Saturday, February 13, 2016

Wewe ndiye Valentine wangu wa kweli

Nuzulack Dausen
Twitter: @nuzulack
Kwako mke wangu mtarajiwa. Valentine imewadia tena.
Najua bado una huzuni na wasiwasi nimekutelekeza. Una hofu na miaka inavyokwenda kasi bila kunipata mimi, kipenzi chako cha kweli.
Rafiki zako ambao mwaka jana walikuwa waseja kama wewe, tayari wameshaolewa ama kuchumbiwa. Na wewe umeshiriki kikamilifu kuwaoza.
Lakini bado wanisubiri nifike, nije kukuoa licha ya kuwa miaka inazidi kuyoyoma. Hujakata tamaa.
Nafahamu bayana mabarobaro wengi hujipitisha pitisha na kukulaghai uwakubali. Lakini moyo wako u thabiti na hujawapa nafasi. Ndoto yako ya kuwa na mimi imekutawala siku zote.
Mwaka jana nilikusihi usifadhaike wakati wa sherehe za valentine. Nilikusihi usisitetereke na rafiki zako waliokuwa wakiringa kwa zawadi walizopewa na mabwana zao. Mwaka huu pia Valentine inabisha hodi.
Hujapata zawadi yoyote wala ujumbe mzuri kwenye simu yako. Ungetamani umpate mtu wa kukubembeleza ukichoka na kazi na wakati ukiumwa.
Ungetamani uwe na mfalme wa moyo wako ambaye muda wote angekuwa na wewe akikujali na kukupa mapenzi moto.
Kiufupi, unamtaka mume wa kukufanya mke mwema na chaguo la kweli. Lakini bado giza linakuzuia usione nuru. Nuru ya maisha mapya ya kuwa wawili na kutekeleza masharti ya vitabu vya dini.
Tafadhari vumilia.  Hata Valentine hii imefika na hujaniona, usifadhaike. Narudia usikate tamaa. Nipo nakuja japo sijafika karibu yako. Sidhani kama ni Valentine hii lakini utaniona.
Usitishike na rafiki zako wanaokutambishia zawadi za smartphone walizopewa na mabwana wanaotaka kuwachezea. Wala usibabaike na selfie zao wanazoweka mtandaoni wakiweka ‘status’ za “Ready for Valentine (Tayari kwa valentine).”
Mimi ndiyo zawadi yako ya kweli. Zawadi ya kudumu ya maisha yako. Duniani na mbinguni. Upendo wangu kwako ni zaidi ya zawadi ya smartphone au Vitz. Upendo wangu haubanwi na muda eti mpaka siku ya Valentine pekee la hasha. Mimi ni wako siku zote.
Nakupenda kila siku japo hatujawahi onana. Nakuw
aza wakati wote na nakupenda kutokana na uzuri wa asili ulionao, heshima, upole, werevu, ubunifu na uvumilivu wako.
Siyo mapepe wala waruwaru wa kukufanya nyumbani kwetu wakukatae. Huropoki ovyo na kulalamika mara kwa mara mbele za watu hata kama mtu kakukosea mara 1,000. Huvai nguo za vipisi zikakuonyesha maungo yako kana kwamba upo sokoni.
Huweki nyusi za bandia na kujisiliba rangi tofauti usoni ukaonekana kama kichekesho mbele za watu. Hujawahi waza kuweka makalio ya ziada kwa sababu una uhakika mimi situmii maumbo hayo kama kigezo cha mwanamke mzuri.
Hutumi mara kwa mara picha mtandaoni kuonyesha unaponda raha kwa kuwa unajua mwanamke bora hupenda kusitiri mwenendo wa maisha yake binafsi na ya nyumbani.
Hakika wewe ndiyo Valentine wangu. Na mimi ndiyo Valentine wako wa kweli. Nisubiri nije nikupoze moyo. Nivumilie kidogo tu. Nikifika, sitachelewa, nitakutolea posa na kukuoa.
Nikutakie heri ya wapendanao huko uliko japo kila siku hufanya hivyo. Nakupenda mchumba wangu.


No comments:

Post a Comment