Friday, November 30, 2012

UKUAJI WA UCHUMI NCHINI HAUTAWASADIA WATANZANIA-WADAU




UKUAJI wa uchumi nchini hautawasaidia  watanzania kutoka kwenye lindi la umaskini iwapo njia mbadala  hazitachukuliwa kudhibiti rushwa na  uhusiano usiosawia  baina ya serikali na sekta binafsi, imeelezwa.

Wakichangia mada kuhusu wajibu  wa sekta binafsi katika kupunguza umaskini Jijini Dar es salaam juzi, wadau mbalimbali wa maendeleo walisema kuwa jitahada za Tanzania kukuza uchumi wake hazitakuwa na msaada wowote kwa Watanzania katika kupunguza umaskini iwapo rushwa na  uhusiano hasi baina ya Serikali na sekta binafsi havitaondolewa.

Walisema kuwa uhusiano uliopo baina ya Serikali na sekta binafsi hauna usawa kwani sekta binafsi imekuwa na nguvu nyingi kuliko Serikali na kusababisha malengo na jitaha za  Serikali kupunguza umaskini nchini kutofikiwa ipasavyo.

Mwendesha Walsha ya kujadili wajibu wa Sekta binafsi katika jitahada za kupunguza umaskini Bakari Bujari (kushoto0 akiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa British Council Dkt Conor Snowden wakati wa uzinduzi wa Walsha hiyo Jijini Dar es salaam juzi.
Akizungumza katika mdahalo huo Afisa Mtendaji wa Taasisi ya kimataifa  isiyo ya Kiserikali ya  VSO  Marg Mayne alisema kuwa taarifa ya Benki ya Dunia inaonyesha Uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi lakini ukuaji huo umeshindwa kuwakomboa Watanzania wengi hususani waishio vijijini kutoka kwenye lindi la umaskini bali umeongeza tofauti kati ya maskini na matajiri.

Aliongeza kuwa ugunduzi wa gesi na mafuta nchini unaotarajia kukuza uchumi wa nchi kwa aslimia 6.5 hadi 7 hautaleta mabadiliko yoyote iwapo mfumo wa sasa wa uhusiano baina ya serikali na sekta binafsi hautavunjwa.
Alishauri uanzishwaji wa ushirikiano wa kina na ushawishi uliosawa baina ya wadau wa maendeleo na sekta binafsi ambao utaenda mbele zaidi ya sera ya Wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR) ili kuongeza mchango mkubwa wa makampuni katika jitahada za kupambana na kupunguza umaskini nchini.

Rananie Kunanayagam, Mkuu wa Utendaji wa Jamii Kampuni ya BG group alisema ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi si jambo jipya duniani kwani lilishakuwepo miaka 15 hadi 20 iliyopita katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania lakini umaskini bado upo palepale hivyo anahitajika mtu wa kusimamia uhusianobaina  ya Serikali na sekta binafsi.
“Kunahitajika uwepo wa mtu au taasisi katikati ya Serikali na Sekta binafsi ambaye hatang’ata upande wowote na kuwashawishi wote kutekeleza majukumu yao kwa usahihi” alibainisha Kunanayagam.

Mshiriki wa mdahalo wa kujadili wajibu wa Sekta binafsi katika jitahada za kupunguza umaskini nchini akitoa maoni juu ya mada hiyo juzi katika ukumbi wa British Council.Jijini Dar es salaam juzi.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa UNDP nchini Phillipe Poinsot alisema kuwa lazima kuwe na mgawanyo sawa wa wajibu baina ya Serikali na sekta binafsi katika kupambana na umaskini na pia Serikali izidishe uhusiano ndani ya Sekta binafsi.

Alisema kuwa Serikali ihakikishe inatengeneza miundombinu na mazingira rafiki kwa sekta binafsi kwa kutengeneza barabara safi, umeme wa uhakika, sheria thabiti, usimamizi mzuri wa rasilimali,  wasomi na viongozi  makini wasiopenda rushwa wakati huohuo  sekta binafsi ina wajibu wa kutoa kodi halali, uwazi katika uendeshaji, kuendeleza teknolojia na kutoa ajira stahiki kwa Watanzania.

Mjumbe wa Mdahalo huo Semkai Kilonzo alisema uwepo wa miongozo mingi inayohusika na jitahada za kupunguza na kupambana na umaskini kama MKUKUTA, Dira ya 2025, Kilimo Kwanza na mingine ni chanzo kikubwa cha ukuaji wa uchumi nchini kushindwa kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye lindi la umaskini.
“Uwepo wa Miongozo mingi kwa wakati mmoja  kama MKUKUTA, Mkurabita, Kilimo Kwanza kunachanganya Wadau wa maendeleo na pia imekuwa haina ushirikishwaji wa Wananchi katika kufanya maamuzi ya maendeleo yao hivyo inashindwa kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau” alisema Kilonzo.

Mdahalo huo Uliandaliwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya VSO International ikishirikana na BG Tanzania na British Council ambapo wadau walitaka rushwa itokomezwe,  uwazi wa utendaji katika makampuni na serikali, kuanzishwa kwa sera na sheria inayotoa kiwango na aina za miradi inayoweza kufanywa na makampuni katika Sera ya Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR).




No comments:

Post a Comment