Thursday, October 13, 2011

Nyerere day iwe chachu ya mabadiliko Bongo

         Ijumaa ya tarehe 14 mwezi huu watanzania tunaadhimisha miaka 12 ya kifo cha Hayati baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere. Siku hiyo Watanzania hatutakuwepo makazini kwa kuwa ni siku ya mapumziko kitaifa. Hii ni siku maalumu kukumbuka kifo cha kiongozi huyu mahiri wa taifa la Tanzania. Siku hii tunahitajika kuzitafakari nasaha za hayati baba wa taifa huku tukimuombea astarehe kwa amani huko alikotutangulia.
Hayati Baba wa taifa Mwalimu Julius K. Nyerere  1922 - 1999
           
            Siku hii si ya kulewa baa au kufanya madhambi kama miongoni mwetu tunavyofikiri. Wengi hutumia siku hii ya mapumziko kwa mambo yao ya ajabu ajabu ambayo baba wa taifa aliyakemea sana kwa kuwa hayana tija katika taifa maskini kama hili. Wakati tukiadhimisha kifo hicho kuna baadhi  yetu wamepanga kutumia siku hiyo kujinufaisha wenyewe. Wapo watu ambao watatumia bajeti iliyopangwa kuwezesha maadhimisho hayo kama mitaji yao binafsi. Na wapo wengine watakao tumia siku hii kufanya mambo yao yasiofaa katika jamii ya kitanzania kama wizi, na masuala mengine ya uvunjifu wa amani.
     Umma wa watanzania lazima utafakari ni changamoto gani tunazipata tangu kuondokewa na kiongozi wetu shupavu JK I. Maadhimisho haya ya miaka 12 ya kifo cha baba wa taifa yanaambatana na maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania bara. Je Watanzania tunayaishi aliyotuachia mwalumu? Bila shaka kila mtu anajibu moyoni mwake basi hivyo ndivyo tunavyohitajika kutafakari zaidi ili kutoa mipango bora na endelevu ya kujenga nchi yetu na si ufisadi.
Ni matumaini yangu kuwa watanzania wengi wataitumia siku hii kutafakari kwa kina masuala yote aliyotuachia ba ba wa taifa kama njia moja wapo ya kujenga nchi, Hivyo basi Serikali ihakikishe usimamizi wa kutosha katika maadhimisho hayo. Nyerere day inatuhusu watanzania wote na inabidi tushirikiane kuendeleza kumbukumbu hizi ili zidumu vizazi na viziazi.
      Nawatakia mema katika maadhimisho haya ya kifo cha baba wa taifa!

       

Saturday, October 1, 2011

Uchaguzi mdogo Igunga: Ni patashika nguo kuchanika

Rostam Aziz mbunge wa zamani Igunga
      Ikiwa imesalia siku moja tu kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa mbunge katika jimbo la Igunga hali ya kisiasa bado haijakaa sawa. Mvutano wa kisiasa ni mkali sana na wenye changamoto nyingi kwa Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) pamoja na vyama husika vinavyoshiriki uchaguzi huo.
     Vyama mbalimbali vimejitokeza kushindania kiti hicho kilichoachwa na mbunge wa zamani wa jimbo hilo Bwana Rostam Aziz baada ya kujiudhuru nyazifa zote za kichama ndani ya CCM na kuwa mwanachama wa kawaida. Chama tawala CCM  kinatetea jimbo lake kwa kumsimamisha mgombea wake Dk. Dalali Kafumu huku CHADEMA nao wakimsimamisha mgombea wao bwana Joseph kashindye. Kwa upande wa CUF wamemsimamisha Bwana Leopold Mahona.
Mwananchi akijiandaa kupiga kura.
     Tangu kampeni za uchaguzi huo kufunguliwa mapema mwezi Septemba mwaka huu watanzania tumeshuhudia mengi kutoka Igunga.  Mengi kati ya hayo ni ya kusikitisha na hayafai kuwepo katika jamii ya leo. Wananchi wa Igunga wamejikuta wakipata mshikemshike wa kutosha kutoka kwa vyama vinavyowania Jimbo hilo. Moja ya matukio yaliogusa hisia za wengi ni kuchomwa  moto nyumba ya Bwana Hamis Makala  katibu wa CCM kata ya Nyandekwa. Tukio jingine la fedheha nikukamatwa kwa Mkuu wa wilaya ya Igunga Bi. Fatma Kimario na vijana wa CHADEMA katika Mkutano wa siri aliokuwa akifanya na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM. 
      Si hayo tu, pia tumeshuhudia mengi kutoka Igunga ikiwemo tuhuma ya kada wa CCM kushikwa na majina  ya wapiga kura pamoja na shahada zao na mengine ni tuhuma za CCM kuandaa maninja 500  kwa ajili ya uchaguzi huku nao CHADEMA wakituhumiwa kuandaa Makomandoo 33 kudhibiti uchaguzi jimboni hapo. Vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo vimejikuta vikiingia katika malumbano yasio na tija kwa Wananchi wa Igunga. Kilichokuwa kikiendelea Igunga ni malumbano na si kutoa sera kwa watu wa Igunga.
     Licha ya matukio yote hayo bado umma wa watanzania unahitaji uchaguzi huru na wa haki Igunga. Wananchi wa Igunga hawatakiwi kurubuniwa katika kufanya maamuzi yao sahihi wakati wakichagua viongozi wao. Ikumbukwe kuwa safari ya mbwembwe zote za kampeni hizo inaishia leo hii na kesho tunahitaji utulivu, amani na upendo miongoni mwa watu wa Igunga. Naamini kuwa itikadi za kivyama zipo miongoni mwao lakini haziwezi zikawafanya wapigane au wavunje amani yao kwa sababu ya maslahi ya watu wachache.
Bwana Rajabu Kiravu, Mkurugenzi Mtendaji NEC
     Tume ya taifa ya uchaguzi na jeshi la polisi wanahitaji umakini na nguvu za ziada Igunga. Uchaguzi huu si lelemama kama wengi wetu tunavyodhani. Kama matukio makubwa kama hayo yameweza kutokea wakati wakampeni watashindwaje siku moja ya uchaguzi? Watanzania tumejifunza mengi sana Igunga na tunaendelea kujifunza zaidi. Mengi tuliyoshuhudia ni mifano ya ambayo hutokea wakati wa chaguzi nyingine ila huwa hatuyaoni na hatuyasikii sana kutokana na watu wote kuwa bize na uchaguzi na eneo kuwa kubwa tofauti na ilivyo Igunga.
     Japo uchaguzi huu mdogo wa Igunga unaandamana na chaguzi nyingine ndogondogo za Madiwani bado tume ya Uchaguzi ina changamoto nzito toka Igunga. Umma utambue kuwa karibia viongozi wote wa vyama vikubwa nchini wameweka kambi Igunga. Kila chama kikiwa na matumaini ya kushinda kiti hicho. 
     Naamini kuwa tume makini haiwezi kuacha uvunjaji wa sheria uendelee Igunga. Tume chini ya mwenyekiti wa muda Profesa Chaligha na Mkurugenzi mtendaji Bwana Rajabu Kiravu hawana chaguo zaidi ya kuhakikisha  kuwa uchaguzi ni wa haki, huru na wa amani. Tume haina budi kijivua gamba katika uchaguzi huu mdogo ili kutoa kashfa za uchaguzi mkuu uliopita. Binafsi ninayo imani kubwa na utendaji wa profesa Chaligha. Utaalamu wake katika masuala haya ya uchaguzi unaweza ukawa ni chachu ya kuleta mabadiliko katika uchaguzi huu. Umakini alionao mwenyekiti huyu si kidogo, ni umakini unamfanya kila aliyechini yake azifuate nyayo zake. 
Profesa Amon Chaligha Mwenyekiti wa muda NEC
      Iwapo Profesa Chaligha hataangushwa na Vijana wake basi uchaguzi utaenda sawa Igunga.  Namfahamu sana  Profesa tangu alipoanza kunifundisha masuala ya Sayansi ya Siasa  na Utawala pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Huwa hataki mchezo kabisa. Pia anao uwezo mkubwa wa kurekebisha mapungufu mengi yaliokuwepo tume ya uchaguzi. Lakini iwapo itakua kinyume na hayo basi hali ya Igunga hapo kesho ni patashika na nguo kuchanika.


      Mwisho, napenda kuwasihi wana Igunga kuwa kesho si siku ya kufanya makosa, ni siku ya  kutoa maamuzi magumu kwa kumchagua mtu anaewafaa kuwaletea maendeleo jimboni mwao na si ushabiki  wa vyama. Siasa ya kisasa na iliyokomaa haiendani na woga kwa vyama vya kisiasa kuwazia kushindwa au kukosa. Vyama shiriki katika uchaguzi huo havina budi kuwa makini katika masuala yote ya kiuchaguzi ili kuzuia tafrani hapo kesho. Nawatakieni uchaguzi mwema.
    Mungu Ibariki Tanzania, Mungu tubariki watoto wa Tanzania!

Monday, September 12, 2011

Salha Israel: Vodacom miss Tanzania 2011


    Hatimaye aliyekuwa Miss Redds Ilala, Salha Israel ameibuka mshindi wa Vodacom miss Tanzania 2011. Fainali za mashindano haya zilifanyika usiku wa Jumamosi wa tarehe 10 mwezi huu ndani ya ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na wapenzi wa tasnia ya urembo kibao. Salha aiibuka mshindi kati ya warimbwende 30 waliokuwa wakigombania taji hilo.
Mshindi wa Miss Vodacom Tanzania 2011 Salha Israel katikati akiwa na Mshindi wa pili Tracy Sospeter (kulia) na mshindi wa tatu Alexia william (Kushoto)
    Shindano la Umiss Tanzania mwaka limeonekana kuboreshwa zaidi kuliko miaka ya nyuma. Wadhamini wakuu wa shindano hili mwaka huu (Vodacom) wamejitahidi kufuta lawama nyingi zilizokuwa zikitoka mara kwa mara baada ya mashindano ya Miss Tanzania kuisha takribani miaka yote ya nyuma. Tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu watu hawalaumu sana badala yake wanaonekana kusifia mfumo mzima uliotumika kuyaandaa mashindano haya.
Diamond Platnumz na Vijana wake wakilisakata jukwaa la Miss Tz usiku wa Jumamosi, Mlimani City.
      Kuanzishwa kwa Vodacom House na kupigia kura warembo wakiwa ndani ya jumba hilo kuliongeza msisimuko mkubwa na uhalali wa mashindano haya. Warembo Thelathini kutoka Mikoa mbalimbali na Vituo walishiriki mashindano haya. Katika fainali hizo mshindi wa pili ni Tracy Sospeter na mshindi wa tatu ni Alexia William. Huu ni mwanzo wa safari kwa mrembo Salha Israel kuelekea mashindano ya Miss world mwaka huu. Mshindi wa Kwanza Salha Israel alizawadiwa gari aina ya Jeep na zawadi nyingine nyingi kutoka kwa Wadhamini.
Washiriki wa Vodacom Miss Tanzania 2011 wakiwa katika picha pamoja.
     Licha kuwa na mvuto na maboresho mengi baadhi wadau wa tasnia ya Urembo wamelalamikia ukosekanaji wa tiketi za kuhudhuria shindano hilo. Tiketi mwaka zilionekana kuwa chache sana kwa Wananchi wa kawaida kuliko Miaka ya nyuma. Baadhi ya Wananchi wamelalamikia kiwango cha kuingilia kuwa kikubwa mno tofauti na siku za nyuma.
    Wasanii mbalimbali kama Diamond, Akil the Brain akiwa na SaRaha na Big Jahman, Juliana kutoka Uganda pamoja na Bob Junior (Rais wa Masharobaro) walitoa burudani ya nguvu katika shindano  hilo na kuufanya usiku wa Miss Tz kuwa mfupi.
    Kwa ambao hawakubahatika kuhudhuria shindano hili pale Mlimani City waliweza kutizama live kupitia Kituo cha televisheni cha Star Tv ambao pia walikua moja ya Wadhamini wa shindano hili chini ya Sahara Communication.
 Salha Israel akionyesha funguo za Jeep baada ya kushinda Umiss Tz 2011.
   Baada ya ushindi wa Salha kuwa Miss Tanzania 2011, Watanzania bado tunahitajika kumjenga, kumshauri na kumuandaa vema mrembo huyu ili aweze kutuwakilisha Vyema katika Mashindano ya Miss World. Kila la Kheri Salha na bado Watanzania tunakuombea uweze kufika mbali zaidi katika tasnia hii ya Urembo.  Hongera, na Mungu Akubariki!

Friday, September 2, 2011

Kujivua gamba si kujivua uhai; Wanaotuhumiwa CCM wakubali kujivua.....

        Ule Usemi wa Kujivua gamba unaotumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) una dalili zote za kukiregeza chama hicho. Msemo huu uliteka masikio na akili za Watanzania wengi hasa pale ulipokuwa ukitolewa na Vyombo mbalimbali vya habari na kusindikizwa na kampeni za nchi nzima kutoka kwa Viongozi wapya wa Chama hiki kikongwe hapa nchini wakiongozwa na Katibu Mkuu Mh. Wilson Mukama akifuatiwa na Katibu Mwenezi Itikadi na Sera, Bwana Nape Nnauye. Ukijaribu kufanya tathmini ya harakaharaka kuhusu propaganda hii utagundua kuwa imetumika kutishia  Wanachama wenye kashfa za Ufisadi ndani ya Chama hicho bila ya kuwa na nyenzo mahsusi za kuwang'oa watuhumiwa hao. Msemo huu wa kujivua gamba hautofautiani sana na Mbwa mwenye kelele asiye na meno. Kiuhalisia Mbwa wa aina hii hawezi kumng'ata mtu kamwe labda kwa miujiza ya Freemasonry.
     Lakini katika safari hiyo ya kujivua gamba Watanzania tumeshuhudia Mwanasiasa Mashuhuri wa CCM ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo Igunga Bwana Rostam Aziz akiwa wa Mwanasiasa wa kwanza wa Chama hicho miongoni ya Wanaotuhumiwa aking'uka madarakani kwa kuachia ngazi zote za Uongozi kichama na kubaki kuwa Mwanachama wa kawaida. Tukio hilo lilipa sura mpya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Kuamsha hisia tofauti miongoni mwa Wanachama wa Chama hiki pamoja na Wananchi wa kawaida. Hata hivyo Bwana Rostam aliutamkia Umma wa Watanzania kuwa kung'atuka madarakani hakuhusiani na kampeni zinazoendeshwa na Chama Tawala za "Kujivua gamba".
Nape Nnauye moja ya Viongozi wa Kampeni za "Vua gamba"

Aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
     Wakati hilo likitokea bado Watuhumiwa kibao wa Ufisadi wa Chama hicho wanaendelea na Shughuli mbalimbali za Kichama na nyazifa nyingine za Kiserikali kama Kawaida. Kuendelea kufanya kazi kwa Wanachama hawa hakumaanishi kuwa CCM na Kampeni zake imewasamehe na kuwasahau kabisa; bali imefunga breki na kuanza kufikiri mchongo mpya wa kuwang'oa. Sifikirii kuwa Viongozi hao wapya na wenye shauku kubwa ya kukisafisha Chama wameridhia na mafanikio walioyapata ambayo yapo kinyume kabisa na dhamira yao ya Kujivua gamba. Kijana machachari katika Siasa ya Nchi hii Bwana Nape Nnauye na Mzee Mukama wamepata funzo kubwa la kutokukurupuka kuanzisha mkakati bila ya kuwa na Vitendea kazi. Yalionekana katika kampeni hizi ndiyo hayahaya yanayoonekana katika Sera nyingi za Serikali ambazo huwa nzuri na za kuvutia lakini hukosa njia za kuziwesha kufikia  lengo. 
      Ikumbukwe kuwa kuvuma kwa Kampeni za Kujivua gamba hakumaanishi kuwa CCM ndiyo imetakata bali hali itazidi kuwa mbaya zaidi kwa sababu hata kampeni hii isiyohitaji ushindani wa nafasi mbalimbali za Uongozi wa Nchi wameshindwa kutekeleza, Je sera na Mipango mbalimbali ya Maendeleo pamoja na Kuwapa Madaraka tena mwaka 2015 wataweza kutekeleza? Watanzania tukumbuke siku 90 zilizotolewa na Kamati Tendaji ya CCM Mapema Mwaka huu zilifikia lengo?
        Licha ya kuwa Meno ya CCM yameshindwa kuwauma baadhi ya Watuhumiwa wa Chama hicho bado Watuhumiwa hao wanawakati mwingine wa kutafakari kuhusu Mustakabali mzima wa Chama. Ni bora wajiengue mapema wenyewe bila hata ya mawazo ya kuwa wanatimiza matakwa ya dhana ya Kujivua gamba. Wanasiasa wa CCM hawana budi kuzisoma alama za nyakati. Kukaa kwa CCM madarakani muda mrefu hakumaanishi kuwa itatawala maisha. Wakumbuke kuwa Chama huongoza nchi kwa muda na pia hupoteza. CCM ikumbuke kuangushwa kwa Chama cha Institutional Revolutionary Party (PRI) Chama Tawala cha Mexico Mwaka 1997 ambapo kilikuwepo madarakani tangu Mwaka 1929 au Chama cha Congress cha India kilichoangushwa madarakani Mwaka 1977 kikitawala tangu Mwaka 1952. Hii ni Mifano tu CCM wanahitaji kuifahamu. Dominant Party System inaweza kupotea haraka sana na Watu wakaisahau. Hivi ndivyo CCM itakavyopotea na kusahaulika Miongoni mwa Watanzania iwapo wataendelea kutoa Sera na Michakato hewa na isiyo na tija kwa Watanzania.
       Watuhumiwa wa Ufisadi kutoka CCM pamoja na Viongozi wa kampeni  za Kujivua gamba hawana budi kujivua gamba kwa pamoja kwa sababu wanazidi kukipoteza na kukigharimu Chama. Baadala ya CCM kuwa na ngozi mpya na nyororo kama ilivyotarajiwa baada ya hizi kampeni itakuja kuwa na  Ngozi ngumu na yenye nundunundu hapo baadaye iwapo jitahada za ziada zisipo chukuliwa.
    Ili kulinda Heshima ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Heshima zao binafsi wale wote wanaosakamwa na Kampeni za "Vua gamba" hawana budi kujipumzisha kama Rostam Aziz. Heshima atakayoipata Rostam hapo baadaye itakuwa tofauti na hawa wanaong'ang'ania kukaa madarakani. Uchu wa madaraka utawaponza. Tunafahamu wengi wao ni Office seekers ndani ya Chama na si Message seekers kama inavyotakiwa kuwa ndo maana wapo radhi kudhaaririka. Lakini ubishi wa Vigogo hao ni furaha kwa Vyama vya Upinzani kutengeneza B52 za kuing'oa CCM.
      Ndugu zangu wapendwa, Kujivua gamba si Kujivua Uhai; Wanaotuhumiwa na Kampeni za Vua gamba wakubali kujivua kwani hawatapoteza Maisha bali wataongeza heshima ya Kisiasa na Masuala mengine ya Kimaisha kama Biashara na Mengineyo. Hata Hivyo nguzo zinazoishikiria CCM zimeanza kubomoka kazi kwenu Wapinzani kuukusanya Udongo na Kuufanyia Modifikesheni ili kuishika nchi mapema iwezekanavyo.





Friday, August 26, 2011

Kwa hili... Vyuo Vikuu vitageuka Darfur!

       Hatimaye Tume iliundwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete mnamo  tarehe 14/02/2011 imetoa mapendekezo yake ya namna ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharimiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya Elimu ya Juu. Mapendekezo hayo yalitolewa rasmi na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Dk. Shukuru J. Kawambwa tarehe 19 Agosti mwaka huu kama taarifa kwa umma. Taarifa hiyo ilitangazwa na vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini yakiwemo magezeti ya kila siku. Kwa undani zaidi rejea Gazeti la Mwananchi la Jumanne Agosti 23 2011 Ukurasa wa 15 Sehemu ya Matangazo.
       Kwa wadau wote nchini wanafuatilia na waliomo katika mfumo wa Elimu ya Juu najua wanatambua adha wanayoipata Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuhusiana na Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Toka Bodi ianzishwe matatizo yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku. Bodi Imesababisha Migomo mingi ya Vyuo Vikuu huku ikisababisha baadhi ya Wanafunzi wa Vyuo hivyo kupoteza masomo kabisa. 
     Bodi imekuwa kero kwa Wanafunzi, Utawala wa Vyuo Vikuu pamoja na Jeshi la Polisi nchini. Tukianza na Wanafunzi Bodi hii ya Vyuo Vikuu imesababisha Wanafunzi wengi kusoma kwa shida sana aidha kwa kucheleweshewa Mikopo yao au kucheleweshewa Means Test zao. Kwa upande wa Utawala wa Vyuo Vikuu wamekuwa wakipata kashikashi nyingi za kufunga Vyuo mara kwa mara, kuharibiwa mali na bajeti nyingine za kiutawala. Na kwa upande wa ndugu zetu Jeshi la Polisi wamekuwa wakipambana na Wanafunzi kila Mgomo unapotokea. Kwa maana hiyo Bodi inaongeza gharama za utendaji badala ya kuzipunguza kama ilivyotarajiwa.
    Matarajio ya Watanzania wengi kutoka kwenye Tume maalumu ilioundwa na Mheshimiwa Rais ni Maboreshao zaidi na si kuharibu zaidi kama inavyotabiriwa na taarifa iliyotolewa na Wizara kama ilivyotolewa na Mheshimiwa Kawambwa. Katika taarifa hiyo kwa Ummakuna vipengele sita vinavyoeleza mapendekezo hayo. Kwenye vipengele hivyo mi napenda nivielezee vipengele namba 2, 3, 4 na 5. 
    Kipengele namba 2(i) kinaelezea Utoaji wa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Katika kipengele hiki taarifa hii inawataarifu Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kuwa Mikopo itatolewa kwa Wanafunzi waliodahiliwa na Vyuo Vikuu moja kwa moja Shuleni tu yaani Direct entrants na wale wenye sifa kupitia mfumo wa mafunzo ya Elimu ya Ufundi (TVET) na si kwa wale ambao wanatumia sifa linganishi (Equivalent qualifications  & Mature Age entrants). Kipengele hiki kinaondoa haki za Watanzania waliounganisha elimu na wanahitaji kusoma Elimu ya Juu kwa udhamini wa Bodi ya Mikopo.
      Hata hivyo kipenegele 2(ii) kinamaboresho kidogo hasa ni ile sehemu ya kugharamia Mafunzo kwa vitendo kwa fani zote zitakazobainishwa na Tume ya Vyuo Vikuu kwa Asilimia Mia Moja. Ingawa mabadilisho haya yameandikwa ila inawezekana yakabaki kwenye makaratasi tu. Kwa hilo tunasubiri utekelezaji. Na sehemu nyingine za asilimia Mia Moja zinabaki kama kawaida hasa kwenye maeneo ya Chakula na Malazi, Vitabu na Viandikwa (Stationary) na Utafiti (Research). 
     Fani za kipaumbele zimebaki zilezile za awali yaani Ualimu, Sayansi za Tiba, Uhandisi, Sayansi za Kilimo,  na Sayansi za Mifugo. Hata hivyo Walimu wa Masomo ya Sanaa wamepitiwa na Tsunami kwani hawatapata Asilimia Mia Moja kama wale wa Sayansi na na hawatapata chini ya Asilimia 50%. Hali mbaya  zaidi kwa wale wa fani zisizo za Ualimu, Sayansi na Uandisi. Kwa wale wote ambao ni Mature Age entrants  na wenye sifa linganishi mikopo watapata kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii au kwa Waajili wao. Je kwa hili ni haki?
      Mbaya zaidi ni hii ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu kupewa gharama za ada sawa na zile za Serikali wakati muundo wa ada upo tofauti kati ya Vyuo Binafsi na Vya Umma. Kama hali hii je wanafunzi waliopo Vyuo Banafsi watasaivu? Kwa mabadiliko haya lazima tukubaliane kuwa Migomo ya Vyuo Vikuu hasa vile vya Binafsi itawekwa kwenye ratiba maalumu kwa ajili ya kushindwa kulipa kiasi hicho cha ziada. Mifano tunayo mingi sana ya hivi karibuni. Moja ya mifano hiyo ni kufungwa kwa Chuo cha IMTU, na maandamano ya Wanafunzi wa Udaktari wa Chuo cha Kumbukumbu ya Hurbert Kairuki kwenda tume ya Vyuo Vikuu (TCU). 
      Haya si maboresho tena bali ni maangamizi kwa sababu Wanafunzi wengi hawatasoma Vyuo Vikuu kulingana na uwezo kifedha hasa hiyo ya kujazia viwango vya ada vilivyozidi kutoka kwenye vile vya Serikali. Ikumbukwe kuwa Vyuo Binafsi ndio vinachukua idadi kubwa ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Kama hali itakuwa kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mheshimiwa Rais basi ndugu zetu wote wasio na uwezo na waliokosa nafasi za Vyuo Vya Umma hawatasoma kabisa. Hili ni angamizo kabisa hata wale wanaosoma Sayansi kama kipaumbele kinavyoeleza hawatafankisha kwa sababu ada za Vyuo binafsi fani za Sayansi ni tofauti na Vyuo vya Umma. Hapa Tume au wizara iliangalie upya suala hili kwani gharama itakayotumika kuzima migogoro itakayojitokeza inaweza kuwa kubwa kuliko hata wangeghalamia masomo ya Wanafunzi hawa wa Vyuo binafsi.
     Kipengele namba 3 kinaelezea Urejeshaji wa Mikopo. Katika kipengele hiki Tume imeweka kiwango cha urudishwaji wa mikopo kuwa ni Asimia 8 ya Mshahara wa kila Mfanyakazi aliyesomeshwa na Bodi ya Mikopo na Sheria zitatungwa kuwabana Wafanyakazi hao ili kurejesha Mikopo.
       Kipengele ambacho kitaleta sana balaa ni hiki cha namba 4. Kipengele hiki kinazungumzia Masuala ya kiutawala hasa kuhusiana na Mikopo kwa Ujumla. Hapa Vyuo Vikuu vyote nchini vimeombwa vianzishe Dawati Maalumu la Masuala ya Mikopo na Dawati hili litakuwa chini ya Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma. Na kuanzia Mwaka wa Masomo unaokuja yaani 2011/12 Wanafunzi wote watachukulia fedha zao Vyuoni na si Bodi kama awali. Kwa maana hiyo basi Malalamiko yote yanayohusiana na kukosa au kucheleweshewa fedha yatatuliwa ndani ya Chuo husika Hapa Bodi imeamua kujivua gamba. Hata hivyo gamba lenyewe imechelewa kujivua kwa sababu bado Vyuo Vikuu vitakupambana na balaa kali zaidi ya ile kutoka kwa Bodi. 
      Balaa hili linakuja kwa sababu Vyuo vingi havitakuwa na uwezo thabiti wa kukabilana na kashikashi za Wanafunzi, pili kufeli kwa Mawasialiano na Mahusiano bora katika ya Chuo na Bodi kunaweza kuleta balaa kali kwa Vyuo Vikuu husika. Mfano Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) wamekuwa wakimpa shughuli nzito sana Afisa wa Mikopo wa Chuo hicho Maarufu kama Bush. Ofisi huwa haitulii kwa Wanafunzi wachache sana ambao si zaidi ya Mia tatu. Kama hali ni hiyo kwa Mia Tatu, je Wanafunzi karibia 15000 itakuwaje? Na kama inavyofahamika Wanafunzi wa Chuo hiki huwa wana hitaji haki kila sehemu inayowahusu kama ilivyokuwa Mwezi Februari Mwaka huu ambapo mgomo wao ulisababisha kuundwa kwa Tume hii ilyoleta mapendekezo haya pamoja na kuongezeka kwa fedha za kujikimu (Boom) toka Shilingi 5000-7500.
       Kwa pendekezo hili la kuchukulia hela Vyuoni Serikali ijiandae na Maandamano yasiyoisha kutoka kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vyote nchini. Kwa sababu Vyuo Vingi vina Wanafunzi wengi kuliko uwezo unaohitajika. Utawala wa Vyuo Vikuu vyote nchini ujiandae kwa lolote litakalowakuta iwapo watashindwa kutimiza mipango hiyo.
       Kipengele cha mwisho kujadili ni cha 5 ambacho kinazungumzia Ruzuku kwa Wanafunzi wa sayansi za Tiba. Hapa Wanafunzi wote wenye Division Three wasitegemee kabisa Ruzuku hii isipokuwa kwa wale wenye Three za Penati yaani waliofeli somo la General Studies katika mitihani ya Kidato cha Sita. Ruzuku hii pia inaanzia Mwaka wa Masomo ujao wa 2011/12.
      Kutokana na Mapendekezo hayo ya Tume na Wizara kwa Ujumla bado Bodi ya Mikopo haijaboreshwa na Wanafunzi hawatatuliwa kero zao nyingi. Kilichofanyika ni kutoa nafuu na kuweka angalu. sababu wanafunzi wengi watakosa kusoma na wale wote wanaotumia Mature Age entry na equivalent hawatajiendeleza Masomo yao iwapo Mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii au Taasisi hizo zitakataa kuwasomesha
    Hivyo basi Mapendekezo haya yamekuja kuwagawa Wanafunzi wengi na kuongeza Matatizo. Naiomba Bodi ya Mikopo, Tume pamoja na Wizara warudi tena kazini kurekebisha mapungufu haya ili waje na Maboresho na si haya Mabomosho.


Wednesday, August 24, 2011

Langa: Madawa ya kulevya sasa basi!

       Msanii wa mziki wa Hiphop nchini Langa ameuthibitishia umma kuwa hatatumia tena Madawa ya kulevya kama zamani. Langa alibainisha hayo katika mahojiano na kipindi cha kupambana na madawa ya kulevya kilichorushwa hewani na Redio One chini ya Mtangazaji Abdallah Mwaipaya maarufu kama ABD majira ya Saa kumi na moja jioni siku ya Jumatano ya tarehe 24 mwezi huu.
       Langa alishiriki kipindi hicho pamoja na Bwana Jamal Mtisi wa Tume ya kupambana na kudhibiti Madawa ya kulevya na Mama Fatma Supa Tume ya kupambana na Madawa ya kulevy a Zanzibar. Katika maelezo yake Langa alikiri uwepo wa wasanii wanaotumia madawa ya kulevya kama ilivyokuwa kwake.
    Anasema baada ya kutumia kwa muda sasa madawa hayo kaona hayana faida kabisa na yanasababisha masuala mengine ya kibiashara na kimaisha kuzorota. Langa anafichua kuwa moja ya vitu vilivyochangia kazi zake za mziki kutokuwa sawa ni Madawa ya kulevya.
      Ili vijana wafanikiwe kimaisha hawana budi kuachana kabisa na madawa hayo hatari ambayo huleta uteja pamoja na kurukwa na akili. Langa alisema yupo radhi kuisaidia serikali katika jitahada za kupambana na Madawa ya kulevya kwa kutoa elimu kwa vijana wenzike na umma kwa ujumla. Ili kufanikisha anatoa elimu ya kutosha kuhusu madawa ya kulevya Langa aliwaomba wadau mbalimbali wa mambo haya pamoja na Serikali  kumfadhiri aweze kuanzisha NGO ya kupiga vita madawa ya kulevya.
     Ili kuonyesha kuwa  kashaachana na madawa ya kulevya na yupo kwenye mchakato wa kutoa elimu kwa jamii Langa katunga singo maalumu ya kuelimisha ambayo aliimba kwa akapera studioni hapo. Aliendelea kubainisha kuwa atarudi kwenye game kama zamani alipokuwa na kundi la mziki la Wakilisha lilokuwa likiundwa na yeye (Langa) , Witness na Shaa. Kwa mashabiki mnaombwa kukaa mkao wa kula kusikia vitu vipya vya msanii huyu ambaye kwa sasa anatamba kwa singo yake Pesapesa mkubwa wa kushawishi jamii nzima.
     Big up sana mzee Langa tunakutakia maisha mapya ya kimziki na masuala mengine ya maendeleo. endeleza juhudi hizo mpaka tupate uhuru mwingine kutoka kwenye madawa ya kulevya.

Tuesday, August 23, 2011

Video ya Tajiri wa mahaba ya Cassim Mganga ni nomaaa!

     Tasnia ya mziki wa kizazi kipya inazidi kupanda chati kila uchwao. Wasanii wapya wanaongezeka huku wale wazamani nao wakiokoa status zao kuzuia kupotea katika game. Katika safari hiyo ya mabadiliko katika game wasanii wengi wakongwe wamepotea na kuacha idadi ndogo sana tofauti na ile ya wanaongezeka kila siku. Licha ya maendeleo hayo ya game la Bongo fleva kuna wasanii ambao wamekuwa wakifanya kazi zao vizuri na kufanya zipate sifa mbalimbali katika ulimwengu wa mziki huu wa kizazi kipya mmoja ya wasanii hao ni Cassim Mganga wa kundi la mziki la TIPTOP lenye maskani yake pale Manzese Jijini Dar es salaam.
Moja ya kipande cha video ya tajiri wa Mahaba

Sehemu nyingine ya video hiyo ikimuonyesha Cassim na mrembo wake kwenye video ya tajiri wa mahaba
    Tofauti na wasanii wanaotamba katika chati kwa sasa Cassim yeye anao wimbo wa tajiri wa Mahaba wenye asili ya Kitanzania. Wadau mbalimbali wa mziki huu wametokea kuukubali sana wimbo huu. "Ukiusikiliza kwa makini sana wimbo huu utagundua upo tofauti kidogo na hizi nyingine zinatamba kwenye Top ten mbalimbali za redio zetu, tofauti inakuja kwenye beat na style aliotumia mkali huyu wa nyimbo za malavidavi" anasema Feruuz mkazi wa Tabata Segerea. Nae Esther wa mitaa hiyohiyo ya Segerea alitoa mtazamo wake kuhusu wimbo huu akasema "Unajua bro tuache unafiki na wivu wa kijinga, wimbo wa tajiri wa mahaba wa Cassim ndo unaenikuna sana ila utamu unazidi sana nikiiona video yake kwenye TV steshen mbalimbali kila siku" alibainisha.
      Hata hivyo safari ya kujua ni video ipi msimu huu wa kusherekea miaka hamsini ya Uhuru inasadifu Utanzania wetu ilizidi kusonga mbele na kuuliza wadau mbalimbali wa mziki huu wakiwemo wauza CD, kanda na wasikilizaji. Lakini majibu yote yalisifia video ya wimbo huo wenye mahadhi ya kipwani.
    "Kweli Cassim ni nomaa hata video yake ipo You Tube inaquality zote. Nakupa big up sana kijana kaza buti na endelea kutoa vitu adimu kama hivyo kila siku ili kukuza game. keep it up!" anasifia muuza kanda mmoja wa Kariakoo.
    Sasa ni kazi yako Mtanzania kununua kazi za Cassim na si kudownload kama tulivyozoea, tujitahidi kusupport wasanii wetu ili watoe kazi nzuri zaidi kama hii. Tafadhari usiombe zikupite kazi hizi adimu. 
         Just Watch out today its more than good!

Madibira kumechafuka!!

Na: Nuzulack J. Dausen
     Hali si shwari katika mji mdogo wa Madibira wilayani Mbarali. Matukio mengi ya wizi na ujambazi ndio yanashika kasi katika mji huu. Amani na upendo wa awali vimetoweka, sasa ni unyamaunyama na pesa ndio sabuni ya roho. Zimepita wiki mbili tu toka tukio liloibua hisia za wengi kupitia vyombo vya habari kutokea katika mji huu. Tukio hili ni lile lilohusisha mganga na mteja wake walioshiriki kuua raia mwenzao kama njia ya kujipatia dawa. 
    Kabla ya tukio hilo miezi kumi iliyopita palitokea tena tukio kubwa la ujambazi ambapo watu wasiofahamika waliteka mtaa wa maduka katika kijiji cha Mkunywa na kuvamia duka la Mfanyabiashara mmoja anayejulikana kwa jina la bwana Charles Mohele na kutokomea na kitita cha mamilioni ya fedha. Hata hivyo jumuiya ya Wafanyabiashara wa mji huu walikaa kikao kwa kushirikiana na Serikali na kuanzisha Ulinzi shirikishi. Ulinzi ambao tuliamini ungekuwa mzizi wa masuala ya wizi na ujambazi lakini haikuwa hivyo kama ilivyotegemewa.
    Hali ilitulia kwa muda katka mji huu huku wizi mdogomdogo ukiendelea kutokea majumbani mwa raia kila uchwao. Jeshi la polisi na Serikali ya za mitaa vipo katika mji huu lakini hali si shwari. Wananchi wengi wa mji huu wanadai kuwa Kituo cha Polisi kipo mbali sana na mitaani wanapokaa raia wengi ambapo matukio mengi ya wizi yanatokea. Akiongea na blog hii mmoja ya wakazi wa mji ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema " Tatizo kubwa la hawa polisi wetu tunashinda nao humu baa muda mwingi kwa hiyo hata matukio yakijambazi yakitokea tunakuwa nao pamoja kujiokoa na si wao kutuokoa pia hata waliopo kituoni huwa wachache sana sababu inayoleta ugumu hata kuwaomba msaada wakati wa shida kama hiyo"
     Kwa takribani miaka kumi hivi mji huu umekuwa maarufu sana kwa kuzalisha zao la mpunga na idadi ya watu mbalimbali imekuwa ikiongezeka siku hadi siku. Katika ongezeko hilo la watu, matukio ya hatari nayo  yameongezeka.
   Tukio la kusikitisha zaidi ni hili lilotokea usiku wa kuamkia tarehe 22 mwezi huu katika mtaa wa kichangani katika kijiji hicho cha Mkunywa. Tukio hilo linahusisha mauaji ya moja ya wafanyabiashara maarufu katika kijiji hicho aliyeuwa kinyama na majambazi usiku huo. Marehemu huyo aliyefahamika sana kwa jina la Msigalah alikutwa na mauti nyumbani alipopanga katika mtaa huo kwa Mzee  Euzebio Mhimba. Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Makambako mtoto wa mwenye nyumba hiyo Bwana Emmanuel Mhimba anasimulia kuwa "Ilikuwa usiku wa saa saba au saa nane ambapo walivamiwa na majambazi na kufungiwa vyumba vyao kwa nje. Azma kubwa ya majambazi hayo ni kutaka kuchukua fedha kwa bwana Msigalah hata hivyo hakuwanazo kwa wakati ule hatimaye walimuua kwa kumjeruhi vibaya na siraha. Hata hivyo mke wa marehemu hawakumuua ila alipata majeraha kiasi".
     Kutokana na tukio hilo la kusikitisha na lilorudisha nyuma maendeleo ya mji huu kwa sababu marehemu alisaidia sana kusambaza umeme kijijini hapo na kwa sasa huduma hiyo haipo tena. Huzuni imetawala mji huu, Uchumi unatarajiwa kushuka sana sababu ya kutopatikana kwa nishati hiyo muhimu katika maendeleo.
    Wadau mbalimbali wametoa maoni kwa Serikali ya Mkoa kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali kuahamisha kituo cha Polisi toka kilipo maeneo ya ofisi za chama cha wakulima wadogowadogo kuja mjini ili kuzuia uharifu wa aina hii. "Kwa hela hizi za mpunga tulizo nazo tutaisha mwaka huu" anasema mkazi mmoja wa Mtaa wa Mlwasi ambao unamiradi mingi ya maendeleo.
      Blog hii kama vyombo vingine vya Habari inatoa pole kwa Familia ya Marehemu Msigalah pamoja na ndugu na jamaa. Hata hivyo natoa wito kwa Wananchi wa mji huu kujitoa kuulinda mji wao kwa kutumia ulinzi shirikishi kama linavyosisitiza jeshi la polisi kwa sababu idadi ya Askari waliopo hawatoshelezi mahitaji ya nchi. Kwa upande wa Serikali inatakiwa kuongeza idadi ya Askari na kuhakikisha Ulinzi na Usalama kwa kila mahali ambapo matukio ya ujamabazi kama haya yanatokea.
    Poleni sana watu wa Madibira. Mungu awalinde tena na majanga kama haya.

Friday, August 19, 2011

The best start up to Simba.

It was Wednesday  at 20:00 when the match of Simba Vs Yanga started at the National stadium. The ground was crowded by fans with yellow, green, red and white clothes which reflected their interests to these competing clubs in Tanzania. Five minutes before the match kick off the MC of that event announced the names of players of each team. Noises from each corner of the ground came when names of new registered players announced. One of the most name people made noises with great happiness was of that newly Simba registered player Felix Sunzu. I sat behind a man approximately aged 70's he said to be Simba fan, when the names of whole team announced he was very happy and seems to be so confident.

The match began at 20:02 exactly. Within first 16 minutes of the match Simba scored the first goal through Boban and later on within the same first half aquired another goal through Felix Sunzu by penalty. The match continued till first half was over. The second half began by strong force from Yanga, Fabregas as named by Yanga fans was the mostly pronounced name to both competing fans of Simba and Yanga. Fabregas played well with combination his players but were unsuccessful. The match ended by Simba 2 and Yanga 0. The man of the match was Patrick Mafisango.
The winner was Simba. that is why i said a new beginning.

Monday, August 15, 2011

Huu ni mchezo mchafu ......

       Siku 12 baada ya serikali kutangaza kushushwa kwa bei ya mafuta nchini hali imerudi kama awali. EWURA imetangaza kuongezeka kwa bei ya mafuta ya Dizeli, Petrol na mafuta ya taa. Hadi kufikia leo asubuhi vituo vingi vya mafuta hapa jijini Dar es salaam na ngineko vilikuwa vimeshabadirisha bei na kutumia mpya zilizotangazwa na chombo hicho cha serikali. Ikumbukwe kwamba huu ni mwendelezo wa machungu kwa Watanzania wa kipato cha chini ambao walitarajia kuwa kushuka kwa bei ya mafuta kama ilivyotangazwa hapo agosti 3 kungewasaidia japo palikuwepo na usumbufu mkubwa wa upatikanaji wa mafuta wiki iliyopita.
    Hii nia hatua nyingine ambapo serikali itapata changamoto kutoka kwa wadau mbalimbali wa kupigania haki na maendeleo nchini. Kwangu mimi naweza nikasema huu ni mchezo mchafu "Siasa". Hapa naomba tuelewane kidogo ndugu wananchi wenzangu. Bei hii ya mafuta imepandishwa kukiwa na matukio makubwa ya kuihusianisha. Mosi ni kupitishwa kwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapema juzi Jumamosi. Kabla hata masaa 24 ya kupitishwa kwa bajeti hiyo ewura wakapandisha mafuta. Hii inaweza ikatusaidia kufikiria mrorongo huu wa matatizo ya mafuta kama matimizo ya matakwa ya siasa na si kwa mahitaji ya wananchi. Pili, bei hii mpya ya mafuta imepanda wakati serikali ikiwa na mazungumzo ya kina na wafanyabiashara wa mafuta nchini na huku wengine wakiwa wamechukuliwa hatua madhubuti kama kampuni ya British Petrolium (BP). Kwa haraka naweza nikasema serikali imekuwa lobbied na wafanyabiashara hawa wa mafuta.
     Tukumbuke kuwa wakati Serikali inatangaza kushuka kwa bei ya nishati hii muhimu mnamo agosti 3 mwaka huu hali ya uchumi Duniani ilishaanza kuwa tete. Kwa hiyo tumepigwa changa la macho hapa. Ishu si kuanguka kwa thamani ya shilingi  yetu ila kuna sababu nyingine zaidi ya hiyo.
  Ewe Mtanzania tafakari!

Friday, August 12, 2011

BP bado ngangari mgomo wa mafuta


                             Moja ya vituo vya mafuta vya BP kikiwa hakitoi huduma ya
                                        mafuta hata baada ya masaa 24 ya serikali kupita.

       Baada ya Watanzania kukosa nishati ya mafuta kwa takriban siku tano mfulilizo baadhi ya vituo vilianza kutoa mafuta haraka mara tu baada ya Waziri mwenye dhamana ya nishati hiyo kutoa masaa 24 kwa wote wanaohusika na usambazi au uuzaji wa nishati hiyo. Hadi kufikia alhamisi ya tarehe 11 asilimia ya kubwa ya vituo hivyo vya mafuta vilianza kuuza nishati hiyo kwa wananchi waliokuwa wamechoshwa na uadimu wa nishati hiyo. Hata hivyo baadhi ya vituo vingine vya mafuta kama kampuni kongwe hapa nchini Brtiish Petroleum (BP) ambapo Serikali ya Tanzania ina hisa Asilimia hamsini havitoi huduma hiyo licha ya masaa 24 ya serikali kupita. 
      Wananchi wengi bado wana maswali  mengi vichwani mwao kuhusu ukaidi huu wa BP na makampuni mengine hasa ambayo hayana majina kwa kutokutii amri ya serikali. Naamini kuwa na hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa kwamba hakuna kitu kingime zaidi ya Serikali. Serikali ndio kila kitu katika masuala ya huduma kwa wananchi. Uwepo wa makampuni binafsi ni moja ya njia tu za kuongeza ufanisi na umakini katika utoaji huduma hitajika kwa Watanzania. Bado wananchi wengi hawana taarifa rasmi za kwanini BP haifanyi kazi? Hatutakiwi kulaumu  harakaharaka kuhusu hili suala bila ya uchunguzi na tafakari ya kina. Inawezekana kuwa jamaa ndio wameacha kabisa kuuza nishati hiyo au bado ipo njiani kuletwa nchini tayari kwa huduma. Hata kama majibu ndo hayo sisi kama wateja wa BP ilibidi tujulishwe hata kwa  njia ya magazeti na matangazo mengine Radioni na Televisheni kuwa huduma hii imesitishwa kwa muda na waombe radhi kwetu sisi wanachi ambao ni wateja wao. Iwapo watafanya hivyo watakuwa wamefuta kashfa ya kuwa wameigomea Serikali na kama sababu si hizo Serikali ichukue hatua kali dhidi ya kampuni hili hata kama wamegawana hisa.
        Ni matarajio yangu kuwa miaka na siku zijazo hatuoni tena uzembe na hasara zilizojitokeza kuhusiana  na mgomo wa wafanyabiashara wowote licha ya hawa wauza mafuta. Ni dharau kubwa kwa Serikali kusumbuliwa na wafanyabiashara. Na iwapo itatokea tena hivyo lazima tukubaliane kuwa Serikali yetu ni lobbied na wafanyabiashara na Sera zote zilizopo zinasadifu matakwa ya vigogo na wafanyabiashara na si wananchi. Hivyo basi Watanzania wote tuungane tena mara nyingine na siku nyingine litakapo tokea hili kuupinga mgomo na hata Serikali itakayokuwepo madarakani. Hatutakubali kuingizwa kwenye hasara za kizembe za nchi zima kwa Mabepari wawili.
       Mungu Ibariki Tanzania, Mungu tubariki watoto wa Tanzania!
    

Friday, August 5, 2011

The best Hits of the week

 1. Mathematics-Roma
2. Ridhione-Izzo Business
3.Wango- Jay D ft Mr Blu
4.Mganga-Sajna ft Josefly
5.Nlilipe nisepe- Belle 9
6.Kizunzungu- Dyna
7.Na huku wapo- Samu wa ukweli
8.Gangsta- Chege & Temba ft Ferooz
9. Zila ni balaa- Godizilla
10.Kiujamaa-Nikki II

Monday, August 1, 2011

"Nuru mpya ya mabadiliko hii hapa..."

Wapendwa Watanzania, yapata miaka 50 sasa tangu nchi yetu pendwa ilipopata uhuru toka kwa Mkoloni wa Kiingereza. Serikali nne tofauti zimetuongoza mpaka tumefika hapa tulipo toka ile ya Hayati Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius K. Nyerere, Mzee A.H. Mwinyi, Benjamin W. Mkapa na hii ya sasa ya Mheshimiwa Rais Jakaya M. Kikwete. Kama Mataifa mengine duniani yaliojikomboa kutoka kwa Mkoloni nchi yetu chini ya serikali zake imefanya mipango(Nation Building Projects) mbalimbali ili kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Lakini licha ya michakato hiyo ya maendeleo bado Watanzania hatujapata matunda halisi ya Uhuru. Maisha magumu ndio Wimbo wetu kila siku.
      Hivyo basi ili kujenga mustakabali chanya kwa Watanzania wote nchini na nje ya nchi, mimi kama Mtanzania mpenda mabadiliko na ninaeguswa na harakati mabalimbali za watu binafsi na Taasisi mbalimbali katika kuleta maendeleo na kupigania haki mwiongoni mwetu (Watanzania) napenda kutumia blog hii kujadili mambo mabalimbali ya Kiuchumi, Kisiasa, Kijamii, Mazingira, Michezo na Burudani na mengine yanayotuhusu ili kujenga Tanzania yetu. Naahidi kushirikiana na kuyaendeleza mambo mazuri ya wote waliotangulia katika harakati hizi za kuijenga Tanzania bora na endelevu.
    Ewe Mtanzania!  ungana nami katika  nuru hii ya mabadiliko ya kweli kutoka leo  ili tuijenge Tanzania yetu.
    Mungu Ibariki Tanzania, Mungu tubariki Watoto wa Tanzania!