Na: Nuzulack J. Dausen
Hali si shwari katika mji mdogo wa Madibira wilayani Mbarali. Matukio mengi ya wizi na ujambazi ndio yanashika kasi katika mji huu. Amani na upendo wa awali vimetoweka, sasa ni unyamaunyama na pesa ndio sabuni ya roho. Zimepita wiki mbili tu toka tukio liloibua hisia za wengi kupitia vyombo vya habari kutokea katika mji huu. Tukio hili ni lile lilohusisha mganga na mteja wake walioshiriki kuua raia mwenzao kama njia ya kujipatia dawa.
Kabla ya tukio hilo miezi kumi iliyopita palitokea tena tukio kubwa la ujambazi ambapo watu wasiofahamika waliteka mtaa wa maduka katika kijiji cha Mkunywa na kuvamia duka la Mfanyabiashara mmoja anayejulikana kwa jina la bwana Charles Mohele na kutokomea na kitita cha mamilioni ya fedha. Hata hivyo jumuiya ya Wafanyabiashara wa mji huu walikaa kikao kwa kushirikiana na Serikali na kuanzisha Ulinzi shirikishi. Ulinzi ambao tuliamini ungekuwa mzizi wa masuala ya wizi na ujambazi lakini haikuwa hivyo kama ilivyotegemewa.
Hali ilitulia kwa muda katka mji huu huku wizi mdogomdogo ukiendelea kutokea majumbani mwa raia kila uchwao. Jeshi la polisi na Serikali ya za mitaa vipo katika mji huu lakini hali si shwari. Wananchi wengi wa mji huu wanadai kuwa Kituo cha Polisi kipo mbali sana na mitaani wanapokaa raia wengi ambapo matukio mengi ya wizi yanatokea. Akiongea na blog hii mmoja ya wakazi wa mji ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema " Tatizo kubwa la hawa polisi wetu tunashinda nao humu baa muda mwingi kwa hiyo hata matukio yakijambazi yakitokea tunakuwa nao pamoja kujiokoa na si wao kutuokoa pia hata waliopo kituoni huwa wachache sana sababu inayoleta ugumu hata kuwaomba msaada wakati wa shida kama hiyo"
Kwa takribani miaka kumi hivi mji huu umekuwa maarufu sana kwa kuzalisha zao la mpunga na idadi ya watu mbalimbali imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Katika ongezeko hilo la watu, matukio ya hatari nayo yameongezeka.
Tukio la kusikitisha zaidi ni hili lilotokea usiku wa kuamkia tarehe 22 mwezi huu katika mtaa wa kichangani katika kijiji hicho cha Mkunywa. Tukio hilo linahusisha mauaji ya moja ya wafanyabiashara maarufu katika kijiji hicho aliyeuwa kinyama na majambazi usiku huo. Marehemu huyo aliyefahamika sana kwa jina la Msigalah alikutwa na mauti nyumbani alipopanga katika mtaa huo kwa Mzee Euzebio Mhimba. Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Makambako mtoto wa mwenye nyumba hiyo Bwana Emmanuel Mhimba anasimulia kuwa "Ilikuwa usiku wa saa saba au saa nane ambapo walivamiwa na majambazi na kufungiwa vyumba vyao kwa nje. Azma kubwa ya majambazi hayo ni kutaka kuchukua fedha kwa bwana Msigalah hata hivyo hakuwanazo kwa wakati ule hatimaye walimuua kwa kumjeruhi vibaya na siraha. Hata hivyo mke wa marehemu hawakumuua ila alipata majeraha kiasi".
Kutokana na tukio hilo la kusikitisha na lilorudisha nyuma maendeleo ya mji huu kwa sababu marehemu alisaidia sana kusambaza umeme kijijini hapo na kwa sasa huduma hiyo haipo tena. Huzuni imetawala mji huu, Uchumi unatarajiwa kushuka sana sababu ya kutopatikana kwa nishati hiyo muhimu katika maendeleo.
Wadau mbalimbali wametoa maoni kwa Serikali ya Mkoa kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali kuahamisha kituo cha Polisi toka kilipo maeneo ya ofisi za chama cha wakulima wadogowadogo kuja mjini ili kuzuia uharifu wa aina hii. "Kwa hela hizi za mpunga tulizo nazo tutaisha mwaka huu" anasema mkazi mmoja wa Mtaa wa Mlwasi ambao unamiradi mingi ya maendeleo.
Blog hii kama vyombo vingine vya Habari inatoa pole kwa Familia ya Marehemu Msigalah pamoja na ndugu na jamaa. Hata hivyo natoa wito kwa Wananchi wa mji huu kujitoa kuulinda mji wao kwa kutumia ulinzi shirikishi kama linavyosisitiza jeshi la polisi kwa sababu idadi ya Askari waliopo hawatoshelezi mahitaji ya nchi. Kwa upande wa Serikali inatakiwa kuongeza idadi ya Askari na kuhakikisha Ulinzi na Usalama kwa kila mahali ambapo matukio ya ujamabazi kama haya yanatokea.
Poleni sana watu wa Madibira. Mungu awalinde tena na majanga kama haya.
No comments:
Post a Comment