Wednesday, July 4, 2012


Tumehitimu Vyuo Vikuu……….. wapi ajira?
Mwishoni mwa mwezi wa sita na mwezi huu wa saba taasisi nyingi za elimu ya juu zimeanza kutoa wahitimu wa taaluma mbalimbali na katika  ngazi tofauti za elimu toka cheti, diploma, degree na masters. Wanafunzi tuliohitimu ni maelfu kwa maelfu kutoka zaidi Vyuo vikuu 30 na Vyuo vya  mafunzo ya ufundi (Vocational Training Colleges). Kundi lote hili la wahitimu linahitaji ajira katika makampuni binafsi na Serikali huku asilimia ndogo sana ya wahitimu wakipanga kujiajiri. 

Baadhi ya Wahitimu wa Shahada ya Sayansi Siasa na Utawala kutoka  Chuo Kikuu cha Dar es salaam 2009/12 katika picha pamoja baada ya mtihani wao wa mwisho. Picha kwa msaada wa Political Science gradutes 2012 facebook page
Inafahamika wazi kuwa mwajiri mkuu nchini ni Serikali huku sekta binafsi ikichikua asilimia zilizobaki. Pia ifahamike kuwa hata hao waajiriwa katika sekta binafsi hufanya kazi mara nyingi katika sekta isiyo rasmi (informal sectors). Wakati jamii kubwa ikitegemea Serikali itoe ajira kwa wahitimu hawa, Serikali yenyewe imejikuta ikishindwa hata kuwahudumia watumishi waliopo. Matatizo mengi yanayohusu ajira za wafanyakazi wa Serikali yameshuhudiwa kwa muda mrefu likiwemo hili linaloshika Vichwa vya habari hivi sasa la mgomo wa madaktari. Serikali imeshindwa kutoa stahili husika kwa Wafanyakazi wake.


Pia serkali imeweka vigezo vigumu sana ambavyo kwa wahitimu wa sasa na wa mwaka jana hawawezi kuomba kazi. Moja ya vigezo hivyo ni kuwa na cheti halisi cha chuo Kikuu na si Provisional statements au transcripts kama ilivyozoeleka. Pili uzoefu kazini bado ni wimbo usiochuja, bado uzoefu usiopungua miaka kadhaa unasisitizwa. Jambo jingine ni ufinyu wa bajeti ya serikali katika kuongeza ajira. Serikali imekua ikijitetea kuwa haina uwezo kifedha kuajiri idadi kubwa ya Wafanyakazi licha ya kuwa na upungufu mkubwa wa watumishi katika taasisi zake. Jingine ni unamfahamu nani kwenye system ya Serikali ili upate kazi kama humfahamu mtu basi nauli yako imeisha. Je kama hali ndo hiyo maelfu ya wahitimu mwaka huu tutaende wapi?

Kwa upande wa Sekta binafsi,  makampuni mengi hayaajiri idadi kubwa ya watu kwa misingi ya kupunguza gharama za uendeshaji. Idadi ndogo sana ya wahitimu huajiriwa na Sekta binafsi iliyo rasmi kama Benki, Viwandani na Makampuni madogomadogo ya biashara. Pia ifahamike tena kuwa sekta binafsi huchagua kundi Fulani la Wahitimu hasa kwa kuangalia ufaulu na uzoefu kazini. Kwa wahitimu waliowengi uzoefu bado mdogo zaidi ya mafunzo ya vitendo ambayo hupatikana kwa njia ya interns (Practical trainings). Kwa upande wa performance kuna kundi kubwa la wahitimu halina First Class degrees au diploma wanazotaka. Uzito na ugumu wa kozi vimetofautiana kutoka aina Fulani ya masomo kama engineering Vs arts au toka Chuo kimoja hadi kingine kama University of Dar es Salaam Vs Tumaini n.k. Kwa utofauti huu wangapi wataajiriwa?

Kwa upande wa Kujiajiri bado kuna tatizo kubwa. Ni idadi ndogo sana ya wahitimu ambao wana uwezo wa kujiajiri wenyewe. Tatizo sio kuwa hawana uwezo wa kujiajiri kwa kufanya biashara na mambo mengi bali ukata wa kifedha na mfumo wa elimu ni vyanzo vikuu hali hii. Mfumo wa elimu ya bongo unamuandaa mwanafunzi kuajiriwa na si kujiajiri. Mfano mzuri ni pale mtu aliyehitimu VETA anapotafuta ajira. Mfumo huu hauna utofauti na ule wakikoloni wa kuandaa watu kufanya kazi za kuajiriwa maalufu kama white Color Jobs. Jambo jingine ni kukosa kwa mtaji wa kuanzisha biashara. Benki zimekuwa na imani ndogo sana kukopeha wahitimu kwa kuwa hawana dhamana yoyote zaidi ya Cheti na akili tu kichwani.  Pia wengine wanakatishwa tama na urasmu wa kusajiri biashara Serikalini na mfumo mzima wa kodi ambao unaharibiwa na wafanyakazi wenye tabia ya rushwarushwa (rent seeking behavior)
Mimi wa pili kushoto waliosimama na wahitimu wengine baada ya kumaliza mtihani wa mwisho wa shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala, June 20, 2012 Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM)

Hii ndio halisi ambayo wahitimu wengi wa Vyuo mbalimbali nnchini wanakumbana nazo. Jamii haitakiwi kuwalumu Vijana kwa dalili za utegemezi wanaouonyesha zaidi jitahada malimu zinahitajika kutatua tatizo la kupunguza vifaranga vingi vinavyototolewa Vyuo Vikuu huku vikienda kwenye mabanda ya no ajira.

Tujifunze kupitia haya. Tutafute njia mbadala wa kutatua tatizo kwa kila mdau nchini.

No comments:

Post a Comment