Ni kawaida
kwa vijana wengi nchini kuwa na ndoto lukuki za mafanikio wanapoingia vyuo
vikuu na vyuo vya kati. Asilimia kubwa huamini kozi wanazochagua na kusomea
zitawapatia mafanikio ya haraka zaidi katika maisha.
Dhana hiyo
huwafanya kuchagua kozi nzuri ambazo wakihitimu bila shaka watakua mameneja au
watu wenye nafasi nzuri zaidi katika kampuni au mashirika makubwa ya umma.
Katika
mawazo hayo ya ‘kusadikika’ huwa kuna mipango mingi ya kutekeleza mara baada ya
kumaliza elimu zao ikiwamo kupata kazi haraka katika kampuni wanazotarajia
kufanya, kuoa au kuolewa na wachache sana huwaza kuwekeza.
Hata hivyo
mambo huwa ni magumu pale wanapomaliza stashahada au shahada zao kwa kukosa
ajira ambazo huaribu mipango mingine yote. Kwa kiasi kikubwa ajira ndiyo msingi
wa mipango mingi ya vijana hivyo ikikosekana kila kitu kinazama.
Nakumbuka
hata mimi nilipata wakati mgumu kuchagua kozi ya kusoma kutokana na ushawishi
mkubwa niliokuwa na upata kwa wakubwa zangu kuchagua masomo waliyoyaita ya
‘pesa pesa’.
Katika kundi
la watu wote waliokuwa wakinishauri hakuna aliyeniambia kuwa nikienda kusoma
Mlimani nitumie masomo hayo ili niweze kupata ufahamu wa kuwekeza.

Hakuna
aliyethubutu kuniambia kuwa nikiwa shule nitunze fedha kidogo ntakazokuwa
napata kwenye mkopo wa elimu ya juu au kutafuta ‘dili’ za muda mfupi
zitakazoniongezea kipato kitakachosaidia kuanzisha biashara zangu.
Aina hiyo ya
ushauri inazidi kuangamiza asilimia kubwa ya vijana nchini hasa wanaobahatika
kupitia vyuo vikuu. Dhana ya kijamaa ya miaka 35 iliyopita ya kupata kazi baada
ya chuo bado inatutafuna na kutufanya tuwe watumwa wa ajira.
Vijana wengi
tumekuwa waoga wa kujaribu kujiajiri na kujikuta tunabaki mtaani hata baada ya
kuhitimu kozi nzuri za biashara. Baadhi yetu hata kabla ya kujaribu kutafuta
mawazo ya biashara tunakatishwa tamaa na nafsi zetu kuwa hatuwezi na hakuna
vyanzo vya fedha kutuwezesha.
Hofu hiyo
kama hiyo ndiyo anayoiita aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
Ludovick Utouh, kuwa ni matokeo ya kutobadilika ya mawazo ya muda mrefu ya
kijamaa. Ni sehemu ya utegemezi wa kufikiri kila kitu kinafanywa na serikali na
kuwapatia wananchi mambo mazuri.
Kizazi chetu
kimebatika kuishi katika ulimwengu wa habari tele za biashara na uwekezaji lakini
ni wachache sana wanaoweza wakatulia na kompyuta zao mpakato au simu wakasoma
habari kama hizo.
Aina hiyo ya
mawazo itaongeza idadi kubwa ya vijana wasio na ajira ambao baadhi ya wanasiasa
wanaliita tatizo hilo kama bomu linalosubiri kulipuka. Iwapo kila mwaka
wanahitimu zaidi ya 1 milioni na kuingia kwenye soko la ajira, na asilimia
ndogo tu ndiyo wanaajiriwa kuna umuhimu mkubwa kujifunza kuwekeza.
Lakini mawazo
na tabia ya kusubiri ajira yanaweza kuondolewa miongoni mwa vijana iwapo
tunaweza kufanya yafuatayo;
Mosi,
kujenga tabia ya kuwekeza kidogo kinachopatikana wakati tukiwa masomoni. Ni
dhahiri kuna baadhi ya vijana wana matatizo ya kifedha lakini pia wapo wenye
fedha kidogo zinazoweza kukusanywa taratibu benki pale wawapo masomoni
zitakazowasaidia kupata mitaji watakapomaliza vyuo.
Ukikusanya
Sh3 milioni kwa miaka mitatu itakayotokana na kuhifadhi kiasi kidogo cha pesa
zako na kufanya vibarua bila shaka inaweza kusaidia kuanzisha biashara yoyote
itakayosaidia kuishi mjini.
Pili,
usomaji wa taarifa mbalimbali utasaidia vijana wengi kupata taarifa za namna ya
kuanzisha biashara kutoka kwa watu mbalimbali wenye uzoefu. Binafsi nimejiunga
na mtandao kibao inayotoa mafunzo ya ujasiriamali kama yes.com, Forbes,
Vijanatz.com, Buni hub na mingine lukuki.
Kwenye
vyanzo hivyo vya habari unaweza kupata taarifa nyingi zikiwemo namna ya kupata
mitaji kwa kuanzisha mawazo mazuri ya biashara. Kuna wawekezaji lukuki
wanatafuta vijana wabunifu watakaokuja na mawazo mazuri ya biashara yatakayoleta
faida kubwa kwa mwekezaji na jamii.
Tatu, kuunda
mtandao wa vijana wenye malengo ya kibiashara kunaweza kutuepusha na bomu.
Vijana tunatakiwa tuwe na uhusiano wa karibu wa kibiashara kwa kuunda mtandao.
Aina ya mtandao kama huo unaweza kusadia kuunda wazo, kuwakutanisha na taasisi
za kimataifa na za ndani zinazotoa mitaji isiyo na riba kwa njia ya ushindani
wa mawazo. Pia, kupitia kikundi ni rahisi kuomba miadi na wajasiriamali wakubwa
ili kupatiwa mafunzo ya kutoka kibiashara. Katika soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kuna wawekezaji lukuki wanaotafuta maeneo ya kuwekeza ila hawajapata
mawazo na kumpuni nzuri za chini na
kati.
Mbinu kama
hizo zinaweza kuwatoa vijana woga katika kufanya biashara na hatimaye kupunguza
idadi ya wanaotegemea ajira. Kama asilimia kubwa ya vijana waliosoma watakuwa
wanawaza ujasiriamali basi kuna kila dalili kuwa ajira nyingi zitatengenezwa na
kupunguza kundi la wasio na ajira wenye elimu na ujuzi.