Leo ulimwengu umeadhimisha miaka 19 baada ya mauaji ya
Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 na kugharimu maisha ya watu
takriban milioni moja. Maadhimisho hayo hufanyika duniani kote kama siku
maalumu ya kuwakumbuka wahanga wa vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya Wahutu na
Watusi iliyopiganiwa ndani ya siku 1oo.
Maadhimisho hayo yalianza kuazimishwa tangu mwaka 2004 baada
ya Umoja wa Mataifa kuiteua April 7 kila mwaka kuwa ni siku ya kumbukumbu ya
mauaji ya Kimbari.
Nchini Tanzania maadhimisho hayo yamefanyika leo jijini Dar
es salaam ambapo baadhi ya Wanadiplomasia mbalimbali walikusanyika katika
Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City kwa ajili ya maadhimisho ambapo waliongozwa
na Balozi wa Rwanda nchini Dk Benjamin Rugangazi huku mgeni rasmi akiwa ni Mwanadiplomasia
mkongwe Dk Salim Ahmed Salim.
Kabla ya maadhimisho hayo yalifanyika matembezi ya kumbukumbu kuanzia katika Viwanja vya New World Cinema- Mwenge
hadi Mlimani City ambapo yalihudhuriwa na Wanafunzi mbalimbali wa Shule za Msingi
na Sekondari za jijini Dar es salaam.
Maadhimisho hayo yalianza kwa kuwasha mishumaa ikiwa ni
ishara ya upendo wa kuwakumbuka waliopoteza maisha katika vita hivyo mbapo
yalifuatiwa na burudani kutoka kwa Wanafunzi wa shule ya Msingi ya Heritage na
baadaye kumaliziwa na hotuba mbalimbali ikiwemo ya Dk salim.
Picha zifuatazo zinaonyesha matukio mbalimbali ya maadhimisho
hayo.