Moja ya
vipindi vigumu kwa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) mwaka
huu ni hiki inapotakiwa kufanya aumuzi wa kutangaza nauli mpya za usafiri wa
umma.
Kwa kipindi
cha miezi sita sasa mamlaka hiyo imekuwa aking’ang’anizwa na wadau na viongozi
serikalini ishushe nauli kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la
dunia.
Pamoja na
Sumatra kupinga mara kadhaa kuwa mabadiliko yasingefanyika haraka kwa sababu
mafuta hushuka na kupaa kwa muda mfupi, wadau hao wakiwemo Baraza la Kutetea Watumiaji
wa Uchukuzi (Sumatra CCC) walizidi kuongeza presha ya kushusha nauli.
Sumatra ilishasisitiza
kuwa bei ya mafuta inachukua sehemu ndogo tu ya vigezo vya ukokotoaji nauli
mpya na zipo gharama nyingine za uendeshaji kama vipuri, bima, mishahara, kodi
na mengineyo.
Ni dhahiri
kuwa kwa zaidi ya miezi sita wamiliki wa daladala na mabasi ya masafa marefu
walipata faida zaidi baada ya kushuka kwa mafuta pasina nauli kushuka na wananchi
nao walinyimwa unafuu wa nauli ambao ungesaidia kukuza shughuli zao za
kiuchumi.
Tofauti na
miaka iliyopita, katikati ya mwaka jana hadi Machi mwaka huu mafuta yalishuka sana kiasi cha Petroli kufikia Sh1,650 jijini Dar es Salaam, bei ambayo ilifikiwa
miaka minne iliyopita.
Baada ya mashinikizo,
Sumatra ilianza kukusanya maoni ya wadau kama sheria inavyowataka ili kupata
mitazamo tofauti ya kutekeleza zoezi hilo.
Katika mkutano
uliofanyika Dar es Salaam Machi 18, wamiliki daladala walipinga ushushaji nauli
wakihofia mafuta yangepanda bei zaidi na wakatishia iwapo nauli itashushwa,
wataanzsisha nauli kwa askari wa majeshi yote.
Wakati
Sumatra ikiyafanyia kazi maoni na kufuatilia hali ya soko, Waziri wa Uchukuzi,
Samuel Sitta wiki iliyopita aliigiza tena mamlaka hiyo kuharakisha majadiriano
na wadau na kisha kutangaza nauli mpya ndani ya juma hilo. Hata hivyo, mpaka
sasa nauli mpya hazijatangazwa.
Presha kama
hizo ni changamoto na kipimo cha uweledi na ufanisi kwa mamlaka za udhibiti
nchini. Kuna kila dalili pia kuwa Sumatra inahofia kufanya uamuzi huo isionekane
ya ‘kijinga’ na isiyofuata uweledi kutokana na hali halisi ya soko dhidi ya
siasa.
Kama Wachumi
wengi walivyoonya awali, bei ya mafuta imeanza kupanda tena hata kabla ya nauli
mpya kutangazwa. Petroli mwezi huu, Dar es Salaam inauzwa Sh103 zaidi ya bei ya
Machi ya Sh1652. Dizeli imepanda kwa Sh109 na Mafuta ya Taa kwa Sh132.
Shilingi
nayo imezidi kuporomoka kutokana na kuongezeka thamani ya Dola ya Marekani
ulimwenguni na sasa Dola moja inabadilishwa kwa Sh1, 850. Vipuri na mabasi huingizwa
nchini na wafanyabiashara wake huathiriwa sana na udhaifu wa thamani ya
Shilingi.
Hali ya
kisiasa mwaka huu inayohusiana na Uchaguzi Mkuu inaweza kuathiri mwenendo wa
kiuchumi kutokana na wawekezaji wengi kuhofia hatari za kiuwekezaji na
mabadiliko ya kiutawala yanayoweza kutokea.
Pia, kuna
kila dalili bei ya mafuta ikazidi kupanda. Takwimu za Benki ya Dunia (WB)
zinaonyesha wastani wa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia kwa mwezi
Februari iliongezeka hadi Dola za Marekani 54.93 (Sh101, 600) kwa pipa kutoka
bei ya chini kuliko zote kwa miaka mitano ya Dola 47.45 (Sh87,780) kwa pipa
mwezi Januari mwaka huu.
Ripoti ya Machi,
2015 ya nchi zinazozalisha mafuta sana ulimwenguni (Opec) inaonyesha mahitaji
ya mafuta duniani mwaka huu yataongezeka kwa mapipa 1.17 milioni kwa siku na
kufanya wastani wa mahitaji ya jumla kwa siku kuwa mapipa 92.37 milioni. Hii
itapandisha bei ya nishati hiyo licha ya Marekani na Canada kwa kuzalisha
mafuta mepesi mengi zaidi kwa bei ndogo.
Kwa mantiki
hiyo na ukiachana na siasa, uamuzi wa Sumatra kushusha nauli ni mtego usiofanana
hata kidogo na kipindi cha mabadiliko ya nauli mwaka 2009.
Iwapo
Sumatra italazimishwa, itaingia kwenye mgogoro na wasafirishaji na kuwapa
wananchi ahueni ya muda mfupi tu.
Mfumo mzuri na
wa haraka wa ukokotoaji nauli uendao na soko ni kama unaotumika na Ewura
kukotoa bei ya mafuta kila mwezi. Huo ungewaepusha Sumatra na kadhia na presha
za kisiasa.
Sumatra
ingekuwa inapitia nauli angalau kwa miezi sita au mwaka kuepusha unyonyaji kama
ulitokea hivi karibuni kwa wananchi kwa kushindwa kushusha nauli haraka kwa
mujibu wa mwenendo wa soko la mafuta.
Nuzulack Dausen ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi anapatikana
kupitia ndausen@tz.nationmedia.com au Twitter: @nuzulack
No comments:
Post a Comment