Tuesday, November 27, 2012

R.I.P SHARO MILIONEA

Nuzulack Dausen

Kifo cha Msanii wa Maigizo na Muziki Hussein Mkiety a.k.a Sharo Milionea kimenishtua sana. Nilipoipata habari ya kifo chake mapema leo asubuhi nilidhani rafiki zangu wananitania kwa kuwa msanii huyu alikuwa ni  maarufu wa vituko na vichekesho vingi na alishika akili za watanzania wengi kwa staili yake ya Kisharobaro hivyo walitaka tu kunighiribu akili yangu. 


Hata hivyo haukupita muda mrefu taarifa zikawa zimeshasambaa kwenye vituo mbalimbali vya habari na kufanya taarifa hiyo kuwa rasmi. Taarifa hizo zinathibitisha kifo chake kilichosababishwa na ajali ya gari gari yenye namba T478 BVR Toyota Harrier alilokuwa akiliendesha katika kijiji cha Lusanga Wilayani Muheza Mkoani Tanga na kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa  Tanga, Constatine Masawe alithibitisha kutokea.  

Binafsi nautambua mchango wa Sharo Milionea katika gemu la Bongo Movies na Bongo Fleva. Uwepo wa Sharo Milionea katika gemu kwa muda mfupi kuliamsha ari ya wasanii wengi wachanga kuingia kwenye gemu na hata wale wakubwa kukaza ili kukabilana na ushindani mkubwa alokuwa ameuanzisha Sharo Milionea.

Kwa muda huo mfupi katika muziki na filamu Sharo amekuwa gumzo miongoni mwa wadau wa muziki na filamu kwa staili zake ambazo zimekua zikitoa burudani safi ya tofauti na wasanii wengine.

“Umebugi meeni” “nasubiri mrija meeni” ni baadhi tu ya maneno ya Sharo yaliyozoeleka midomoni mwa mashabiki wake. Maneno hayo hayakumpa tu umaarufu yemwenyewe bali mpaka baadhi ya bendi za Dansi ziliyatumia. Watoto mitaani na baadhi ya watu wazima walitumia maneno hayo kutaniana.

Binafsi nimesikitishwa sana na kifo chake lakini hatuna cha kufanya kwa kuwa yote hayo ni mipango ya Mungu. Yeye ametangulia, sisi tutafuatia.

Nawapa pole ndugu wa karibu wa marehemu Sharo Milionea, Wasanii wote wa Bongo Movies na Bongo Fleva, Mashabiki na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuondokewa na Msanii muhimu sana katika maendeleo ya sanaa nchini.

Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Mungu amlaze mahali pema peponi Sharo Milionea.








No comments:

Post a Comment