Friday, September 2, 2011

Kujivua gamba si kujivua uhai; Wanaotuhumiwa CCM wakubali kujivua.....

        Ule Usemi wa Kujivua gamba unaotumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) una dalili zote za kukiregeza chama hicho. Msemo huu uliteka masikio na akili za Watanzania wengi hasa pale ulipokuwa ukitolewa na Vyombo mbalimbali vya habari na kusindikizwa na kampeni za nchi nzima kutoka kwa Viongozi wapya wa Chama hiki kikongwe hapa nchini wakiongozwa na Katibu Mkuu Mh. Wilson Mukama akifuatiwa na Katibu Mwenezi Itikadi na Sera, Bwana Nape Nnauye. Ukijaribu kufanya tathmini ya harakaharaka kuhusu propaganda hii utagundua kuwa imetumika kutishia  Wanachama wenye kashfa za Ufisadi ndani ya Chama hicho bila ya kuwa na nyenzo mahsusi za kuwang'oa watuhumiwa hao. Msemo huu wa kujivua gamba hautofautiani sana na Mbwa mwenye kelele asiye na meno. Kiuhalisia Mbwa wa aina hii hawezi kumng'ata mtu kamwe labda kwa miujiza ya Freemasonry.
     Lakini katika safari hiyo ya kujivua gamba Watanzania tumeshuhudia Mwanasiasa Mashuhuri wa CCM ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo Igunga Bwana Rostam Aziz akiwa wa Mwanasiasa wa kwanza wa Chama hicho miongoni ya Wanaotuhumiwa aking'uka madarakani kwa kuachia ngazi zote za Uongozi kichama na kubaki kuwa Mwanachama wa kawaida. Tukio hilo lilipa sura mpya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Kuamsha hisia tofauti miongoni mwa Wanachama wa Chama hiki pamoja na Wananchi wa kawaida. Hata hivyo Bwana Rostam aliutamkia Umma wa Watanzania kuwa kung'atuka madarakani hakuhusiani na kampeni zinazoendeshwa na Chama Tawala za "Kujivua gamba".
Nape Nnauye moja ya Viongozi wa Kampeni za "Vua gamba"

Aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
     Wakati hilo likitokea bado Watuhumiwa kibao wa Ufisadi wa Chama hicho wanaendelea na Shughuli mbalimbali za Kichama na nyazifa nyingine za Kiserikali kama Kawaida. Kuendelea kufanya kazi kwa Wanachama hawa hakumaanishi kuwa CCM na Kampeni zake imewasamehe na kuwasahau kabisa; bali imefunga breki na kuanza kufikiri mchongo mpya wa kuwang'oa. Sifikirii kuwa Viongozi hao wapya na wenye shauku kubwa ya kukisafisha Chama wameridhia na mafanikio walioyapata ambayo yapo kinyume kabisa na dhamira yao ya Kujivua gamba. Kijana machachari katika Siasa ya Nchi hii Bwana Nape Nnauye na Mzee Mukama wamepata funzo kubwa la kutokukurupuka kuanzisha mkakati bila ya kuwa na Vitendea kazi. Yalionekana katika kampeni hizi ndiyo hayahaya yanayoonekana katika Sera nyingi za Serikali ambazo huwa nzuri na za kuvutia lakini hukosa njia za kuziwesha kufikia  lengo. 
      Ikumbukwe kuwa kuvuma kwa Kampeni za Kujivua gamba hakumaanishi kuwa CCM ndiyo imetakata bali hali itazidi kuwa mbaya zaidi kwa sababu hata kampeni hii isiyohitaji ushindani wa nafasi mbalimbali za Uongozi wa Nchi wameshindwa kutekeleza, Je sera na Mipango mbalimbali ya Maendeleo pamoja na Kuwapa Madaraka tena mwaka 2015 wataweza kutekeleza? Watanzania tukumbuke siku 90 zilizotolewa na Kamati Tendaji ya CCM Mapema Mwaka huu zilifikia lengo?
        Licha ya kuwa Meno ya CCM yameshindwa kuwauma baadhi ya Watuhumiwa wa Chama hicho bado Watuhumiwa hao wanawakati mwingine wa kutafakari kuhusu Mustakabali mzima wa Chama. Ni bora wajiengue mapema wenyewe bila hata ya mawazo ya kuwa wanatimiza matakwa ya dhana ya Kujivua gamba. Wanasiasa wa CCM hawana budi kuzisoma alama za nyakati. Kukaa kwa CCM madarakani muda mrefu hakumaanishi kuwa itatawala maisha. Wakumbuke kuwa Chama huongoza nchi kwa muda na pia hupoteza. CCM ikumbuke kuangushwa kwa Chama cha Institutional Revolutionary Party (PRI) Chama Tawala cha Mexico Mwaka 1997 ambapo kilikuwepo madarakani tangu Mwaka 1929 au Chama cha Congress cha India kilichoangushwa madarakani Mwaka 1977 kikitawala tangu Mwaka 1952. Hii ni Mifano tu CCM wanahitaji kuifahamu. Dominant Party System inaweza kupotea haraka sana na Watu wakaisahau. Hivi ndivyo CCM itakavyopotea na kusahaulika Miongoni mwa Watanzania iwapo wataendelea kutoa Sera na Michakato hewa na isiyo na tija kwa Watanzania.
       Watuhumiwa wa Ufisadi kutoka CCM pamoja na Viongozi wa kampeni  za Kujivua gamba hawana budi kujivua gamba kwa pamoja kwa sababu wanazidi kukipoteza na kukigharimu Chama. Baadala ya CCM kuwa na ngozi mpya na nyororo kama ilivyotarajiwa baada ya hizi kampeni itakuja kuwa na  Ngozi ngumu na yenye nundunundu hapo baadaye iwapo jitahada za ziada zisipo chukuliwa.
    Ili kulinda Heshima ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Heshima zao binafsi wale wote wanaosakamwa na Kampeni za "Vua gamba" hawana budi kujipumzisha kama Rostam Aziz. Heshima atakayoipata Rostam hapo baadaye itakuwa tofauti na hawa wanaong'ang'ania kukaa madarakani. Uchu wa madaraka utawaponza. Tunafahamu wengi wao ni Office seekers ndani ya Chama na si Message seekers kama inavyotakiwa kuwa ndo maana wapo radhi kudhaaririka. Lakini ubishi wa Vigogo hao ni furaha kwa Vyama vya Upinzani kutengeneza B52 za kuing'oa CCM.
      Ndugu zangu wapendwa, Kujivua gamba si Kujivua Uhai; Wanaotuhumiwa na Kampeni za Vua gamba wakubali kujivua kwani hawatapoteza Maisha bali wataongeza heshima ya Kisiasa na Masuala mengine ya Kimaisha kama Biashara na Mengineyo. Hata Hivyo nguzo zinazoishikiria CCM zimeanza kubomoka kazi kwenu Wapinzani kuukusanya Udongo na Kuufanyia Modifikesheni ili kuishika nchi mapema iwezekanavyo.





No comments:

Post a Comment