Sunday, April 12, 2015

Siasa zitaiangamiza Sumatra, sekta ya Uchukuzi

Moja ya vipindi vigumu kwa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) mwaka huu ni hiki inapotakiwa kufanya aumuzi wa kutangaza nauli mpya za usafiri wa umma.
Kwa kipindi cha miezi sita sasa mamlaka hiyo imekuwa aking’ang’anizwa na wadau na viongozi serikalini ishushe nauli kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Pamoja na Sumatra kupinga mara kadhaa kuwa mabadiliko yasingefanyika haraka kwa sababu mafuta hushuka na kupaa kwa muda mfupi, wadau hao wakiwemo Baraza la Kutetea Watumiaji wa Uchukuzi (Sumatra CCC) walizidi kuongeza presha ya kushusha nauli.
Sumatra ilishasisitiza kuwa bei ya mafuta inachukua sehemu ndogo tu ya vigezo vya ukokotoaji nauli mpya na zipo gharama nyingine za uendeshaji kama vipuri, bima, mishahara, kodi na mengineyo.
Ni dhahiri kuwa kwa zaidi ya miezi sita wamiliki wa daladala na mabasi ya masafa marefu walipata faida zaidi baada ya kushuka kwa mafuta pasina nauli kushuka na wananchi nao walinyimwa unafuu wa nauli ambao ungesaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Tofauti na miaka iliyopita, katikati ya mwaka jana hadi Machi mwaka huu mafuta yalishuka sana kiasi cha Petroli kufikia Sh1,650 jijini Dar es Salaam, bei ambayo ilifikiwa miaka minne iliyopita.
Baada ya mashinikizo, Sumatra ilianza kukusanya maoni ya wadau kama sheria inavyowataka ili kupata mitazamo tofauti ya kutekeleza zoezi hilo.
Katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam Machi 18, wamiliki daladala walipinga ushushaji nauli wakihofia mafuta yangepanda bei zaidi na wakatishia iwapo nauli itashushwa, wataanzsisha nauli kwa askari wa majeshi yote.
Wakati Sumatra ikiyafanyia kazi maoni na kufuatilia hali ya soko, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta wiki iliyopita aliigiza tena mamlaka hiyo kuharakisha majadiriano na wadau na kisha kutangaza nauli mpya ndani ya juma hilo. Hata hivyo, mpaka sasa nauli mpya hazijatangazwa.
Presha kama hizo ni changamoto na kipimo cha uweledi na ufanisi kwa mamlaka za udhibiti nchini. Kuna kila dalili pia kuwa Sumatra inahofia kufanya uamuzi huo isionekane ya ‘kijinga’ na isiyofuata uweledi kutokana na hali halisi ya soko dhidi ya siasa.
Kama Wachumi wengi walivyoonya awali, bei ya mafuta imeanza kupanda tena hata kabla ya nauli mpya kutangazwa. Petroli mwezi huu, Dar es Salaam inauzwa Sh103 zaidi ya bei ya Machi ya Sh1652. Dizeli imepanda kwa Sh109 na Mafuta ya Taa kwa Sh132.
Shilingi nayo imezidi kuporomoka kutokana na kuongezeka thamani ya Dola ya Marekani ulimwenguni na sasa Dola moja inabadilishwa kwa Sh1, 850. Vipuri na mabasi huingizwa nchini na wafanyabiashara wake huathiriwa sana na udhaifu wa thamani ya Shilingi.
Hali ya kisiasa mwaka huu inayohusiana na Uchaguzi Mkuu inaweza kuathiri mwenendo wa kiuchumi kutokana na wawekezaji wengi kuhofia hatari za kiuwekezaji na mabadiliko ya kiutawala yanayoweza kutokea.
Pia, kuna kila dalili bei ya mafuta ikazidi kupanda. Takwimu za Benki ya Dunia (WB) zinaonyesha wastani wa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia kwa mwezi Februari iliongezeka hadi Dola za Marekani 54.93 (Sh101, 600) kwa pipa kutoka bei ya chini kuliko zote kwa miaka mitano ya Dola 47.45 (Sh87,780) kwa pipa mwezi Januari mwaka huu.
Ripoti ya Machi, 2015 ya nchi zinazozalisha mafuta sana ulimwenguni (Opec) inaonyesha mahitaji ya mafuta duniani mwaka huu yataongezeka kwa mapipa 1.17 milioni kwa siku na kufanya wastani wa mahitaji ya jumla kwa siku kuwa mapipa 92.37 milioni. Hii itapandisha bei ya nishati hiyo licha ya Marekani na Canada kwa kuzalisha mafuta mepesi mengi zaidi kwa bei ndogo.
Kwa mantiki hiyo na ukiachana na siasa, uamuzi wa Sumatra kushusha nauli ni mtego usiofanana hata kidogo na kipindi cha mabadiliko ya nauli mwaka 2009.
Iwapo Sumatra italazimishwa, itaingia kwenye mgogoro na wasafirishaji na kuwapa wananchi ahueni ya muda mfupi tu.
Mfumo mzuri na wa haraka wa ukokotoaji nauli uendao na soko ni kama unaotumika na Ewura kukotoa bei ya mafuta kila mwezi. Huo ungewaepusha Sumatra na kadhia na presha za kisiasa.
Sumatra ingekuwa inapitia nauli angalau kwa miezi sita au mwaka kuepusha unyonyaji kama ulitokea hivi karibuni kwa wananchi kwa kushindwa kushusha nauli haraka kwa mujibu wa mwenendo wa soko la mafuta.
Nuzulack Dausen ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi anapatikana kupitia ndausen@tz.nationmedia.com au Twitter: @nuzulack






No comments:

Post a Comment