Monday, September 12, 2011

Salha Israel: Vodacom miss Tanzania 2011


    Hatimaye aliyekuwa Miss Redds Ilala, Salha Israel ameibuka mshindi wa Vodacom miss Tanzania 2011. Fainali za mashindano haya zilifanyika usiku wa Jumamosi wa tarehe 10 mwezi huu ndani ya ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na wapenzi wa tasnia ya urembo kibao. Salha aiibuka mshindi kati ya warimbwende 30 waliokuwa wakigombania taji hilo.
Mshindi wa Miss Vodacom Tanzania 2011 Salha Israel katikati akiwa na Mshindi wa pili Tracy Sospeter (kulia) na mshindi wa tatu Alexia william (Kushoto)
    Shindano la Umiss Tanzania mwaka limeonekana kuboreshwa zaidi kuliko miaka ya nyuma. Wadhamini wakuu wa shindano hili mwaka huu (Vodacom) wamejitahidi kufuta lawama nyingi zilizokuwa zikitoka mara kwa mara baada ya mashindano ya Miss Tanzania kuisha takribani miaka yote ya nyuma. Tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu watu hawalaumu sana badala yake wanaonekana kusifia mfumo mzima uliotumika kuyaandaa mashindano haya.
Diamond Platnumz na Vijana wake wakilisakata jukwaa la Miss Tz usiku wa Jumamosi, Mlimani City.
      Kuanzishwa kwa Vodacom House na kupigia kura warembo wakiwa ndani ya jumba hilo kuliongeza msisimuko mkubwa na uhalali wa mashindano haya. Warembo Thelathini kutoka Mikoa mbalimbali na Vituo walishiriki mashindano haya. Katika fainali hizo mshindi wa pili ni Tracy Sospeter na mshindi wa tatu ni Alexia William. Huu ni mwanzo wa safari kwa mrembo Salha Israel kuelekea mashindano ya Miss world mwaka huu. Mshindi wa Kwanza Salha Israel alizawadiwa gari aina ya Jeep na zawadi nyingine nyingi kutoka kwa Wadhamini.
Washiriki wa Vodacom Miss Tanzania 2011 wakiwa katika picha pamoja.
     Licha kuwa na mvuto na maboresho mengi baadhi wadau wa tasnia ya Urembo wamelalamikia ukosekanaji wa tiketi za kuhudhuria shindano hilo. Tiketi mwaka zilionekana kuwa chache sana kwa Wananchi wa kawaida kuliko Miaka ya nyuma. Baadhi ya Wananchi wamelalamikia kiwango cha kuingilia kuwa kikubwa mno tofauti na siku za nyuma.
    Wasanii mbalimbali kama Diamond, Akil the Brain akiwa na SaRaha na Big Jahman, Juliana kutoka Uganda pamoja na Bob Junior (Rais wa Masharobaro) walitoa burudani ya nguvu katika shindano  hilo na kuufanya usiku wa Miss Tz kuwa mfupi.
    Kwa ambao hawakubahatika kuhudhuria shindano hili pale Mlimani City waliweza kutizama live kupitia Kituo cha televisheni cha Star Tv ambao pia walikua moja ya Wadhamini wa shindano hili chini ya Sahara Communication.
 Salha Israel akionyesha funguo za Jeep baada ya kushinda Umiss Tz 2011.
   Baada ya ushindi wa Salha kuwa Miss Tanzania 2011, Watanzania bado tunahitajika kumjenga, kumshauri na kumuandaa vema mrembo huyu ili aweze kutuwakilisha Vyema katika Mashindano ya Miss World. Kila la Kheri Salha na bado Watanzania tunakuombea uweze kufika mbali zaidi katika tasnia hii ya Urembo.  Hongera, na Mungu Akubariki!

No comments:

Post a Comment