WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji
Dk Mary Nagu jana aliongoza mamia ya wananchi katika matembezi ya hisani ya
kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana yaliondaliwa na mamlaka ya Elimu
nchini (TEA) na kudhaminiwa na Cokacola yaliyoanzia Mlimani city na kumalizika
viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Dk Nagu alichangisha
kiasi cha zaidi ya Sh 13 milioni na
kufanya jumla ya michango iliyokusanywa kuwa Sh 50 milioni ambayo inakaribia
kufikia lengo la kukusanya Sh 78 milioni ambazo zitasaidia ujenzi wa mabweni 30 ya shule 8 za Sekondari zilizochaguliwa
kuanza na mpango huo maalumu wa kuwasaidia watoto wa kike kutokana na kuwa na
mazingira magumu sana.
Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye matembezi
hayo Dk Nagu alisema kuwa ni kipindi kirefu sana watoto wakike wamekuwa
wakikosa elimu kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kihistoria kama
kunyimwa kusoma, ndoa na mimba za utotoni lakini serikali pamoja na wadau wa
elimu wameendelea kushirikiana kuhakikisha hali inabadilika kwa haraka.
Alisema kuwa
ili kuendelea kukabiliana na changamoto hizo vyombo husika na kila mtanzania
anahitajika kuchangia na kukemea vitendo vinavyorudisha nyuma maendeleo ya
elimu ya mtoto wa kike ili kutokomeza janga hilo.
“Natoa wito
kwa vyombo vinavyopaswa kuwachukulia hatua wahusika wa uharibifu huu watimize
wajibu wao wa kuhakikisha watoto wa kike wanapata haki yao ya kikatiba ya
kupata elimu bora bila kubughuziwa” alisema Waziri Nagu.
Aidha
aliwashauri wanafunzi wa kike kujidhatiti na kuacha kurubuniwa na vitu
vidogovidogo vinavyoweza kuwaharibia maisha yao ya baadaye na kuongeza kuwa ni
bora wakatumia muda wao wa masomo vizuri ili wasijutie hapo baadaye
watakaposhindwa kutimiza ndoto zao za kielimu.
Waziri Nagu
aliviomba vyombo vya habari kuhamasisha uchangiaji wa ujenzi wa mabweni hayo na
kusema kuwa watangaze na kuandika sana kama walivyoandika habari zake za
ushindi wa Nec.
Katika
matembezi hayo Waziri Nagu alichangia kiasi cha sh 1 milioni na kuahidi kuwa
atatumia muda wake wa wiki nzima
kuhamasisha uchangiaji zaidi wa ujenzi wa mabweni hayo ya wanafunzi wa
kike.
Vilevile
katika matembezi hayo walioambatana na Waziri Nagu ni Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii Lazaro Nyarandu na mke wake Faraja Nyarandu, Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka
ya elimu Dk Naomi Katunzi na Mabalozi wa
uchangiaji huo Msanii Barnaba na Rebeca Gyumi wakiongozwa na mwenyeji wao
Mkurugenzi Mkuu wa TEA Rosemary Lulabuka ambapo Naibu Waziri Nyarandu na
familia yake walichangia Sh 10 milioni.
Wakati huo
huo Mwanafunzi Hadija Nuru wa Shule ya Sekondari Baobab aliwaomba na kushauri TEA wapanue wigo wa uchangiaji
kwa kufanya bahati nasibu na kuongeza kuwa ujenzi wa mabweni hayo uambatane na
uwepo wa huduma za afya, maji, umeme na nyumba za walimu na kufanya ukarabati
wa majengo hayo kila wakati itakapohitajika
ili kuyadumisha zaidi.
Barnaba naye afunguka
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Barabas Elias naye alifunguka katika matembezi hayo na kusema kuwa wasanii waote wenye sauti kama yake waanze kujihusisha na masuala ya kijamii kama anavyofanya yeye kwa kuwa balozi wa kampeni za kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana.
Barnaba wa pili kutoka kulia akitumbuiza na wasanii wenzake wa THT wakati wa hitimisho la matembezi ya hisani ya kuchangia ujenzi wa mabweni. |
Alisema kuwa wasanii kama Diamond, Amin, Linna na wengineo wanaweza wakapanga muda wao japo kidogo kuchangia kidogo ili kuwasaidie wasichana ha waendelee na elimu zaidi.
Barnaba aliburudisha umati wa wanafunzi na wadau wengine waliokuwepo kwa kuipa nyimbo zake mabalimbali kama Magumegume, Sijutii niliyempata na zingine zilizotamba kwa vipindi vyote.
Hata hivyo Barnaba aliimba wimbo wa Linnah "angalau nina furaha" kama ishara ya kumshirikisha mwanamziki huyo kwenye ubalozi huo na pia kama heshima ya mtoto wa kike.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jangwani wakifuatilia shoo ya Barnaba. |
No comments:
Post a Comment