Saturday, December 8, 2012

STANBIC NA CAT FINANCIAL WASHIRIKIANA KUKOPESHA WAKANDARASI



Nuzulack Dausen

Wakandarasi na wafanyabiashara mbalimbali nchini wanatarajia kunufaika na mkopo wa mashine na mitambo mbalimbali ya Ujenzi ya aina ya Caterpillar baada ya Benki ya Stanbic Tanzania kusaini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na kampuni ya Cat Financial ambayo ni mdhamini mkuu wa kifedha wa Vifaa hivyo.

Katika mkataba huo Wakandarasi wa ndani watanufaika na huduma za kifedha hasa zile za mikopo zenye masharti nafuu na zitakazowawezesha kununua mitambao bora, ambayo itasaidia utendaji kazi kwa ufanisi na ubora zaidi.

Lilian Kitomari(kushoto) wa Stanbic Benki akizungumza wakati wa hafla hiyo, katikati ni
Neimat El Maghraby  Mkuu wa Kitengo cha fedha Mantrac Unatrac Group na kulia ni Adel Selim  meneja wa mantrac Kanda ya Afrika Mashariki.
Akizugumza katika hafla ya kusainiana mkataba huo jijini Dar es salaam hivi karibuni Meneja wa Rasilimali na Bima wa Benki ya Stanbic Tanzania Lilian Kitomari alisema benki yake itaendelea kutoa huduma na njia madhubuti zitakazosaidia wateja wake kutatua matatizo mbalimbali ya kifedha ili kukuza biashara zao nchi nzima.


Meneja wa Mantrac kanda ya Afrika Mashariki Adel Selim akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini ya makubaliano ya kibiashara yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam.
Aidha, Rais wa kampuni ya Cat Financial ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Caterpillar Inc, Kent Adams, alisema kuwa “mchanganyiko huo wa bidhaa unaotambuliwa kimataifa kati ya  kampuni ya Cat na Benki ya Stanbic ambazo zinaheshimiwa na kuaminiwa na taasisi za kifedha barani Afrika vitajenga nguvu ya ushindani wenye faida kwa mitandao yetu na wateja wao na kuongeza mauzo yao ya vifaa.”

Naye Naibu Ofisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Standard, Bw. Ben Kruger, alisema “tuna thamini uhusiano wetu uliopo na kampuni ya Cat na tunaamini kuwa uhusiano huu unatoa jukwaa la kuimarisha mahusiano haya na kutoa huduma zaidi kwa nchi nyingine katika bara la Afrika.”

Alisema kuwa Benki ya Standard  Chertered ambayo ni Kampuni mama ya Stanbic Tanzania yenye shughuli zake barani Afrika ina timu ya wataalam ambao ni wazoefu  wa biashara na kanuni, watahakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wateja wa benki hiyo na kampuni ya CAT Financial.
Aliongeza kuwa mpango huo wa magari na rasilimali unafadhiliwa na Benki ya Standard  Chartered ya Afrika Kusini.

Wafanyabiashara hao wa Tanzania wataungana na wenzao wa nchi tano za Nigeria, Kenya Uganda, Ghana na Sierra Leone, ambapo huduma hizo zitatolewa.

Ni kipindi kirefu sasa  Wakandarasi wengi nchini wamekuwa wakilalamikia kukosa mitaji itakayowawezesha kununua mitambo mikubwa na bora ambayo ni chachu ya  kufanya kazi zao kwa ufanisi na ubora zaidi jambo linalowafanya kukosa zabuni mbalimbali za Ujenzi ambazo kampuni za kigeni zimekuwa zikinufaika nazo kwa kuwa na mitambo na mashine za kisasa.


No comments:

Post a Comment