Saturday, November 3, 2012

Vijana, Mafanikio hayaji kwa Kimbunga

IMEKUWA ni jambo la kawaida sana miongoni mwa vijana hivi sasa kuwa na mawazo ya kupata mafanikio makubwa bila ya kupigika. Vijana wengi wamejikuta wakipanga kuwa na vitu vingi vya thamani na nafasi za juu kiuchumi, kisiasa na kikazi wakati wakiwa mwanzoni mwa safari ya maisha.

Fikra sahihi za kuwa mafanikio hufuata hatua zimeshapotea kabisa, njia za mkatomkato zimekuwa suluhu ya kuharakisha mipango yetu kuelekea kwenye kilele cha mafanikio hata hivyo wengi wetu hushindwa kufikia malengo kama ilivyotarajiwa.

Ifahamike kuwa kila mtu ana mipango yake madhubuti ya kumletea maendeleo na kufanikisha mipango yake na matokeo mazuri ni tuzo ya jitihada zake, lakini swali hubaki ni njia zipi zimetumika kutimiza malengo hayo?

Kwa hali ilivyo sasa ukijaribu kufanya tathmini miongoni mwa vijana nchini utagundua kuwa wengi wanamipango mingi na ya juu sana ambayo si rahisi sana kutekelezeka kwa muda mfupi. Hali hii hufanya vijana wengi kuingia katika vitendo vya ujambazi, wizi , utapeli, uuzaji wa madawa ya kulevya, rushwa na hata kujiingiza kwenye vitendo vya kikahaba kwa wasichana na mambo mengi ambayo hayapaswi kuzungumzwa humu.

Tumeshuhudia hivi karibuni vijana wengi wenye mafanikio ya haraka na makubwa wakihusishwa na kujiingiiza kwenye mitandao ya Freemason na pesa za manyoka (uchawi). Na si tuhuma za magazetini tu bali vijana wengine wamesikika wakiulizia wapi wanaweza kuzipata huduma hizi ili wajiunge haraka wapate utajiri. Si ajabu sana kumkuta kijana akisoma kwa makini vibao vya matangazo ya waganga wakinigeria wanaotoa huduma za utajiri na kufaulu bila kusoma na kufuata huduma hiyo haraka bila kufikiri ukweli wake.

Mbali na kuzitafuta pesa kwa njia zisizo za halali pia imetokea tabia ya wanafunzi shuleni na vyuoni kutaka kufaulu bila kukaza msuli (kusoma). Tuhuma nyingi za wanafunzi kushirikiana na walimu kimapenzi ili wafaulu vizuri zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.Tabia hii inazidi kupamba moto kwenye baadhi ya vyuo vyetu nchini ambapo kuna warembo ambao hutumia muda wao kujiremba na kufanya starehe zao huku wakisubiri kujaziwa alama nzuri bila hata ya kuhudhuria vipindi, kufanya assignments na kujisomea kwa makini.

Nini chanzo cha tatizo hili?
 Mfumo uliopo wa utandawazi ukisukumwa na fikra na tamaduni za magharibi umekuwa chanzo kikubwa sana cha vijana wengi kutaka kufanikiwa kwa shortcut. Matumizi makubwa ya pesa kwa kununua magari ya kifahari, nyumba, mavazi na starehe nyingine vimekuwa chachu ya vijana kutafuta pesa kwa hali na mali kwa kutumia njia zisizo za halali kama nilivyoaainsha hapo juu. Imekuwa nikawaida kwa vijana wanaobahatika kuzipata pesa kwa njia ya halali kutokuzitumia vizuri kwa kuwekeza zaidi, wengi hutumia kwa starehe zao mbalimbali za kujirusha club na kubadilisha mavazi, warembo na magari.

Mfano mzuri unaweza kuupata kutoka kwa wasanii wetu wa bongo fleva na filamu waliobahatika kuzishika fedha kwa muda mfupi. Ukiwatembelea mpaka sasa wengine hawana hata viwanja vya kujenga na mambo mengine ya msingi. Baada ya kuchoka kiuchumi vijana hawa hutaka kurudisha hadhi yao ambapo njia mbadala za kutafuta pesa huanza zikiwemo za kusafirisha madawa ya kulevya.

Jambo jingine ni mfumo wa ufisadi unaoendelea kulitafuna taifa letu, baadhi ya vijana waliobahatika kupata kazi hujikuta wakiingia katika mfumo wa rushwa ili kujiongezea kipato cha haraka. Kwa sasa si ajabu sana kukuta vijana wengi wakitumia madaraka mbalimbali ili kupata mafanikio ya haraka kama mafisadi wanavyotafuna nchi.

Mfano mzuri ni kukithiri kwa rushwa ndani ya uchaguzi wa UVCCM, hawa ni vijana ambao kwa utashi wao walitoa rushwa ili wapate madaraka na wengine walipokea rushwa ili wapate kidogo kitu. Ni aibu kwa kijana kuuza utu wako kwa ajiri tu ya maslahi, mafanikio yapo ila hayaji kwa namna hiyo.Utajiuliza kulikuwa na umuhimu gani wa kutoa au kupokea rushwa katika uchaguzi huo zaidi ya kutaka mafanikio ya fasta? kama kusingekuwa na rushwa na kugombania madaraka makada hao vijana wasingetwishana makonde na kutembea na mabango kupinga matokeo kwa minajiri ya kuwepo kwa rushwa miongoni mwao katika uchaguzi huo.

Huo ni mfano tu wa njia ambazo vijana hutumia kupata mafanikio ya haraka. Mambo mengine ya wizi, ujambazi na ukahaba yamekuwa yakitumiwa na vijana wengine ambao hawajabahatika kupata elimu au nafasi katika siasa au nafasi mbalimbali za uongozi. tumeshuhudia vijana wengi wakipoteza maisha kwa ajili ya tamaa za mafanikio yasiopitia njia za halali. Wangapi wamekamatwa na madawa ya kulevya wakitumiwa na vigogo kuyasafirisha nje kwa ahadi nono za kujengewa nyumba za kifahari na magari? na wangapi wamechomwa moto wakijaribu kuiba pesa na vitu mbalimbali vya thamani?

Huo ni baadhi tu ya mifano inayoonyesha hali halisi ya vijana na maendeleokatika karne hii.

Nini kifanyike?
Kijana jiulize, mpaka sasa umepanga malengo gani ambayo kwa njia za halali yatakufikisha kwenye kilele cha mafanikio? Huu ni wakati ambao vijana wanatakiwa kukabiliana na changamoto za utandawazi kwa kutumia nafasi hiyo kama njia ya kupata mali halali hasa kwa kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia ubunifu na nidhamu ya hali ya juu. Usharobalo katika kutafuta pesa na kufanikisha mambo mengine hautakufikisha popote. Kijana sharobalo hawezi kukabiliana na matatizo magumu, hawezi kuthamini utu mbele ya pesa na mambo ya anasa na pia sharobalo mzembe si mbunifu wa mambo ya kumuingizia kipato kwa njia ya halali.

Siwaasemi vibaya mashrobalo bali nawapa njia sahihi za kutumia pesa na nafasi walizonazo ili waeze kuwekeza kwa siku zijazo na si kwa matumizi mabovu ya kukidhi haja za siku za soni tu. Sharobalo na Sharomalo wa ukweli ni yule anayeheshimu kazi na kujiwekeza katika mambo mbalimbali ya maendeleo yatakayo mpa heshima siku zijazo.

Kwa wakati huu wa utandawazi wenye ushindani katika mambo mbalimbali ya maisha vijana hawana budi kufuata busara za wazee na kukopi mambo mazuri ambayo vijana wengine wamefanikiwa. Kama upo shuleni au chuoni soma kadiri uwezavyo upate ufaulu wa halali na kama upo kazini fanya kazi kwa bidii upate promotions na offer kwa wingi na kama umejiajiari fanya kazi kwa bidii na nidhamu ya hali juu kuonegza kipato chako.

Funguuuuuka!



No comments:

Post a Comment