Ndani ya mwezi mmoja watanzania tumeshuhudia mfulululizo wa
ajali mbaya za mabasi ya masafa marefu zilizogharimu maisha ya watu zaidi ya 50
na kuwaacha wengine wakiwa majeruhi.
Tofauti na ajali zilizokuwa zikitokea miaka ya nyuma, ambazo
waharifu walikuwa wakiiba mali za majeruhi na marehemu, safari hii kuna aina
mpya ya uhalifu: uzalilishaji.
Mara tu baada ya ajali hizo kutokea baadhi ya watu aidha
walionusurika au mashuhuda walijikuta wakiacha kusaidia majeruhi na kurekodi
video au picha za kutisha na kuweka mtandaoni.
Asilimia kubwa ya picha hizo zimesambaa kwa kasi sana ndani
ya majuma matatu haya na sasa zimekuwa zikipatikana kwa haraka bila hata
kuangalia utu wa majeruhi au marehemu hao.
Dakika chache baada ya kugongana mabasi mawili ya Mwanza
Coach na J4 Express hivi karibuni mkoani Mara, baadhi ya picha za maiti
waliotolewa ndani ya magari hayo zilisambazwa zikionyesha wamelala chini bila
hata ya kufunikwa.
Sanjari na picha hizo,
pia kulikuwapo na nyingine ilionyesha watu wawili wakiwa wananing’inia kwenye
moja ya mabasi hayo baada ya sehemu za miili kunasa kwenye viti.
Picha hiyo ambayo inaonyesha maiti hao--wanaoweza
kutambulika--wakiwa wamening’iniza vichwa vyao mtawalia huku damu nyingi
zikichuruzika.
Pia, siku kadhaa baada ya ajali hiyo, ilitokea nyingine
wilayani Kilosa ambayo iliua watu wanne na kujeruhi 35 baada ya basi walilokuwa
wakisafiria kutoka dar es Salaam kwenda Tabora kuanguka eneo l la Berega.
Kama ilivyoa ada, watu hao ‘waandishi wa habari’ wa kisasa
walisambaza tena picha za marehemu wanne wakiwa wamelazwa chini baada ya ajali.
Ndani ya saa 24 tena iklitokea ajali nyingine katika eneo la Tangi
Bovu Jijini Dar es Salaam ambapo Lori lilipita basi na kuwagonga vibaya mwendesha
pikipiki na abiria wake.
Mwili wa dereva ulitupwa mtaroni wakati ule wa abiria ulichubuliwa
na kugawanywa nusu baada ya kuburutwa na gari hilo.
Kama mchezo tena , picha za ajali hiyo zilisambazwa katika
mitandao ya kijamii kama blogu, Whatsapp, facebook, Twitter na mingineyo.
Pamoja, na uwingi wa mitandao hiyo, matumizi ya whatsapp ndiyo yamezidisha hali
hiyo na inaonyesha jinsi gani Watanzania tulivyochanyikiwa na teknolojia ya
mitandao ya kijamii.
Wengi tunaotumia mitandao hiyo hapana shaka tumeshatumiwa au tumeziona
picha hizo tena zaidi hata ambazo nimezitumia kama mfano.
Katika ulimwengu wa dijitali ni dhahiri tunatakiwa kwenda na
wakati hususan mabadiliko ya teknolojia. Hata sisi waandishi tunaofanyia katika
vyombo vya habari vilivyo na sera zake na kuaminika kwa jamii tunapaswa kufanya
hivyo lakini kwa kuzingatia maadili na utu wa watu.
Matumizi ya mitandao ya kijamii hayaepukiki katika kutoa
habari za haraka lakini ni lazima tuheshimu utu wa Watanzania au yeyote yule
ambayo anakutwa na maafa.
Usambazaji wa picha za kutisha na zinazozalilisha marehemu
katika mitandao unatishia usalama wa taifa na unatia hofu kuwa Watanzania
hawajali tena ndugu au rafiki zao.
Naamini wengi wanaopiga picha hizo hawajakutwa na majanga kama
hayo kiasi cha mama, baba, kaka au wajomba zao kupatwa na ajali na miili yao
kuwa miongoni ya ile inayoisambazwa katika mitandao.
Kuweka picha katika mitandao hiyo kunaziumiza kisaikolojia
familia za ndugu waliopoteza maisha hasa zile zinazooneka wazi na katika hali
isiyotakiwa kuoneshwa kwa mujibu wa mila zetu.
Pia, kunatia hasira kiasi cha kutengeneza kisasi iwapo ndugu
hao wakibaini msambazaji na kuleta mambo ambayo taifa la umoja na upendo kama
letu hatutaka tushuhudie.
Binafsi sipingani na uchukuaji wa picha za matukio hayo
lakini uangalifu mkubwa unatakiwa kulinda heshima zetu na amani yetu kwa
kusambaza picha ambazo haziogopeshi au kuzalilisha watu kama inavyoendelea
nchini.
Nchi zilizoendelea, ambako teknolojia ya mitandao ya kijamii ilianzia,
usambazaji wa picha kama hizo umepitwa na wakati na wameona haufai kwa ustawi
wa taifa.
![]() |
Mitandao ya kijamii kama hii itumike kutuunganisha sio kubomoa uhusiano wetu. Picha hisani ya socialmediamarketing.com |
Wakati wa maafa kama hayo wenzetu hujumuika kwa pamoja na
kutumia mitandao hiyo kukusanya michango ya fedha na damu kuchangia matibabu na
kuokoa maisha ya majeruhi.
Mfano mzuri ni nchini Kenya. Baada ya Shambulio la duka la
Westigate na magaidi wa Alshabab Septemba mwaka jana, Wakenya waliungana na
kuchangia damu na mali hadi majeruhi walipopata nafuu; hakuna aliyeweka picha
ya marehemu akikenua meno baada ya kuuawa…kwanini sisi tunadhalilishana!?
Ifike kipindi tuache ushamba wa mitandao na utumiaji wa
kamera ovyo kuzalilisha marehemu na majeruhi. Yatupasa kuvivaa viatu vya watu
na familia zao na namna wanavyoumia kwa picha hizo kusambaa ili kutokomeza tabia
hiyo.
Makala haya yalichapishwa awali Jumanne, 16 katika gazeti la Mwananchi.