Njia za kutatua Migomo Vyuo Vikuu Tanzania hizi hapa.
MAONI
YANGU KWA UTAWALA WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM JUU YA NAMNA YA
KUONDOA AU KUPUNGUZA MIGOMO NA MAANDAMANO YANAYOONEKANA KUONGEZEKA KILA
KUKICHA.
Na: Ole Mesaya
Tatizo la migomo na maandamano ndani ya chuo kikuu cha Dar
es salaam halijaanza hivi karibu. Tatizo hili lilikuwepo toka enzi
lakini kwa miaka ya hivi karibuni limeonekana kushika kasi zaidi na
kupelekea chuo kupoteza rasilimali nyingi na kuwatimua chuo wanafunzi
wote ambao wanaonekana kuwa ni chanzo cha tatizo hili. Pamoja na
jitihada zote hizi zinazofanywa na uongozi wa chuo bado tatizo hili
limeonekana kutokoma, zaidi wanafunzi wengi wanazidi kupotea na
rasilimali nyingi zinatokomea bila mafanikio.
Ningependa kuchukua
nafasi hii kama mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam kutoa maoni
yangu juu ya nini kifanyike ili kupunguza kama sio kutokomeza kabisa
suala la migomo ndani ya chuo chetu.
I. Kwanza kabisa Chuo pamaja na
taasisi zinazohusika zijitahidi kukabiliana na kutatua matatizo
yanayowakabili wanafunzi kwa njia ya majadiliano na kwa haraka zaidi na
siyo kusubiri mpaka mgomo au maandamano kutokea. Tofauti na ilivyo sasa
hivi, ambapo taasisi zinazohusika zinasubiri mpaka mgomo utokee ndipo
wachukue hatua za kukabiliana na mgomo badala ya kuchukua hatua hizo
kukabiliana na matitizo hayo kabla mgomo haujatokea.
II. Chuo
kiangalie zaidi na kijikita kwenye vyanzo vya migomo, ikiwa ni pamoja na
sababu ya mgomo kutokea kuliko kujikita na kuwapa adhabu wanafunzi
wanaoanzisha na kushiriki kwenye mgomo huo. Kwa kufanya hivyo chuo
kitakuwa kimezuia uwezekano wa mgomo mwingine kutokea kuliko ilivyo sasa
ambapo chuo kinawapa adhabu, ikiwepo kuwafukuza chuo wanafunzi
wanaooekana kushiriki kwenye mgomo ilihali tatizo lilosababisha mgomo
likibaki bila muafaka.
III. Chuo kiweke utaratibu ambao utawalazimu
viongozi wa serikali ya wanafunzi kukutana na wanafunzi na kujadili kwa
pamoja juu ya matatizo na changamoto zinazowakabili wanafunzi angalau
mara tatu kwa muhula wa masomo yaani mwanzo, katikati na mwishoni mwa
muhula wa masomo. Tofauti na ilivyo sasa ambapo school baraza ipo mara
moja tu kwa mwaka na mara nyingi imekuwa haifanyiki. Kwa kufanya hivi
wanafunzi wataweza kuwasilisha changamoto zinazowakabili kwa uongozi wao
na hoja hizo kuwasilishwa panapohusika haraka na mapema zaidi.
IV.
Chuo kikuu kifanywe kitovu cha kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto
zinazoikabili nchi yetu. Hii itawezekana kama chuo kitaweka utaratibu
wa kuruhusu jukwaa la malumbano ya hoja baina ya wanafunzi angalau kila
jumamosi ya mwisho wa wiki, kwani hii itawapa nafasi vijana na wasomi wa
vyuo vikuu kushiriki katika harakati za kukabiliana na changamoto
zinazoikabili nchi yetu. Kwa kufanya hivyo chuo kitakuwa kimeondoa
uwezekano wa wanafunzi kufanya mikutano isiyo ya halali kama ilivyo sasa
kujadili mwenendo na hatma ya taifa letu.
V. Ilivyo sasa, Chuo
kinatumia rasilimali na nguvu nyingi kupambana na wanafunzi. Kwa kufanya
hivi Chuo kitakuwa kinapambana na wahanga wa tatizo huku tatizo
likiendelea kushamiri na kunawiri pasipo kutafutiwa ufumbuzi wa
kuliondoa tatizo lenyewe. Kwa maoni yangu chuo kingetumia nguvu hizo na
rasilimali hizo kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi,
kwani kama wataendelea kupambana na wanafunzi na kuliacha tatizo
likiendelea kukua ni dhahiri shairi kwamba migomo na maandamano kamwe
hayatakwisha kwani chanzo cha mgomo bado kipo na kinaendelea kukua.
VI. Pindi mgomo au maandamano yanapotokea, chuo kijikite zaidi kwenye
tatizo lililosababisha mgomo kuliko kukimbilia kuhusisha matatizo
yaliyosababisha mgomo na vyama vya siasa. Kwani kufanya hivyo kamwe
hakutakuwa na suluhisho la migomo na maandamano, kutokana na kwamba
tatizo halisi litakuwa limeachwa kwa kujikita kwenye hoja isiyo ya
msingi.
VII. Pindi adhabu inapotolewa na chuo, Chuo kijitahidi
kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuondoa malalamiko
miongoni mwa wanafunzi pamoja na wale waliopewa adhabu. Kwa mfano
wanafunzi wapewe adhabu baada ya kuhojiwa na kusikilizwa ushahidi wao
badala ya kufuata hisia na hasira kama ilivyo sasa.
VIII. Uongozi
na utawala wa chuo usikimbie changamoto bali watumie changamoto hizo
kama vyanzo vya uwajibikaji. Tofauti na ilivyo hivi sasa, wenye madaraka
ndani ya chuo kikuu wanakwepa changamoto zinazowakabili wanafunzi kwa
kuogopa kupoteza nafasi zao za madaraka endapo wataungana pamoja na
wanafunzi kuwasilisha changamoto hizo panapohusika.
IX. Serikali ya
wanafunzi DARUSO iwe chombo huru na kinachotambuliwa na kuheshimiwa na
utawala wa chuo kikuu cha Dar es salaam. Ilivyo sasa, serikali ya
wanafunzi DARUSO haitambuliwi wala kuheshimiwa na utawala wa chuo kwani
katika hatua zote za kinidhamu zilizochukuliwa na utawala wa chuo kwa
wanafunzi, serikali ya wananfunzi haijajulishwa kimaandishi. Mfano barua
zote za kuwasimamisha na kuwafukuza chuo wanafunzi hakuna nakala yoyote
iliyopelekwa kwa serikali ya wanafunzi.
Ni matumaini yangu kwamba
kama tutashirikiana kwa pamoja kuyatekeleza haya, siyo siri tutakuwa
tumepunguza kama siyo kutokomeza kabisa mianya yote inayosababisha
migomo na maandamano na kushusha heshima ya chombo hiki cha umma.
Asanteni.
Maoni haya yamenivutia sana mpaka nimeona niyachapishe hapa ili wahusika waweze kuchukua chochote wanachoona kinafaa kutatua Migomo Vyuo Vikuu nchini hususani Utawala wa Vyuo hivyo na Serikali. Pia serikali za Wanafunzi kama DARUSO, IFMSO, UDOSO na zingine zisome makala hii kujiongeza. maoni haya ni mali ya mwandishi Bwana ole Mesaya pichani juu. Yametolewa toka kwenye Ukurasa wa facebook wa UDSM. Bofya hapa kujiunga
No comments:
Post a Comment