Tuesday, March 19, 2013

TAARIFA YA AFRICAN BARRICK GOLD KUHUSU UWEKEZAJI WA MFUKO WA MAENDELEO WA ABG




DAR ES SALAAM – Kampuni ya uchimbaji madini ya African Barrick Gold (ABG) inafuraha kutoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo wa ABG tangu kuanzishwa kwake mnamo Septemba 2011.

Mfuko huu umesimamia uwekezaji wa kampuni ya ABG kwenye jamii katika kipindi kilichopita cha miezi 18 na kufanikiwa kutekeleza zaidi ya miradi 50 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 7.5 (takriban shilingi bilioni 12 katika kipindi cha mwaka 2011/12.

Greg Hawkins, Afisa Mtendaji Mkuu wa ABG, amesema: “Tunafurahi kuona mafanikio makubwa ambayo Mfuko wa Maendeleo wa ABG umeyapata kwenye kipindi cha miezi 18 mpaka sasa. Tulianzisha Mfuko huu kama sehemu ya jitihada zetu za kuchangia kwenye maendeleo endelevu nchini Tanzania na tayari tumeona mafanikio makubwa kwenye zaidi ya miradi 50 mpaka sasa."

"Tunaendelea kuweka msisitizo kuhakikisha kuwa jamii zinazotuzunguka zinapata faida kutokana na kuwepo wa shughuli zetu kwenye maeneo yao na ninafurahi kutangaza kuwa kampuni ya ABG itaendelea kutenga dola za Marekani milioni 10 kila mwaka kwa ajili ya uwekezaji wa Mfuko wa Maendeleo wa ABG kwa mwaka 2013."

Mpaka hii leo, Mfuko wa Maendeleo wa ABG umewekeza dola za Marekani milioni 2.2 (zaidi ya shilingi bilioni 3.6) kusaidia kuboresha afya ya umma kwenye jamii zinazozunguko migodi yake.

Mfuko huu pia umesaidia kujenga miundombinu na kuwawezesha wananchi wapate huduma za afya ya msingi na za hospitali ya rufaa. Pia Mfuko umewekeza kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa sekta ya afya ili waweze kuboresha upatikanaji wa huduma za afya.

Kwa upande wa elimu, Mfuko umetumia zaidi za dola za Marekani milioni 1.9 (takriban shilingi bilioni 3) kuwekeza kwenye sekta hii muhimu. Uwekezaji wa Mfuko huu umesaidia kujenga shule mpya na kuongeza idadi ya madarasa kwenye shule nyingine ili kuwapa watoto wengi zaidi fursa ya kupata elimu bora.

Mfuko pia umewekeza kwenye ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni ya wanafunzi, na maabara ya masomo ya sayansi, sambamba na kuboresha miundombinu mingine ya shule ili kuleta ufanisi kwenye utoaji wa huduma na kuboresha mazingira ya elimu.

Mfuko wa Maendeleo wa ABG pia umewekeza dola za Marekani milioni 1.4 (sawa na shilingi bilioni 2.2) kuhakikisha upatikanaji wa huduma za maji safi ikiwa ni moja ya michango yake kwenye maendeleo ya jamii.

Kwenye mgodi wa North Mara uliopo wilaya ya Tarime, Mfuko umewekeza dola za Marekani
800,000 (sawa na shilingi bilioni 1.3) kuchimba visima vya maji ili kuwasaidia wananchi wapate maji safi na salama ya kunywa.

Ili kuboresha maisha ya wananchi kwenye jamii zinazozunguka migodi yetu minne, Mfuko wa Maendeleo wa ABG umewekeza dola za Marekani 1.4 milioni (zaidi ya shilingi bilioni 2) kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii.

“Tumeanza kuona mafanikio kwenye uwekezaji wetu wa jamii na tutandelea na njia hiyo. Uamuzi wa kuendelea kutenga dola za Marekani milioni 10 kwa  Mfuko wa Maendeleo wa ABG mwaka huu utawezesha tuendelee na kazi ambayo tumeianza, huku tukiweka msisitizo zaidi kwenye maendeleo ya jamii,” amesema Hawkins.

Mfuko wa Maendeleo wa ABG unashirikiana na jamii husika kubainisha vipaumbele vyao ili wanajamii wenyewe wawe mstari wa mbele kwenye utekelezaji wa miradi. Kipaumbele kinatolewa kwa programu ambazo zinaendelezwa kwa njia shirikishi huku kukiwa na ushirikiano wa karibu na washikadau mbalimbali kutegemea na mahitaji ya jamii na mikakati ya maendeleo ya serikali.

Kampuni ya ABG inalipa gharama zote za uendeshaji wa Mfuko wa Maendeleo wa ABG ili kuhakikisha kuwa asilimia 100 ya fedha za Mfuko huo zinaenda moja kwa moja kwenye miradi ya jamii.

Kuhusu Kampuni ya African Barrick Gold

ABG ni kampuni kubwa kuliko zote za uchimbaji wa dhahabu Tanzania na ni kati ya kampuni tano kubwa zaidi za uchimbaji wa dhahabu barani Afrika. Tuna migodi minne ya dhahabu nchini (Bulyanhulu, Buzwagi, North Mara na Tulawaka), yote ikiwa kaskazini magharibi mwa Tanzania na tuna miradi kadhaa ya utafutaji wa madini kwenye hatua mbalimbali za uendelezaji.

Tunafanya shughuli zetu kwa kuzingatia wajibu wetu kwa watu, mazingira na jamii ambayo inatuzunguka kama vitu vya msingi vya kutuwezesha tufikie malengo yetu.

ABG imesajiliwa kwenye Soko la Hisa la London (LSE) kwa kutumia alama ya ABG. Mnamo tarehe 7 Desemba 2011, ABG pia ilianza kuuza hisa zake kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).


Nector Pendaeli Foya,
Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano
Simu: (+255 22) 216 4229,
Barua pepe: nfoya@africanbarrickgold.com
www.africanbarrickgold.com



No comments:

Post a Comment