Tuesday, July 10, 2012

Njia za kutatua Migomo Vyuo Vikuu Tanzania hizi hapa.

MAONI YANGU KWA UTAWALA WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM JUU YA NAMNA YA KUONDOA AU KUPUNGUZA MIGOMO NA MAANDAMANO YANAYOONEKANA KUONGEZEKA KILA KUKICHA.
Na: Ole Mesaya

Tatizo la migomo na maandamano ndani ya chuo kikuu cha Dar es salaam halijaanza hivi karibu. Tatizo hili lilikuwepo toka enzi lakini kwa miaka ya hivi karibuni limeonekana kushika kasi zaidi na kupelekea chuo kupoteza rasilimali nyingi na kuwatimua chuo wanafunzi wote ambao wanaonekana kuwa ni chanzo cha tatizo hili. Pamoja na jitihada zote hizi zinazofanywa na uongozi wa chuo bado tatizo hili limeonekana kutokoma, zaidi wanafunzi wengi wanazidi kupotea na rasilimali nyingi zinatokomea bila mafanikio.

Ningependa kuchukua nafasi hii kama mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam kutoa maoni yangu juu ya nini kifanyike ili kupunguza kama sio kutokomeza kabisa suala la migomo ndani ya chuo chetu.
I. Kwanza kabisa Chuo pamaja na taasisi zinazohusika zijitahidi kukabiliana na kutatua matatizo yanayowakabili wanafunzi kwa njia ya majadiliano na kwa haraka zaidi na siyo kusubiri mpaka mgomo au maandamano kutokea. Tofauti na ilivyo sasa hivi, ambapo taasisi zinazohusika zinasubiri mpaka mgomo utokee ndipo wachukue hatua za kukabiliana na mgomo badala ya kuchukua hatua hizo kukabiliana na matitizo hayo kabla mgomo haujatokea.

II. Chuo kiangalie zaidi na kijikita kwenye vyanzo vya migomo, ikiwa ni pamoja na sababu ya mgomo kutokea kuliko kujikita na kuwapa adhabu wanafunzi wanaoanzisha na kushiriki kwenye mgomo huo. Kwa kufanya hivyo chuo kitakuwa kimezuia uwezekano wa mgomo mwingine kutokea kuliko ilivyo sasa ambapo chuo kinawapa adhabu, ikiwepo kuwafukuza chuo wanafunzi wanaooekana kushiriki kwenye mgomo ilihali tatizo lilosababisha mgomo likibaki bila muafaka.

III. Chuo kiweke utaratibu ambao utawalazimu viongozi wa serikali ya wanafunzi kukutana na wanafunzi na kujadili kwa pamoja juu ya matatizo na changamoto zinazowakabili wanafunzi angalau mara tatu kwa muhula wa masomo yaani mwanzo, katikati na mwishoni mwa muhula wa masomo. Tofauti na ilivyo sasa ambapo school baraza ipo mara moja tu kwa mwaka na mara nyingi imekuwa haifanyiki. Kwa kufanya hivi wanafunzi wataweza kuwasilisha changamoto zinazowakabili kwa uongozi wao na hoja hizo kuwasilishwa panapohusika haraka na mapema zaidi.

IV. Chuo kikuu kifanywe kitovu cha kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto zinazoikabili nchi yetu. Hii itawezekana kama chuo kitaweka utaratibu wa kuruhusu jukwaa la malumbano ya hoja baina ya wanafunzi angalau kila jumamosi ya mwisho wa wiki, kwani hii itawapa nafasi vijana na wasomi wa vyuo vikuu kushiriki katika harakati za kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi yetu. Kwa kufanya hivyo chuo kitakuwa kimeondoa uwezekano wa wanafunzi kufanya mikutano isiyo ya halali kama ilivyo sasa kujadili mwenendo na hatma ya taifa letu.

V. Ilivyo sasa, Chuo kinatumia rasilimali na nguvu nyingi kupambana na wanafunzi. Kwa kufanya hivi Chuo kitakuwa kinapambana na wahanga wa tatizo huku tatizo likiendelea kushamiri na kunawiri pasipo kutafutiwa ufumbuzi wa kuliondoa tatizo lenyewe. Kwa maoni yangu chuo kingetumia nguvu hizo na rasilimali hizo kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi, kwani kama wataendelea kupambana na wanafunzi na kuliacha tatizo likiendelea kukua ni dhahiri shairi kwamba migomo na maandamano kamwe hayatakwisha kwani chanzo cha mgomo bado kipo na kinaendelea kukua.

VI. Pindi mgomo au maandamano yanapotokea, chuo kijikite zaidi kwenye tatizo lililosababisha mgomo kuliko kukimbilia kuhusisha matatizo yaliyosababisha mgomo na vyama vya siasa. Kwani kufanya hivyo kamwe hakutakuwa na suluhisho la migomo na maandamano, kutokana na kwamba tatizo halisi litakuwa limeachwa kwa kujikita kwenye hoja isiyo ya msingi.

VII. Pindi adhabu inapotolewa na chuo, Chuo kijitahidi kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuondoa malalamiko miongoni mwa wanafunzi pamoja na wale waliopewa adhabu. Kwa mfano wanafunzi wapewe adhabu baada ya kuhojiwa na kusikilizwa ushahidi wao badala ya kufuata hisia na hasira kama ilivyo sasa. 

VIII. Uongozi na utawala wa chuo usikimbie changamoto bali watumie changamoto hizo kama vyanzo vya uwajibikaji. Tofauti na ilivyo hivi sasa, wenye madaraka ndani ya chuo kikuu wanakwepa changamoto zinazowakabili wanafunzi kwa kuogopa kupoteza nafasi zao za madaraka endapo wataungana pamoja na wanafunzi kuwasilisha changamoto hizo panapohusika.

IX. Serikali ya wanafunzi DARUSO iwe chombo huru na kinachotambuliwa na kuheshimiwa na utawala wa chuo kikuu cha Dar es salaam. Ilivyo sasa, serikali ya wanafunzi DARUSO haitambuliwi wala kuheshimiwa na utawala wa chuo kwani katika hatua zote za kinidhamu zilizochukuliwa na utawala wa chuo kwa wanafunzi, serikali ya wananfunzi haijajulishwa kimaandishi. Mfano barua zote za kuwasimamisha na kuwafukuza chuo wanafunzi hakuna nakala yoyote iliyopelekwa kwa serikali ya wanafunzi.
Ni matumaini yangu kwamba kama tutashirikiana kwa pamoja kuyatekeleza haya, siyo siri tutakuwa tumepunguza kama siyo kutokomeza kabisa mianya yote inayosababisha migomo na maandamano na kushusha heshima ya chombo hiki cha umma.

Asanteni.
Maoni haya yamenivutia sana mpaka nimeona niyachapishe hapa ili wahusika waweze kuchukua chochote wanachoona kinafaa kutatua Migomo Vyuo Vikuu nchini hususani Utawala wa Vyuo hivyo na Serikali. Pia serikali za Wanafunzi kama DARUSO, IFMSO, UDOSO na zingine zisome makala hii kujiongeza. maoni haya ni mali ya mwandishi Bwana ole Mesaya pichani juu. Yametolewa toka kwenye Ukurasa wa facebook wa UDSM. Bofya hapa kujiunga

No comments:

Post a Comment