaza tena picha za marehemu wanne wakiwa wamelazwa chini baada ya ajali.
Ndani ya saa 24 tena iklitokea ajali nyingine katika eneo la Tangi Bovu Jijini Dar es Salaam ambapo Lori lilipita basi na kuwagonga vibaya mwendesha pikipiki na abiria wake. 
Mwili wa dereva ulitupwa mtaroni wakati ule wa abiria ulichubuliwa na kugawanywa nusu baada ya kuburutwa na gari hilo.
Kama mchezo tena , picha za ajali hiyo zilisambazwa katika mitandao ya kijamii kama blogu, Whatsapp, facebook, Twitter na mingineyo. Pamoja, na uwingi wa mitandao hiyo, matumizi ya whatsapp ndiyo yamezidisha hali hiyo na inaonyesha jinsi gani Watanzania tulivyochanyikiwa na teknolojia ya mitandao ya kijamii.
Wengi tunaotumia mitandao hiyo hapana shaka tumeshatumiwa au tumeziona picha hizo tena zaidi hata ambazo nimezitumia kama mfano.
Katika ulimwengu wa dijitali ni dhahiri tunatakiwa kwenda na wakati hususan mabadiliko ya teknolojia. Hata sisi waandishi tunaofanyia katika vyombo vya habari vilivyo na sera zake na kuaminika kwa jamii tunapaswa kufanya hivyo lakini kwa kuzingatia maadili na utu wa watu.
Matumizi ya mitandao ya kijamii hayaepukiki katika kutoa habari za haraka lakini ni lazima tuheshimu utu wa Watanzania au yeyote yule ambayo anakutwa na maafa.
Usambazaji wa picha za kutisha na zinazozalilisha marehemu katika mitandao unatishia usalama wa taifa na unatia hofu kuwa Watanzania hawajali tena ndugu au rafiki zao.
Naamini wengi wanaopiga picha hizo hawajakutwa na majanga kama hayo kiasi cha mama, baba, kaka au wajomba zao kupatwa na ajali na miili yao kuwa miongoni ya ile inayoisambazwa katika mitandao.
Kuweka picha katika mitandao hiyo kunaziumiza kisaikolojia familia za ndugu waliopoteza maisha hasa zile zinazooneka wazi na katika hali isiyotakiwa kuoneshwa kwa mujibu wa mila zetu.
Pia, kunatia hasira kiasi cha kutengeneza kisasi iwapo ndugu hao wakibaini msambazaji na kuleta mambo ambayo taifa la umoja na upendo kama letu hatutaka tushuhudie.
Binafsi sipingani na uchukuaji wa picha za matukio hayo lakini uangalifu mkubwa unatakiwa kulinda heshima zetu na amani yetu kwa kusambaza picha ambazo haziogopeshi au kuzalilisha watu kama inavyoendelea nchini.
Nchi zilizoendelea, ambako teknolojia ya mitandao ya kijamii ilianzia, usambazaji wa picha kama hizo umepitwa na wakati na wameona haufai kwa ustawi wa taifa.
Mitandao ya kijamii kama hii itumike kutuunganisha sio kubomoa uhusiano wetu. Picha hisani ya socialmediamarketing.com
Wakati wa maafa kama hayo wenzetu hujumuika kwa pamoja na kutumia mitandao hiyo kukusanya michango ya fedha na damu kuchangia matibabu na kuokoa maisha ya majeruhi.
Mfano mzuri ni nchini Kenya. Baada ya Shambulio la duka la Westigate na magaidi wa Alshabab Septemba mwaka jana, Wakenya waliungana na kuchangia damu na mali hadi majeruhi walipopata nafuu; hakuna aliyeweka picha ya marehemu akikenua meno baada ya kuuawa…kwanini sisi tunadhalilishana!?
Ifike kipindi tuache ushamba wa mitandao na utumiaji wa kamera ovyo kuzalilisha marehemu na majeruhi. Yatupasa kuvivaa viatu vya watu na familia zao na namna wanavyoumia kwa picha hizo kusambaa ili kutokomeza tabia hiyo.
Makala haya yalichapishwa awali Jumanne, 16 katika gazeti la Mwananchi.