Thursday, February 12, 2015

Zawadi ya pekee kwa mke wangu mtarajiwa siku ya Valentine


Wasalaam kipenzi changu, mke wangu mtarajiwa.
Popote ulipo pokea salamu zangu hizi za dhati zisizo na tone la unafiki. Najua utakuwa umeshtuka kwanini nimekutumia barua hii leo, saa kadhaa kuelekea siku ya Wapendanao ambayo wazungu wanaiita Valentine. Usishtuke, nimekuletea zawadi yako maridhawa, kuwa mtulivu.
Tafadhari, usihudhunike kwa kuwa huna uhakika wa mpenzi au mume kwa sasa. Usisikitike na kujilaani kuwa una kasoro kwa kuwa wenzio wameshaanza pilikapilika za kuandaa au kupokea zawadi mahsusi za Valentine.
Inakuuma kutokuwa miongoni mwa hao thenashara lakini vumilia. Maisha sio maji ya mto yanayofuata mkondo wake. Maisha ni safari na waliombele ndiyo wanaowahi kufika bila kujali wamefika na kupata nini.
Bila shaka ulitegemea kupokea zawadi nzuri za maua mazuri ya waridi yaliyopulizwa manukato yenye rehe nzuri lakini kwa bahati mbaya ni haka kabarua ambako nimesahau kupulizia hata manukato ya ‘Nivea for Men’. Umakini wako kuisoma barua yangu kwa moyo ni zawadi tosha, zawadi nzuri kuliko hata Blackberry, Galaxy Note 4, Vits, IST au safari ya kutembelea visiwa vya Sanane na Zanzibar.
Najua masomo hayaendeki au kazi hazifanyiki huko uliko na unatamani siku ya Valentine iwe fupi, iishe na uachane na ‘mashida’ ya wenzio wanaoweka ‘status’ (ujumbe) mzuri na Selfie na wapenzi wao katika akaunti zao za Whatsapp, Instagram na Facebook.
Tuliza moyo na amini mimi nipo japo hatujawahi kuonana. Futa machozi na usiwaze kulazimisha penzi na mtu ambaye hakupendi, mimi nipo ila wasaa ulikuwa hauujafika wa kuanzisha uhusiano.
Naomba nisikuchoshe sana na maneno ya utangulizi yasiypunguza hata kidogo maumivu ya kovu la kuwa ‘single’ kwa sasa kwa sababu tu yule bepari mwenye gari uliyempenda alikuhadaa kuwa angekuoa lakini kumbe alikuwa na mke na watoto watatu. Au upo single kwa sababu tu vijana wanaoukuja bado hawajielewi au hawajaonyesa nia ya kukuoa na kukucheleweshea kamda kako ka kuolewa.
Simanzi hiyo ni ya muda mfupi. Hata usiumize kichwa kwa kuwamdogo wako wa pili  Rehema tayari ameshachumbiwa na wewe bado. Usipatwe na msongo wa mawazo ukialikwa kwenye harusi za rafiki zako kwa kuwa tu wote wanaolewa lakini wewe hata bado sijaonyesha nia ya kukutongoza. Hayo yote ni mapito. Majaribu. Ukiyashinda na kunisubiri nije utaishi maisha ya furaha na amani siku zote.
Lengo kubwa la barua hii mrembo ni kukujulisha kuwa mpango wangu wa kutaka uwe mama wa watoto wangu upo pale pale sijatoa hata nukta kupunguza uwezekano. Najua siku zinaenda pasina kuonana au kupata mawasiliano baina yetu kiasi cha kuruhusu matapeli wakurubuni, lakini hatma yake imekaribia.
Siku unayoisubiri inakaribia na hivi karibuni tu nitakuja au nitakupigia kukujulisha kuwa ndiyo mimi uliokuwa unanisubiri. Sitamung’unya maneno kukuleza nia yangu ya kukuoa wewe na hata sitapepesa pesa macho kukuangalia umbo lako, umaridadi au mavazi yako ili nipate nguvu ya kuzungumza, la ha sha.
Oooh, samahani mpenzi. Unajua utakuwa unashangaa tangu nimeanza kuandika waraka huu sijakutaja majina yale ya kidhungu ya Baby au Sweetheart. Naomba usifadhaike. Usifadhaike hata kidogo kwa kuwa wewe wangu ni wa asili ambaye hutaki kughushi maisha ndiyo maana sijahangaika kuangalia tamthilia za Maria Clara nipate maneno wanayotumia kwa kuwa najua huna muda wa kuziangalia. Na hata kama huwa unaangalia basi tu kwa kuwa ni mpenzi wa fasihi au familia yako kwa pamoja hupenda kuangalia lakini si kwa nia ya kuiga. Hapana shaka umenielewa.
Turudi kwenye ahadi ya kuonana siku chache ziajazo ili tuanze mchakato wa kuoana. Nilikuwa nakujulisha kuwa jiandae kupata ombi langu la kukutoa katika hali yako yako upweke na ili uushangaze ulimwengu kuwa mahusiano yote uliyokuwa nayo yalikuwa ni majaribio tu kama yale ya Vyuo Vikuu ya kutafuta alama za awali (Course Work) kabla ya vigongo vya mwisho (UE).
Lakini pamoja na kwamba tayari nimeshakuuma sikio juu ya mipango ya kukujia, Mahabuba wangu usikurupuke kwenda kwenye mitandao ya kijamii kuvujisha haka kasiri. Sitaki uanze kunivuta kwa picha zako za mitego ulizohariri na programu za Smartphones ili kuongeza umaridadi na rangi ili ung’ae kama jua la Saa nane. Sihitaji hata kidogo uanze kujibu jibu ujumbe unaotumiwa na wanaume Whatsapp au Facebook ukajua mimi ni miongoni mwao, utanikosa.
Ukikurupuka kujisalimisha na kujiregeza kwa wanaume katika Madaladala au mtaani unavyotembea ukitoka kazini, watakuhadaa sana. Jitahidi kupima mwonekano wa awali wa kila mwanaume (first impression) anayekuja moja kwa moja kukutongoza…mimi ntakuja kienyeji sana. Usinitose kwa sababu sitakuja na kogo za vijana wenzagu za oya oya.
Baada ya kunikubali sitakuwa na pupa za kujionyeha kwa kukupeleka kula Pizza au Burger Mlimani City, KFC au Quality Centre kwa kuwa najua wewe huigizi na unapenda kuishi maisha ya kawaida japo kwenu mpo vizuri. Hata tukitaka kuangalia filamu hutataka tukaangalie zile ambazo kiingilo ni Sh15,000 wakati mi nina televisheni yangu ya nchi 18 na DVD mbayo tunaweza kuangalia filamu za ndani nan je na kwa gharama ndogo tu ya kukatwa uniti za umeme.
Kwa kuwa ujio wangu ni wa kienyeji ndiyo maana nimekuandikia barua hii katika siku hii ya Valentine na wala sikutaka kukutumia picha ua ujumbe wa kwenye vifaa vya dijitali kama simu na kompyuta licha kwamba ninavyo.
Pia, nimekutumia ujumbe wangu mrefu kwa sababu najua unapenda kusoma na kujifunza vipya ikiwemo busara za mmeo mtarajiwa na hauwezi kuchoka kusoma navyoandika kwa sababu utaishi na mimi hadi kifo kitakapotutenganisha.
Mama watoto wangu mtarajiwa tulia, ondoa mawazo, usipate shinikizo la nyumbani la kuulizwa utaolewa lini kwa kuwa nimeshakutegulia kitendawili kuwa nakuja. Hudhuria tu harusi za wenzio na Sherehe za kuagwa huku ukiwa na matumaini kuwa yako inakaribia.
Wape moyo wenzio wanaonyanyasika na kuteseka katika ndoa zao kwa kuwa hawakuvumilia kusibiri na kufanya uchaguzi sahihi kama unavyonisubiri mimi. Wape pole na endelea kuwafariji kuwa  maono ya nje ya fedha, majumba na magari ni utatuzi tu mdogo wa maisha ya kufukarisha aliyejianzia mwadamu.
Waambie hayo yote yanaweza kwisha iwapo watawafunza wadogo zao kusubiri, kufanya uchaguzi sahihi na kutoparamia vinono na wakuige wewe kwani tukishaoana tu tuatawekeza kwenye kibubu vijipesa vyetu na kufanya biashara hadi kuwafikia wale. Kwa jinsi wewe ulivyo jembe, sidhani kama itachukua muda.
Pole mke wangu kwa kukuchosha kusoma maneno mengi sana katika msimu huu wa upendo. Japo, ni mengi nafsi yangu ipo huru ikiamini katika siku ya Valentine hutahudhunika, au kufadhaika kwa kuwa huna mpenzi, hayo ni mapito tu. Nisubiri nakuja.
Nikutakie kila la kheri na upokee ujumbe huu kama zawadi yako pekee ya Valentine.
Wako mumewe mtarajiwa na umpendaye
 Nuzulack Dausen.


Twitter: @nuzulack

No comments:

Post a Comment