Nuzulack Dausen
WITO umetolewa kwa mwananchi yeyote mwenye taarifa za mali za
viongozi wa umma nchini kupeleka taarifa hizo kwa Kamishna wa Sekretarieti ya
Maadili ya Umma ili kusaidia zoezi la uhakiki wa rasilimali na madeni ya
viongozi hao.
Sekretarieti ya
Maadili ya Viongozi wa Umma inatarajia leo kuanza zoezi la uhakiki wa rasilimali
na madeni ya viongozi wa umma mpaka
tarehe 15 februari mwaka huu.
Hayo yamesemwa katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa juma
lililopita na Kamishna wa maadili ya viongozi wa umma Jaji Mstaafu Salome
Kaganda iliyoomba ushirikiano wa karibu kati ya wadau na Sektetarieti katika
kukamilisha zoezi hilo.
“Wito unatolewa kwa mwananchi yeyote mwenye taarifa za mali
za viongozi hao anaweza kuwasilisha taarifa hizo kwa kamishna wa maadili”
alisema Jaji Kaganda.
Zoezi hilo la uhakiki linatarajiwa kufanyika nchi nzima
ambapo litahusisha viongozi wote kutoka katika mihimili mitatu ya dola yaani
Serikali, Bunge na Mahakama.
“Wakati wa uhakiki
watendaji wa Sekretarieti ya Maadili watatembelea maeneo ziliko mali za
viongozi wakiwa na wathamini(valuers) ili kuthamini mali hizo kwa lengo la
kujiridhisha na usahihi wa taarifa za mali walizowasilisha kwa Kamishna wa
Maadili” alisema Jaji Kaganda.
Alisema taratibu zote za uhakiki wa rasilimali hizo
zilishafafanuliwa katika barua za viongozi ambao watahusika katika zoezi hilo
awamu hii.
Aidha, Jaji Kaganda aliwatahadharisha viongozi hao kuwaepuka
matapeli ambao wanaweza kujifanya ni watendaji wa sekretarieti ya maadili ili
kujinufaisha.
“Sekretarieti inawaomba wadau mbalimbali ushirikiano na pia
kuwakumbusha kuwa makini na baadhi ya watu wanaoweza kujifanya ni watendaji wa
sekretarieti ya Maadili kwa lengo la kujinufaisha” alibainisha Jaji Kaganda.
Aliendelea kusema kuwa endapo viongozi hao watakuwa na
mashaka juu ya mwenendo wa mtu yeyote wawasiliane na sekretarieti ya maadili
kwa ufafanuzi zaidi.
“Ieleweke wazi kwamba uhakiki ni zoezi la kawaida na
watakaohusika na uhakiki huo hawana tuhuma ya aina yeyote ile. Viongozi
wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa maafisa
wa sekretarieti wa uhakiki huo” aliongeza Jaji Kaganda.
No comments:
Post a Comment