Wasalaam kipenzi changu, mke wangu mtarajiwa.
Popote ulipo pokea salamu zangu hizi za dhati zisizo na tone
la unafiki. Najua utakuwa umeshtuka kwanini nimekutumia barua hii leo, saa kadhaa
kuelekea siku ya Wapendanao ambayo wazungu wanaiita Valentine. Usishtuke,
nimekuletea zawadi yako maridhawa, kuwa mtulivu.

Inakuuma kutokuwa miongoni mwa hao thenashara lakini vumilia.
Maisha sio maji ya mto yanayofuata mkondo wake. Maisha ni safari na waliombele
ndiyo wanaowahi kufika bila kujali wamefika na kupata nini.
Bila shaka ulitegemea kupokea zawadi nzuri za maua mazuri ya
waridi yaliyopulizwa manukato yenye rehe nzuri lakini kwa bahati mbaya ni haka
kabarua ambako nimesahau kupulizia hata manukato ya ‘Nivea for Men’. Umakini
wako kuisoma barua yangu kwa moyo ni zawadi tosha, zawadi nzuri kuliko hata Blackberry,
Galaxy Note 4, Vits, IST au safari ya kutembelea visiwa vya Sanane na Zanzibar.
Najua masomo hayaendeki au kazi hazifanyiki huko uliko na
unatamani siku ya Valentine iwe fupi, iishe na uachane na ‘mashida’ ya wenzio
wanaoweka ‘status’ (ujumbe) mzuri na Selfie na wapenzi wao katika akaunti zao
za Whatsapp, Instagram na Facebook.
Tuliza moyo na amini mimi nipo japo hatujawahi kuonana. Futa
machozi na usiwaze kulazimisha penzi na mtu ambaye hakupendi, mimi nipo ila
wasaa ulikuwa hauujafika wa kuanzisha uhusiano.
Naomba nisikuchoshe sana na maneno ya utangulizi yasiypunguza
hata kidogo maumivu ya kovu la kuwa ‘single’ kwa sasa kwa sababu tu yule bepari
mwenye gari uliyempenda alikuhadaa kuwa angekuoa lakini kumbe alikuwa na mke na
watoto watatu. Au upo single kwa sababu tu vijana wanaoukuja bado hawajielewi
au hawajaonyesa nia ya kukuoa na kukucheleweshea kamda kako ka kuolewa.