Nuzulack Dausen
Twitter: @nuzulack
Kwako mke
wangu mtarajiwa. Valentine imewadia tena.
Najua bado
una huzuni na wasiwasi nimekutelekeza. Una hofu na miaka inavyokwenda kasi bila
kunipata mimi, kipenzi chako cha kweli.
Rafiki zako
ambao mwaka jana walikuwa waseja kama wewe, tayari wameshaolewa ama kuchumbiwa.
Na wewe umeshiriki kikamilifu kuwaoza.
Lakini bado
wanisubiri nifike, nije kukuoa licha ya kuwa miaka inazidi kuyoyoma. Hujakata
tamaa.
Nafahamu
bayana mabarobaro wengi hujipitisha pitisha na kukulaghai uwakubali. Lakini moyo
wako u thabiti na hujawapa nafasi. Ndoto yako ya kuwa na mimi imekutawala siku
zote.
Mwaka jana
nilikusihi usifadhaike wakati wa sherehe za valentine. Nilikusihi usisitetereke
na rafiki zako waliokuwa wakiringa kwa zawadi walizopewa na mabwana zao. Mwaka
huu pia Valentine inabisha hodi.
Hujapata
zawadi yoyote wala ujumbe mzuri kwenye simu yako. Ungetamani umpate mtu wa
kukubembeleza ukichoka na kazi na wakati ukiumwa.
Ungetamani uwe
na mfalme wa moyo wako ambaye muda wote angekuwa na wewe akikujali na kukupa
mapenzi moto.
Kiufupi,
unamtaka mume wa kukufanya mke mwema na chaguo la kweli. Lakini bado giza
linakuzuia usione nuru. Nuru ya maisha mapya ya kuwa wawili na kutekeleza
masharti ya vitabu vya dini.
Tafadhari
vumilia. Hata Valentine hii imefika na
hujaniona, usifadhaike. Narudia usikate tamaa. Nipo nakuja japo sijafika karibu
yako. Sidhani kama ni Valentine hii lakini utaniona.
Usitishike
na rafiki zako wanaokutambishia zawadi za smartphone walizopewa na mabwana
wanaotaka kuwachezea. Wala usibabaike na selfie zao wanazoweka mtandaoni
wakiweka ‘status’ za “Ready for Valentine (Tayari kwa valentine).”
Mimi ndiyo
zawadi yako ya kweli. Zawadi ya kudumu ya maisha yako. Duniani na mbinguni.
Upendo wangu kwako ni zaidi ya zawadi ya smartphone au Vitz. Upendo wangu
haubanwi na muda eti mpaka siku ya Valentine pekee la hasha. Mimi ni wako siku
zote.
Nakupenda
kila siku japo hatujawahi onana. Nakuw
aza wakati wote na nakupenda kutokana na
uzuri wa asili ulionao, heshima, upole, werevu, ubunifu na uvumilivu wako.
Siyo mapepe
wala waruwaru wa kukufanya nyumbani kwetu wakukatae. Huropoki ovyo na
kulalamika mara kwa mara mbele za watu hata kama mtu kakukosea mara 1,000. Huvai
nguo za vipisi zikakuonyesha maungo yako kana kwamba upo sokoni.
Huweki nyusi
za bandia na kujisiliba rangi tofauti usoni ukaonekana kama kichekesho mbele za
watu. Hujawahi waza kuweka makalio ya ziada kwa sababu una uhakika mimi situmii
maumbo hayo kama kigezo cha mwanamke mzuri.
Hutumi mara
kwa mara picha mtandaoni kuonyesha unaponda raha kwa kuwa unajua mwanamke bora hupenda
kusitiri mwenendo wa maisha yake binafsi na ya nyumbani.
Hakika wewe
ndiyo Valentine wangu. Na mimi ndiyo Valentine wako wa kweli. Nisubiri nije
nikupoze moyo. Nivumilie kidogo tu. Nikifika, sitachelewa, nitakutolea posa na
kukuoa.
Nikutakie
heri ya wapendanao huko uliko japo kila siku hufanya hivyo. Nakupenda mchumba
wangu.