Thursday, September 6, 2012

Nani alizaliwa CEO, Director au Senior Manager?


Binadamu tunapitia katika hatua mbalimbali za makuzi toka utoto, utu uzima hadi uzee. Katika safari hiyo ya maisha hujikuta katika vipindi vigumu na vizuri kama hatua muhimu ya makuzi. Hata hivyo hatua hizo huwa ni changamoto kwa mtu husika awe mtoto, kijana au mzee. Kipindi kigumu katika safari hiyo ya maisha ya mwanadamu huwa ni “ujana”. Ujana ni sehemu ngumu sana ya maisha kwa binadamu kwa kuwa kijana huanza kupanga mikakati yake ya kujitegemea kwa kuanzisha maisha yake mwenyewe kwa kuvunja utegemezi na pia huhitaji mwenza wa kuendesha maisha yake.  Lakini swali huwa ni njia zipi atatumia kupata rasilimali za kumuwezesha kujitegemea yeye na familia yake mpya.

Enzi zile za zamani wazee wetu walipokuwa wakifikisha miaka 17 ua 18 na kuendelea walianza kujitegemea kwa kufanya shughuli za kilimo, uwindaji au uvuvi. Rasilimali zilikuwa za kutosha kiasi kwamba waliweza kutimiza mahitaji yao kwa wakati huo. Shule na ajira havikuwa kipaumbele sana kutokana na hali yenyewe ya maendeleo. Wachache sana waliobahatika kwenda shule ndio waliopata ajira za kufanya kazi serikalini kama walimu, askari, waganga au taaluma nyingine. Ajira za makampuni binafsi hazikuwepo sana kama ilivyo sasa pia kada zilikua chache sana tofauti na nyakati hizi ambapo kila uchwao kada zinaongezeka kutoka uhasibu wa kawaida (Accountant) mpaka afisa ugavi (procurement officer) kama kada tofauti. Ongezeko hili la utaalamu linaonekana kuwa nafasi adimu ya kuongeza ajira lakini hali si sawa na inavyofikiriwa.

Kwa maisha ya sasa  kijana yeyote aliyesoma elimu ya ngazi yeyote ile iwe cheti(Certificate), stashahada (diploma), astashahada (advanced diploma) au Shahada (degree) ni lazima awaze ajira. Ajira ndio chanzo kikubwa cha kipato kwa vijana na ni msingi wa kujitegemea. Lakini katika safari hiyo ya kutafuta ajira vikwazo vingi hujitokeza. Moja ya matatizo hayo ni uzoefu wa miaka kadhaa au lazima uwe na cheti halisi na si Provisional results au transcript. Swali linakuja hapa, je nani alizaliwa Mkurugenzi Mtendaji (CEO), Director au Meneja mwandamizi? 

Kwa mfumo huo wa kuajiri hakuna kijana ambaye atakuja kuwa CEO au Director miaka ijayo kwa kuwa uzoefu hana na hakufanikiwa kupata kazi mara tu alipohitimu masomo yake ambayo yangempa uzoefu. Pia, kwenye mfumo wa vyeti vya kamili vya chuo kikuu bado ni kikwazo. Vyeti vingi hutolewa baada ya mwaka mmoja na vijana wengi wahitmu huwa wanauwezo wa kufanya kazi japo vyeti vyao havijatoka. Je hao wafanye kazi zipi? Sambamba na hivyo hata cheti kikitoka baada ya mwaka mmoja atapataje kazi wakati hana uzoefu? 

Pia, lazima tukumbuke kuwa watu haohao wanaoandika masharti ya Vyeti halisi na uzoefu waliingia kwenye ajira moja kwa moja kutoka vyuoni miaka kumi iliyopita bila uzoefu wala cheti halisi. Hii ilitokana na kuwa walihitajika kufanya kazi haraka sana mara tu ya kumaliza masomo. Je, wao walikuwa bora zaidi walioshushwa na mungu kuweza kufanya kazi bila uzoefu na cheti halisi? Na kama hali ndo hivyo, je ni kitu kinachowafanya wao watoe vigezo vigumu vya kupata ajira? Au ndio woga wa kupoteza vibarua vyao kwa kuwa vijana wa sasa ni majembe kuliko wao?. 

Binafsi naona kuwa kuwa uchoyo, ubinafsi na fikra pungufu za watunga sheria na sera hizo ndo chanzo cha matatizo. Kwa sababu huwezi kutunga sheria au utaratibu wa kusubiri cheti baada ya mwaka mmoja halafu we mwenyewe ukawa wa kwanza kuhitaji uzoefu kazini na cheti halisi na si transcript au provisional results. Pia, huwezi kutunga sheria ya mafunzo kwa vitendo kuwa miezi miwili au kutokuwepo kabisa halafu ukahitaji uoefu, lazima wewe una matatizo. Lazima tufunguke kimawazo kwa suala hili, hivi hata hili tunahitaji kucopy kutoka uingereza?

Napongeza sana makampuni binafsi na baadhi ya taasisi za serikali zinazotumia mfumo wa kutafuta wafanyakazi vyuoni ili kuwapa uzoefu wa kikazi. Na nachukia sana menejimenti zinazowakataa vijana waliohitimu masomo na wana uwezo wa kufanya kazi zaidi ya hata waliomo maofisini mwao. Ni uzamani na kuwa na falsafa y a kizamani ambayo haiendani na mfumo wa sasa wa sayansi na technolojia unaohitaji ufanisi zaidi kazini. Tumeshuhudia makampuni mengi yanayoendeshwa na vijana yakifanikiwa zaidi kuliko hata ya wale wazee ambao wanakataa vijana kufanya nao kazi. Kwa kufanya hivyo ni kuzuia kuandaa maCEO na madirectot wa kesho.

Tufunguke kifra, kifalsafa na kitaaluma kuwa binadamu si mawe kuwa wakashindwa kujifunza na kuzoea mazingira. Kufanya kazi bila uzoefu wa miaka kadhaa na kuwa na transcript au provisional results inawezekana. Tuanze sasa. 

Pia, ijulikane kuwa ili vijana tuzuie utegemezi wa ajira za masharti yasiyo kuwa na mashiko kama hayo lazima tuwe wabunifu wa kuandaa biashara zetu wenyewe japo kwa mitaji ya kuungaunga. Hao wanaokuona leo huwezi watakutafuta wenyewe ukiwa kwenye biashara zako au kampuni ukiliendesha kwa mafanikio makubwa. Si lazima uwapigie magoti. 

Ifahamike kuwa elimu ya juu ni chombo cha kutatua matatizo magumu katika maisha ya mwanadamu na si kuchochea kuwa mvivu wa kufikiri au kuendeshwa kimawazo.  Tujitambue!


Maoni haya ni yangu binafsi hayahusiani na mtu yeyote wala msimamo wa kundi la watu Fulani. Unaweza kuyafanyia kazi ukivutiwa nayo na si lazima utoe malalamiko ya kutoridhishwa nayo.

No comments:

Post a Comment