Thursday, October 13, 2011

Nyerere day iwe chachu ya mabadiliko Bongo

         Ijumaa ya tarehe 14 mwezi huu watanzania tunaadhimisha miaka 12 ya kifo cha Hayati baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere. Siku hiyo Watanzania hatutakuwepo makazini kwa kuwa ni siku ya mapumziko kitaifa. Hii ni siku maalumu kukumbuka kifo cha kiongozi huyu mahiri wa taifa la Tanzania. Siku hii tunahitajika kuzitafakari nasaha za hayati baba wa taifa huku tukimuombea astarehe kwa amani huko alikotutangulia.
Hayati Baba wa taifa Mwalimu Julius K. Nyerere  1922 - 1999
           
            Siku hii si ya kulewa baa au kufanya madhambi kama miongoni mwetu tunavyofikiri. Wengi hutumia siku hii ya mapumziko kwa mambo yao ya ajabu ajabu ambayo baba wa taifa aliyakemea sana kwa kuwa hayana tija katika taifa maskini kama hili. Wakati tukiadhimisha kifo hicho kuna baadhi  yetu wamepanga kutumia siku hiyo kujinufaisha wenyewe. Wapo watu ambao watatumia bajeti iliyopangwa kuwezesha maadhimisho hayo kama mitaji yao binafsi. Na wapo wengine watakao tumia siku hii kufanya mambo yao yasiofaa katika jamii ya kitanzania kama wizi, na masuala mengine ya uvunjifu wa amani.
     Umma wa watanzania lazima utafakari ni changamoto gani tunazipata tangu kuondokewa na kiongozi wetu shupavu JK I. Maadhimisho haya ya miaka 12 ya kifo cha baba wa taifa yanaambatana na maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania bara. Je Watanzania tunayaishi aliyotuachia mwalumu? Bila shaka kila mtu anajibu moyoni mwake basi hivyo ndivyo tunavyohitajika kutafakari zaidi ili kutoa mipango bora na endelevu ya kujenga nchi yetu na si ufisadi.
Ni matumaini yangu kuwa watanzania wengi wataitumia siku hii kutafakari kwa kina masuala yote aliyotuachia ba ba wa taifa kama njia moja wapo ya kujenga nchi, Hivyo basi Serikali ihakikishe usimamizi wa kutosha katika maadhimisho hayo. Nyerere day inatuhusu watanzania wote na inabidi tushirikiane kuendeleza kumbukumbu hizi ili zidumu vizazi na viziazi.
      Nawatakia mema katika maadhimisho haya ya kifo cha baba wa taifa!

       

Saturday, October 1, 2011

Uchaguzi mdogo Igunga: Ni patashika nguo kuchanika

Rostam Aziz mbunge wa zamani Igunga
      Ikiwa imesalia siku moja tu kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa mbunge katika jimbo la Igunga hali ya kisiasa bado haijakaa sawa. Mvutano wa kisiasa ni mkali sana na wenye changamoto nyingi kwa Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) pamoja na vyama husika vinavyoshiriki uchaguzi huo.
     Vyama mbalimbali vimejitokeza kushindania kiti hicho kilichoachwa na mbunge wa zamani wa jimbo hilo Bwana Rostam Aziz baada ya kujiudhuru nyazifa zote za kichama ndani ya CCM na kuwa mwanachama wa kawaida. Chama tawala CCM  kinatetea jimbo lake kwa kumsimamisha mgombea wake Dk. Dalali Kafumu huku CHADEMA nao wakimsimamisha mgombea wao bwana Joseph kashindye. Kwa upande wa CUF wamemsimamisha Bwana Leopold Mahona.
Mwananchi akijiandaa kupiga kura.
     Tangu kampeni za uchaguzi huo kufunguliwa mapema mwezi Septemba mwaka huu watanzania tumeshuhudia mengi kutoka Igunga.  Mengi kati ya hayo ni ya kusikitisha na hayafai kuwepo katika jamii ya leo. Wananchi wa Igunga wamejikuta wakipata mshikemshike wa kutosha kutoka kwa vyama vinavyowania Jimbo hilo. Moja ya matukio yaliogusa hisia za wengi ni kuchomwa  moto nyumba ya Bwana Hamis Makala  katibu wa CCM kata ya Nyandekwa. Tukio jingine la fedheha nikukamatwa kwa Mkuu wa wilaya ya Igunga Bi. Fatma Kimario na vijana wa CHADEMA katika Mkutano wa siri aliokuwa akifanya na watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM. 
      Si hayo tu, pia tumeshuhudia mengi kutoka Igunga ikiwemo tuhuma ya kada wa CCM kushikwa na majina  ya wapiga kura pamoja na shahada zao na mengine ni tuhuma za CCM kuandaa maninja 500  kwa ajili ya uchaguzi huku nao CHADEMA wakituhumiwa kuandaa Makomandoo 33 kudhibiti uchaguzi jimboni hapo. Vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo vimejikuta vikiingia katika malumbano yasio na tija kwa Wananchi wa Igunga. Kilichokuwa kikiendelea Igunga ni malumbano na si kutoa sera kwa watu wa Igunga.
     Licha ya matukio yote hayo bado umma wa watanzania unahitaji uchaguzi huru na wa haki Igunga. Wananchi wa Igunga hawatakiwi kurubuniwa katika kufanya maamuzi yao sahihi wakati wakichagua viongozi wao. Ikumbukwe kuwa safari ya mbwembwe zote za kampeni hizo inaishia leo hii na kesho tunahitaji utulivu, amani na upendo miongoni mwa watu wa Igunga. Naamini kuwa itikadi za kivyama zipo miongoni mwao lakini haziwezi zikawafanya wapigane au wavunje amani yao kwa sababu ya maslahi ya watu wachache.
Bwana Rajabu Kiravu, Mkurugenzi Mtendaji NEC
     Tume ya taifa ya uchaguzi na jeshi la polisi wanahitaji umakini na nguvu za ziada Igunga. Uchaguzi huu si lelemama kama wengi wetu tunavyodhani. Kama matukio makubwa kama hayo yameweza kutokea wakati wakampeni watashindwaje siku moja ya uchaguzi? Watanzania tumejifunza mengi sana Igunga na tunaendelea kujifunza zaidi. Mengi tuliyoshuhudia ni mifano ya ambayo hutokea wakati wa chaguzi nyingine ila huwa hatuyaoni na hatuyasikii sana kutokana na watu wote kuwa bize na uchaguzi na eneo kuwa kubwa tofauti na ilivyo Igunga.
     Japo uchaguzi huu mdogo wa Igunga unaandamana na chaguzi nyingine ndogondogo za Madiwani bado tume ya Uchaguzi ina changamoto nzito toka Igunga. Umma utambue kuwa karibia viongozi wote wa vyama vikubwa nchini wameweka kambi Igunga. Kila chama kikiwa na matumaini ya kushinda kiti hicho. 
     Naamini kuwa tume makini haiwezi kuacha uvunjaji wa sheria uendelee Igunga. Tume chini ya mwenyekiti wa muda Profesa Chaligha na Mkurugenzi mtendaji Bwana Rajabu Kiravu hawana chaguo zaidi ya kuhakikisha  kuwa uchaguzi ni wa haki, huru na wa amani. Tume haina budi kijivua gamba katika uchaguzi huu mdogo ili kutoa kashfa za uchaguzi mkuu uliopita. Binafsi ninayo imani kubwa na utendaji wa profesa Chaligha. Utaalamu wake katika masuala haya ya uchaguzi unaweza ukawa ni chachu ya kuleta mabadiliko katika uchaguzi huu. Umakini alionao mwenyekiti huyu si kidogo, ni umakini unamfanya kila aliyechini yake azifuate nyayo zake. 
Profesa Amon Chaligha Mwenyekiti wa muda NEC
      Iwapo Profesa Chaligha hataangushwa na Vijana wake basi uchaguzi utaenda sawa Igunga.  Namfahamu sana  Profesa tangu alipoanza kunifundisha masuala ya Sayansi ya Siasa  na Utawala pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Huwa hataki mchezo kabisa. Pia anao uwezo mkubwa wa kurekebisha mapungufu mengi yaliokuwepo tume ya uchaguzi. Lakini iwapo itakua kinyume na hayo basi hali ya Igunga hapo kesho ni patashika na nguo kuchanika.


      Mwisho, napenda kuwasihi wana Igunga kuwa kesho si siku ya kufanya makosa, ni siku ya  kutoa maamuzi magumu kwa kumchagua mtu anaewafaa kuwaletea maendeleo jimboni mwao na si ushabiki  wa vyama. Siasa ya kisasa na iliyokomaa haiendani na woga kwa vyama vya kisiasa kuwazia kushindwa au kukosa. Vyama shiriki katika uchaguzi huo havina budi kuwa makini katika masuala yote ya kiuchaguzi ili kuzuia tafrani hapo kesho. Nawatakieni uchaguzi mwema.
    Mungu Ibariki Tanzania, Mungu tubariki watoto wa Tanzania!